22.9 C
New York

Infographic|Nini hatima ya Afghanistan chini ya Taliban

Published:

WIKI iliyopita, wachambuzi wa masuala ya kiusalama nchini Marekani walionya, wakisema zimebaki wiki chache tu Kundi la Taliban kurudi madarakani nchini Afghanistan.

Ikumbukwe kuwa angalizo hilo lilikuja wakati wanajeshi wa Taliban wakielekea kuuteka Mji Mkuu, Kabul, baada ya miji mingine 18 kuwa chini yao ndani ya muda mfupi.

Jumapili ya wiki iliyopita, Taliban wakauteka rasmi Mji Mkuu huo, Kabul, ikiwa ni miaka 20 tangu walipoondoshwa madarakani na wanajeshi wa Marekani walioingia Afghanistan.

Licha ya wanajeshi wa Serikali ya Afghanistan kupewa mafunzo na mataifa ya kigeni, hasa Marekani, walizidiwa kete na wapiganaji wa Taliban, hali iliyomfanya Rais Ashraf Ghani akimbie.

Kuiweka mkononi Kabul kulikuja siku chache tu tangu Taliban ilipoweza kuishikilia miji mingine 18, ikiwamo Lashkar Gah, Hirat, Kandahar, Tirin Kot, Feroz Koh, Qalat, Zaranj, Herat, Ghazni, Aybek, Kunduz, Taleqan, Farah.

Hali hiyo ya ubabe wa Taliban imewafanya Marekani kupeleka kikosi cha wanajeshi 5,000 ikielezwa kuwa wanakwenda kuwalinda Wamarekani walioko huko Afghanistan.

Ni nani hao Taliban?

Hicho ni kikundi kilichoundwa mwaka 1994 na kiliingia madarakani kuiongoza Afghanistan mwaka 1996. Msimamo wa Taliban ulikuwa ni kuitawala nchi hiyo kwa misingi ya Dini ya Kiislam.

Chini ya utawala wa Taliban, taasisi ya Waislam wa Dhehebu la Suni, wanawake hawakuruhusiwa kusoma, kufanya kazi, na kusafiri wenyewe (pasi na kuongozana na mwanaume). Pia, hakukuwa na ruhusa kwa yeyoye kutazama runinga, kusikiliza muziki na kusherehekea Sikukuu zisizo za Kiislam.

Marekani kuingia Afghanistan

Utawala wa Taliban ulianguka baada ya Kituo cha Biashara cha Marekani kushambuliwa katika tukio maarufu la Septemba 11, 2001, ambapo watu zaidi ya 2,700 walipoteza maisha.

Kwa uchunguzi wa Marekani, ilionekana kuwa shambulio hilo lilitekelezwa na Osama bin Laden, kiongozi wa Al Qaeda ambalo ni Kundi lililokuwa likishirikiana na Serikali ya Taliban.

Vikosi vya Marekani vikatua nchini Afghanistan, lengo likiwa ni kuzuia Al Qaeda isiendelee kuitumia Afghanistan kama kambi ya kutekeleza matukio ya kigaidi.

Marekani ilipofanikiwa kuing’oa Serikali ya Taliban lakini huo ukawa mwazo wa vita iliyogharimu maisha ya raia wa Afghanistan takribani 111,000, huku wengine 400,000 wakilazimika kuyakimbia makazi yao.

Nani nyuma ya Taliban?

Kundi hilo linaongozwa na Mawlawi Haibatullah Akhundzada, mmoja kati ya viongozi wa Dini ya Kiislam. Alianza kuiongoza Taliban mwaka 2016, baada ya aliyekuwa kiongozi, Mullah Akhtar Mohammad Mansour, kuuawa katika shambulio la Marekani.

Ukiacha huyo, pia yumo Mullah Abdul Ghani Baradar, miongoni mwa waanzilishi wa Taliban. Huyo ndiye kiongozi wa Kamati ya Siasa kwenye Kundi hilo na hivi karibuni alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi.

Kwa upande mwingine wa Kundi hilo, linatajwa kuwa na wapiganaji wanaofikia 100,000.

Taliban walizungumza nini na Trump?

Mwaka 2017, Taliban walimwandikia barua Donald Trump, wakati huo akiwa ndiyo kwanza ameingia madarakani kuiongoza Marekani. Walimtaka kuondosha majeshi yake nchini Afghanistan.

Yakawa ni mazungumzo yaliyochukua miaka mingi na hatimaye mwaka jana pande mbili hizo (Marekani na Taliban) zikasaini mkataba wa kumaliza ‘uadui’ wao wa tangu mwaka 2001.

Katika mkataba huo, Marekani ikakubali kuondosha majeshi ya kigeni, sambamba na kuachia wapiganaji wa Taliban 5,000 waliokuwa gerezani. Kwa upande wao, Taliban wakakubali kuwa watailinda Afghanistan dhidi ya vikundi vyote vya kigaidi.

Majeshi ya kigeni yalianza kuondoka, ikiwamo Uingereza, huku Marekani ikirejesha nyumbani sehemu kubwa ya wanajeshi wake na kubakiza 650 tu walioko sasa.

Umoja wa Kujihami wa nchi za Magharibi (Nato) nao uliondosha vikosi vyake na kwa sasa ni wanajeshi 13,000 waliobaki kusaidia harakati za kudhibiti matukio ya kigaidi.

Hata hivyo, baada ya kuona majeshi ya kigeni yamepunguza nguvu, Taliban ilionekana kuzidisha kasi ya kuteka maeneo hadi ilipofanikiwa kuuweka chini ya himaya yao Mji Mkuu, Kabul.

Hasara waliyopata Marekani

Kwa haraka, vita hii imeonekana kuigharimu zaidi Marekani, tofauti na Afghanistan na mataifa mengine ya kigeni, ikiwamo Uingereza. Mathalan, wanajeshi wake zaidi ya 2,300 wameshapoteza maisha tangu walipoingia Afghanistan mwaka 2001.

Aidha, Marekani imetumia zaidi ya Dola Trilioni moja tangu ilipoanza kupambana na Taliban katika mahitaji kivita, chakula, dawa, nguo na posho kwa wapiganaji.

Taliban walivyomponza Biden

Kwa Rais wa Marekani, Joe Biden, ukosolewaji umekuwa mkubwa tangu Taliban walivyoiteka rasmi Kabul. Kwanini aliondosha majeshi yote ya Marekani nchini Afghanistan? Hilo ndilo swali analoulizwa kila kona kwa sasa.

Katika majibu yake, Biden aliyeingia madarakani miezi michache iliyopita, amesema wanajeshi wa Serikali ya Afghanistan waliwezeshwa vya kutosha kupigana na Taliban lakini walizembea katika mapambano hayo.

Biden akaongeza kuwa utawala wake ulitekeleza tu lakini makubaliano ya kuondosha wanajeshi yalishafanywa na mtangulizi wake, Trump, alipokutana na Kundi la Taliban.

Hatima ya Afghanistan chini ya Taliban

Taliban wamekuwa wakijaribu kuziaminisha jumuhiya za kimataifa kuwa wamebadilika, kwamba wanaweza kuiongoza Afghanistan bila sheria kali walizokuwa nazo awali. Katika hilo, wanasema wako tayari kuwa na Serikali itakayoshirikisha raia, pia wakiahidi kuzilinda haki za wanawake.

Msemaji wa Taliban, Sohail Shaheen, anasema wanawake wataruhusiwa kuendelea na masomo. Pia, Shaheen anasisitiza kuwa hakutakuwa na marufuku ya kuwapo kwa wanadiplomasia, waandishi wa habari na asasi za kiraia.

Juu ya hilo, dalili zimeanza kuonekana. Mosi, ni kitendo cha uhusiano wa karibu kati ya Taliban na China. Ikumbukwe, China walilitaja kuwa ni Kundi la Kigaidi mwaka 1996 lakini safari hii ni pande mbili zinazoonekana kuwa na ukaribu.

Pili, Uturuki imejitosa kuhakikisha Afghanistan inakuwa salama hata baada ya Taliban kuchukua nchi. Hatua ya Uturuki kuzungumza na vyama vyote vya siasa, ikiwamo Taliban, ni dalili kuwa mambo yanaweza kuwa mazuri.

Lakini, wadadisi wa mambo wanaona hali ikiwa tofauti. Wanaamini Taliban watarudisha utawala wa kibabe waliokuwa nao wakiwa madarakani kuanzia mwaka 1996-2001.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img