21 C
New York

Visual| Watoto walivyoathirika na mafuriko Hanang

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Serikali inaendelea na uratibu wa shughuli mbalimbali baada ya maafa ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang wilayani Hanang mkoani Manyara, usiku wa Desemba 3, 2023.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, jijini Dodoma maporomoko hayo yameweza kusababisha vifo vya watu 89 hadi kufikia Desemba 11, 2023: Saa 10:30 jioni ambapo tayari miili 87 imeshatambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

Aidha, jumla ya majeruhi waliopokelewa tangu maafa yatokee ni 139 lakini waliopo hospitalini ni 17, wagonjwa 120 walisharuhusiwa kurejea nyumbani isipokuwa wawili waliofariki.

“Waathirika waliopo kwenye kambi tatu ni 224 baada ya wengine 98 kurejea kwa ndugu na jamaa zao. Kambi ya Shule ya Msingi Ganana ina waathirika 38, Shule ya Msingi Gendabi 131 na Shule ya Sekondari Katesh 55. Serikali inaendelea na juhudi za kuunganisha waathirika na familia zao na hatimaye kuzifunga kambi,” amesema Matinyi kupitia taarifa hiyo.

Athari kwa Watoto

Watoto ni kati ya makundi yaliyoathirika zaidi na janga hilo wilayani Hanang kwa namna tofauti tofauti ikiwamo kupoteza maisha, kujeruhiwa na kuathirika kwa namna nyingine ikiwamo kukosa masomo.

Mathalani taarifa ya Serikali iliyotolewa Desemba 9, inaonyesha kuwa watoto waliopoteza maisha walikuwa ni 36 ambapo kati yao wakiume ni 16 na wakike ni 20 idadi ambayo ni kubwa kwa ustawi wa taifa la kesho.

Mbali na vifo hivyo, watoto wengine 62 wakiwamo wakimume 28 na wakike 34 walikuwa ni sehemu ya watu waliojeruhiwa na mafuriko hayo huku watoto wengine 56 wakiwa wameathirika kutokana na janga hilo lililogharimu maisha ya watu.

Kukosa makazi

Kwa mujibu wa Serikali, hadi kufikia Desemba 6, kaya 1,150 zenye watu 5,600 zilikuwa zimepoteza makazi katika mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya Jorodom, Ganana, Katesh, Dumbeta na vijiji vya Gendabi, Sarijandu Arukushay na Sebasi.

Hii ni sawa na kusema kwamba ipo sehemu kubwa ya watoto ambao wameathirika na janga hilo kwa kukosa makazi na hata vifaa muhimu vya kujifunzia shuleni ikiwamo vitabu, madaftari, sare za shule na nyenzo nyingine muhimu za kielimu na hivyo kudhorotesha ustawi wao.

Kusitishwa kwa masomo

Kufuatia mafuriko hayo Serikali ilichukua uamuzi wa kuzifunga kwa muda shule ya Sekondari ya Katesha, shule ya msingi ya Gendabi na shule ya msingi ya Ganana ambapo kwa sehemu kubwa ndizo zilikuwa zinatumika kama kambi ya waathirika na hivyo kuathiri masomo.

Hakuna shaka kwamba jambo hili limeweza kuwaathiri watoto hawa kisaikolojia na hivyo mkazo unahitajika katika kuhakikisha kuwa wanasaidiwa kisaikolojia.

Ni habari njema kuona kwamba hadi Desemba 11, wataalamu wa afya ya akili wameshahudumia wananchi 1,370 kwa kuwapa ushauri nasaha.

Juhudi za Serikali

Kulingana na taarifa ya Serikali, bado kuna kazi zaidi inaendelea ikiwemo kusafisha barabara za mitaani na vijijini na nyumba za wananchi zilizojaa tope. Uchimbaji visima unaendelea wakati huduma za umeme, mawasiliano na usafiri barabara kuu ya Babati-Singida zikiwa zimesharejeshwa.

Wizara ya Afya hadi sasa imeshazitembelea kaya 3,993 na kutoa elimu ya afya pamoja na kugawa dawa 59,895 za kutibia maji.

Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu misaada fedha taslimu na vifaa kutoka kwa wahisani mbalimbali wa ndani na nje zikiwemo taasisi za umma na binafsi.

Hadi Desemba 10, jumla ya Sh 138,645,500/- zilishapokelewa kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa (National Relief Fund) iliopo Benki Kuu ya Tanzania, kando ya Sh 2,000,000,000/- alizokadhibiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwenye Ikulu ya Chamwino, Dodoma na Msajili wa Hazina, Desemba 10.

Kamati ya Maafa ya Taifa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imetoa akaunti ya benki ya kuweka fedha kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.

Akaunti hiyo ya kielektronikia ni National Relief Fund – Na. 9921159801 na swift code TANZTZTX kwa wanaotuma fedha kutoka nje ya nchi. Miamala inapotumwa inatakiwa kuwa na maelezo MAAFA HANANG. Akaunti hiyo ipo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na inapokea fedha kutoka ndani na nje ya nchi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img