1.7 C
New York

Visua| Hii ndiyo Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

NI Hifadhi iliyotawaliwa na ukimya mkubwa. Kelele zake utazisikia kupitia ndege tu wanaoruka kutoka tawi moja kwenda jingine wakijitafutia chakula chao cha kila siku.

Ndege hawa ni kama vile kolokolo domo refu ambao kwa mujibu wa watalaam kutoka ndani ya hifadhi hii ya pili kuanzishwa duniani, wako hatarini kutoweka na hivyo zinahitajika jitihada za makusudi kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwapo kwenye misitu hii ya kihistoria.

Upande mwingine utashuhudia mijongeo ya hapa na pale kutoka kwa watalii wa nchi mbalimbali wanaofika ndani ya hifadhi hii kwa ajili ya kujifunza mengi yaliyofichwa.

Kinyonga aina ya pembe tatu (three hornes chameleon) ambao hupatikana katika hifadhi ya Mazingira Asilia Amani tu.

Wapo wanaofika kufanya utalii wa vinyonga wa kuanzia pembe moja, mbili hadi tatu ambao wote wanapatikana ndani ya hifadhi hii.

Pia, wapo wanaofika kushuhudia Bundi pekee anayepatikana ndani ya hifadhi hii ambaye anajulikana kama Usambara Eagle Owl ambaye ana sifa kedekede za kipekee.

Aidha, ndani ya miti hii ambayo sehemu ya historia yake tunaelezwa kuwa kuna kila aina ya miti iliyokusanywa kutoka kote duniani na kuja kupandwa hapa enzi za ukoloni wa Mjerumani.

Hii ni sawa na kusema hata dawa za mitishamba zinapatikana kirahisi zaidi ndani ya hifadhi hii na ndiyo sababu baadhi ya wataalamu wa aina hiyo ya tiba wamekuwa wakitumia misitu hii kama sehemu ya kimbilio.

Je ni wapi huku?

Hii ni Hifadhi ya Asili ya Amani ambayo ilianzishwa ili kulinda mfumo wa kipekee wa ikolojia ya Mashariki mwa Milima ya Usambara iliyopo Mashariki mwa Tanzania.

Hifadhi hii ya viumbe hai ni makazi ya binadamu na spishi nyingine za kipekee zisizopatikana mahali pengine popote duniani.

Jamii zimejihusisha katika usimamizi wa hifadhi hii tangu ilipoanziashwa mwaka 1997.

Kwani wawakilishi wawili wa jamii ni wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Hifadhi ya Asili ya Amani. Utegemezi mkubwa wa jamii za kijadi katika maliasili zilizopo katika eneo hili kilikuwa ndicho kikwazo kikubwa katika kulifikia lengo la kuhifadhi msitu wa kipekee wa Amani.

Bodi ya Usimamizi wa Hifadhi imeanzisha jitihada inayolenga kuanzisha matumizi yasiyo ya ulaji wa maliasili hii na shughuli za kujiongezea kipato kama vile utalii wa mazingira, ufugaji wa nyuki samaki na vipepeo kabla havijapigwa marufuku na Serikali Machi 17,2016.

Kulingana na machapisho mbalimbali, Hifadhi ya Asili ya Amani ilitangazwa kisheria na Serikali ya Tanzania katika gazeti la serikali mwaka 1997, ikiwa na lengo la kuihifadhi bayoanuwai ya Milima ya Usamabara Mashariki.

Safu ya Mashariki ya Milima ya Usambara imeorodheshwa kama kituo cha kimataifa cha bayoanuwai ya mimea na inajivunia kuwa ya pili kwa kuwa na aina nyingi za mimea katika bara la Afrika.

Pia, ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuwa Hifadhi ya Binadamu na Viumbe hai, mwaka 2000. Hifadhi hii ya viumbe hai yenye eneo la takribani hekta 83,600 inajumuisha misitu ya mvua na ardhi ya nyasi na miti ya uwanda wa chini.

Ina sifa ya kuwa na mimea mingi iliyo katika hatari ya kutoweka (ikiwemo mimea mingi ya dawa) na ni makazi ya zaidi ya aina kumi na tatu za ndege wasiopatikana mahali pengine.

Pia misitu hii mikuu hutoa maji kwa wakazi zaidi ya 300,000 katika mji wa Tanga, na wenyeji wa milimani.

Kulingana na jeografia yake, hifadhi hii inaunganisha wilaya mbili za Muheza na Korogwe mkoani Tanga.

Hii ndiyo hifadhi ya Amani

Alphonce Nyululu ni Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Amani ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1997 kwa GN namba 151 kwa lengo kubwa la kulinda, kuhifadhi na kuhakikisha kwamba viumbe vyote au bayonuai zote zilizoko hapa zinahifadhiwa vizuri.

“Kuna vijiji takribani 20 vinavyozunguka hifadhi hii ambayo ndiyo tegemeo kubwa la maji kwa Jiji la Tanga kwani maji yote yanayotumika jiji la Tanga yanatoka ndani ya hifadhi hii.

“Hivyo, usipoweza kuhifadhi vyanzo vya maji huku unaua binadamu wote walioko Tanga, mfano mwaka jana (2022) mvua zilichelewa hivyo maji ikawa ni changamoto. Utaona kwamba maji yanayotililika huku kutoka mto zigi ndiyo yanapeleka maji Tanga ambapo Mamlaka ya Maji ya Tangauwasa wameweka mitambo yao,” anasema Nyululu.

Ndege zaidi 300

Nyululu anasema hifadhi hiyo ina shughuli mbalimbali ambazo zinachochea iendelee kuwa kwenye orodha ya hifadhi zinazopendelewa na watalii duniani.

“Kuna aina ya ndege zaidi ya 340 na kuna ndege mmoja anayepatikana ndani ya hifadhi hii aliyehatarini kutoweka anayefahamika kama Kolokolo domorefu.

“Huyu ndege tukicheza naye anaweza kutoweka ndiyo sababu utakuta kwamba kuna baadhi ya watafiti mablimbali wamekuwa wakifika hapa mara kwa mara kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanafanya utafiti wa ndege huyu ili asiweze kupotea,” anasema Nyululu.

Bundi wa Amani

“Huyu ni bundi anayepatikana ndani ya hifadhi hii tu na ndiyo sababu tumempatia jina la Usambara Egle Owl na amekuwa akivutia watalii wengi wanaofika hapa kwa ajili ya kumuona kwani ni wakipekee kutokana na mwonekano wake,” anasema Nyululu.

Ndege anayepima usafi wa maji

Nyululu anasema kwasasa wanafurahi kuona kwamba kuna baadhi ya viumbe vilivyopo ambavyo awali havikuwepo ndani ya hifadhi hiyo.

“Kwa hivi karibuni wamepatikana Kereng’ende au Amani Dragon Flies ambaye anapatikana ndani ya hifadhi hii na ukiona anapatikana basi ujue mazingira yako yamehifadhiwa vizuri kwani ndege huyu huwa anataga kando kando ya maji yaliyosafi tu, hivyo kwa namna nyingine hutumika kama kipimo,” anasema Nyululu.

Kereng’ende (Amani Dragonflies)

Dunia inaielewa Amani

Kulingana na Nyululu, hifadhi hiyo ndiyo ya kwanza kuanzishwa ikiwa na wadudu, wanyama wadogowadogo huku kidunia ikiwa ni ya 25.

“Hivyo, utaona kwamba dunia inatuelewa vizuri zaidi na ndiyo sababu tumetunukiwa ngao za mara kwa mara kutoka kwa wenzetu wa UNESCO ambao wamekuwa ndiyo kipimo kikubwa cha dunia kujua kuwa uhifadhi unaendelea kwa namna gani,” anasema Nyululu.

Kuna Night Walk

Nyululu anasema kuwa hifadhi hiyo pia ina utalii wa ikolojia ambapo watu mbalimbali wanafika kwa ajili ya kuangalia utalii wa ikolojia kwani kuna utalii wa vinyonga unaofanyika usiku maarufu kama Night Walk.

“Kuna utalii wa vinyonga wa pembe moja, mbili na tatu, kwa hiyo watu wanakuja usiku sababu vinyonga hawa hupatikana usiku, watalii wanakuja na kujionea maajabu haya yanayopatika hapa.

“Pia, wageni wanavutiwa na maporomoko ya maji ya Chemka Waterfalls na mengine, hivyo hili limekuwa likivutia watu wengi,” anasema Nyululu.

Mimea zaidi ya 1,000

“Tuna aneo jingine linaitwa Botaniko Garden lenye jumla ya hekta 340 lilianzishwa mwaka 1902 likikusanya mimea zaidi ya 1,000 kutoka kote duniani ikapandwa hapa na kufanyiwa majaribio ili iweze kupandwa sehemu nyingine.

“Wakati huo Wajerumani walikuwa wakivuna miti kwa ajili ya kuanzisha mashamba, hivyo walitaka kuvuna miti ili kuanza kupanda mazao mengine ya biashara.

“Lakini kila walilolianzisha lilishindikana, walianza na kahawa lakini haikufanya vizuri, hivyo wakaamua kuanzisha botaniko garden kwa kukusanya mimea mbalimbali duniani zaidi ya 1,000 ili kujua ni mimea gani ingeweza kustawi, na ndiyo sababu utaona kuwa Tanga inasifika kwa tiba asili,” anasema Nyululu.

Anasema kwa utajiri huo wa mimea ndiyo sababu hata Serikali NIMRI (Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini Tanzania).

“Hivyo utakuta kwamba hiyo mime ndiyo tiba na hata Uviko 19 ni muendelezo kutoka Uviko 17, pia kuna vikundi mbalimbali vya tiba asili ambavyo vimekuwa vikitumia mime hii kutoa tiba na watu wamepata watoto,” anasema Nyululu.

Anasema upandaji wa miti ya viungo kama iriki, mdarasini na vingine imekuwa ni moja ya nyezo muhimu inayosaidia kutunza mazingira kwani kilimo hicho hakihitaji kuongeza ukubwa wa shamba kila mwaka.

Faida ya Wananchi

Nyululu anasema kuwa wananchi wanapata faida kutokana na msitu huo kwa kupata asilimia kutoka katika mapato ya utalii inayotolewa kwa wanchi hao.

“Wanapata asilimia 20 ya fedha inayopatikana katika utalii unaofanyika, hivyo wamekuwa wakinufaika sana kupitia mpango huu, hii pia inachochea wananchi kuendelea kuwa walinzi wa msitu kwani ni wanufaika wakubwa,’ anasema Nyululu.

Mapato

Ukizungumzia takwimu za utalii wa hifadhi hiyo, Nyululu anasema kuwa: “Kutoka mwaka wa fedha 2017/18 hadi hadi 2022/23 hifadhi imepokea jumla ya watalii 14,096. Tukija katika mapeto tulikusanya jumla ya Sh 538,093,400 hadi Juni, mwaka huu,” anasema Nyululu.

Ndege ni kuvutio

Nyululu anasema kuwa watalii wengi wanaofika ndani ya hifadhi hiyo ni wanavutiwa na ndege hasa kolokolo domorefu ambapo huitwa kwa sauti ya kamera na kutua.

Ndege aina ya kolokolo domorefu ambaye yuko hatarini kutoweka.

“Kingine ni utalii wa usiku wa vinyonga, ambapo wengi wamekuwa wakipenda kuona vionyonga hawa wenye maajabu ya kipekee, hivyo pamoja na mazuri mengi yanayopatikana ndani ya hifadhi hii niwaite Watanzania waje watembelee kwani kuna vitu vingi vya kuvutia na kwa gharama nafuu,” anasema Nyululu huku akiongeza kuwa taifa la Ujerumani ndilo kinara kwa utalii.

Akizungumzia ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, amesema imekuwa ni fursa nzuri kwa wanahabari kutembelea misitu ya Amani Nilo kwani wamejifunza mambo mengi, ikiwamo umuhimu wa kutunza na kulinda ndege ambao wako hatarini kutoweka.

“Tulikuja kwenye Hifadhi ya Misitu Asilia ya Amani Nilo na tumejionea vivutio mbalimbali ambavyo vinawavutia watalii na havipatikani kokote duniani. Tumeona baadhi ya ndege ambao wameainishwa katika dawati la IUCN kuwa wako hatarini kutoweka, lakini hapa wanapatikana.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo.

“Hivyo, kuna umuhimu kwa waandishi wa habari kutembelea eneo hili ili kuhabarisha umma wa Watanzania kuhusu vivutio hivi. Pia, kazi kubwa inayofanywa na wadau mbalimbali wakiwamo USAID kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili, kuhakikisha eneo hili linabaki katika uhalisia wake,” amesema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img