Bajeti mpya ya Serikali tayari imeanza kutumika tangu Julai 1, mwaka huu, huku sehemu ya bajeti hiyo ikiwa ni makusanyo kupitia kodi za wanananchi kwenye nyanja mbalimbali.
Bila shaka umewahi kutamani kufahamu namna Serikali inavyotumia fedha yako unayochangia kupitia kodi.
Gazetini imekuchambulia maeneo muhimu ambayo ni kipaumbele cha Serikali kwenye bajeti hiyo ambayo ni ya kwanza tangu Rais Samia Suluhu alivyoshika madaraka ya kuiongoza Tanzania kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Bajeti ya mwaka huu ni Sh trilioni 36.33.
Katika maelezo yake, anasema kiasi cha Sh trilioni 23 kinatarajiwa kutumika kwenye Matumizi ya Kawaida, huku Sh trilioni 13.33 kikitumika kwa ajili ya Maendeleo.
Matumizi ya Kawaida
Katika matumizi ya maendeleo, Sh trilioni 10.66 kinatumika kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, huku Sh trilioni 8.15 kikitumika kwa ajili ya malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma.
Aidha, Sh trilioni 4.19 ni kwa ajili ya matumizi mengine, huku Sh bilioni 200 kikitengwa kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni na watoa huduma.
Kwa mujibu wa Dk. Nchemba, deni la Taifa limeongezeka na kufikia Sh trilioni 60.9 kutoka Sh trilioni 55.43 mwaka 2020/21.
Matumizi ya Maendeleo
Kwa mujibu wa Dk. Nchemba, katika mgawanyo wa fedha za maendeleo Sh trilioni 2.34 ni kwa ajili ya kuigharamia miradi ya umeme, likiwamo bwawa la Mwalimu Nyerere.
Sh trilioni 2.08 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara, huku Sh trilioni 1.19 ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR).
Aidha, Sh bilioni 589.4 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, Sh bilioni 500 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na Sh bilioni 400 ni kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa.
Pia, kiasi cha Sh bilioni 312.1 ni kwa ajili ya kugharamia elimu ya msingi, Sh bilioni 233.3 zikitengwa kwa ajili ya kugharamia dawa na vifaa tiba huku bilioni 215.6 ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi.
Katika fedha hizo za miradi ya maendeleo, Sh trilioni 10.37 ni fedha za ndani na Sh trilioni 2.96 ni fedha za nje.