1.4 C
New York

TFS: Uvamizi maeneo ya hifadhi ni chanzo cha mabadiliko ya Tabianchi

Published:

*Wataalam waonya huku wakieleza inavyoathiri wanyama

Na Faraja Masinde, Gazetini

Mabadiliko ya Tabianchi ni tatizo linaliokabili Dunia katika karne hii ya 21 ambapo athari zake zimekuwa zikionekana katika nyanja mbalimbali zinazogusa maisha ya binadamu wa kawaida kila siku ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na mazingira kwa ujumla.

Wataalamu wanabainisha kuwa mabadiliko hayo ya tabianchi yamekuwa yanasababu mbalimbali nyuma yake ikiwa ni pamoja na vitendo vya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya misitu kwa ajili ya kujipatia kipato kupitia shughuli za uchomaji mkaa na upasuaji mbao.

Reuben Magandi-Afisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na uhaba wa maji kutokana na kukauka kwa vyanzo mbalimbali vya maji, majira ya msimu ya mvua kutotabirika maeneo mengi ya nchi, uharibifu wa miundombinu unaotokana na upepo mkali, mvua kubwa na mafuriko sambamba na ongezeko la magonjwa.

Reuben Magandi ni Afisa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo akizungumza Februari 15, mwaka huu mjini Bagamoyo katika Warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Amesema vitendo vya wananchi kuvamia maeneo ya misitu kwa shughughuli kama kilimo, uchomaji mkaa na upasuaji wa mbao imekuwa ni changamoto kubwa inayorudisha nyuma juhudi za TFS huku akitaja chanzo kuwa ni hali ngumu ya maisha.

“Sababu kubwa inayosababisha wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi ya misitu na kufanya ushughuli kama uchomaji mkaa, upasuaji mbao na nyingine ni umasikini ambapo mtu anaona kuwa ni njia rahisi zaidi ya kujipatia kipato,” amesema Magandi.

TFS inafanyaje kukabili hilo?

Magandi anasema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo wamekuwa wakiishirikisha jamii zinazozunguka misitu kupata njia mbadala ya kujipatia kipato.

“Changamoto kubwa inayosababisha uharibifu wa mazingira ikiwamo wananchi kukata kuvamia maeneo ya misitu ni hali ngumu ya maisha kwania wananfanya hivyo ili kujipatia kipato.

“Hivyo, tumekuwa tukiwawezesha kwa kuwapatia mbinu mbadala za kujipatia kipato ni pamoja na kuwagawia miche ya miti ikiwamo ya matunda kwa jamii zote zinazozunguka misitu asili.

“Pia tumekuwa tukiwapa mizinga kwa ajili ya ufugaji nyuki, mbinu hizi zote zinawasaidia wananchi kujipatia kipato pamoja na kutunza mazingira badala ya kukata miti kwa ajili ya mbao na mkaa, hivyo hii inakuwa inahamasisha zaidi wao kuwa walinzi wa mazingira badala ya kuharibu,” anasema Magandi.

Ameongeza kuwa miti ya asili inayosimamiwa na TFS inaendelea vizuri isipokuwa maeneo ambayo yana uvunaji mkaa.

“Maeneo ambayo bado yanachangamoto ni yale ambayo kuna uvunaji wa mkaa, hivyo TFS tunajitahidi kuhakisha kuwa uoto huo ulioharibika unarudishiwa kwa kushirikiana na wananchi,” anasema.

Athari zinamgusa kila mtu

Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Erikana Kalumanga anaeleza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinagusa hadi wanyama na kwamba mbinu za kupambana na changamoto hiyo pamoja na kuhifadhiwa vyema kwa shoroba ambako kutasaidia wanyama kupata maji kipindi eneo moja linapokuwa na ukame.

Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Erikana Kalumanga, akifafanua jambo wakati wa warsha hiyo.

“Moja wapo mikakati ya kupambana na mabadiko ya tabianchi tumejaribu kuangalia uwezekano wa kusaidiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kwamba maeneo ambayo ni mapito ya wanyama pori (shoroba) yanahifadhiwa ili wanyamapori wanapopata ukame sehemu moja basi wanaweza wakatembea kwenda eneo jingine kwa ajili ya kupata maji na marisho,” amesema Dk. Kalumanga.

JET na uwezo kwa waandishi

Awali, akizungumzia mchango wa warsha hiyo ya siku mbili iliyoshirikisha waandishi wa habari 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo amebainisha kuwa ni sehemu ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, akizungumza wakati wa warsha hiyo.

Amesema Mradi wa Tuhifadhi Maliasili ni wa miaka mitano na unalenga zaidi kushughulikia tishio la kutoweka kwa wanyama na viumbe hai nchini Tanzania.

“Kupitia mafunzo haya, waandishi wa habari wanapata maarifa, ujuzi na  mtazamo chanya wa kuripoti taarifa za uchunguzi kuhusu uhifadhi wa viumbe hai na mabadiliko ya tabianchi kwa usahihi zaidi.

“Hivyo, JET kwa kushirikiana na wadau wengine jukumu letu ni kuwajengea uwezo wanahabari katika eneo la uhifadhi wa shoroba ili kujua namna ya kuchunguza, kuripoti na kuchambua uhusiano wa wanyamapori, uhifadhi wa bahari na misitu, biashara haramu na ujangili sanjari na kukuza uhifadhi wa wanyamapori na masuala ya utalii,” amesema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img