Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) nchini Tanzania wamekutana kujadili mikakati ya kuimarisha uendelevu wa mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini.
Majadiliano hayo yalifanyika Mei 21, 2025, katika Ofisi Ndogo za TACAIDS jijini Dar es Salaam, yakiwa na lengo la kuweka misingi ya kimkakati ya kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya UKIMWI yanadumu kwa muda mrefu kupitia mifumo ya ndani yenye uwezo na stahimilivu.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Catherine Joachim, aliishukuru CDC kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika kuimarisha uratibu wa kisekta wa mwitikio wa UKIMWI hapa nchini.
“Ili kuhakikisha uendelevu wa mafanikio tuliyoyapata katika mapambano dhidi ya UKIMWI, tunahitaji mifumo imara na stahimilivu ya utoaji wa huduma. Ushirikiano wetu na CDC ni muhimu katika kuweka misingi madhubuti ya uendelevu,” ameema Dk. Joachim.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CDC Tanzania, Dk. Mahesh Swaminathan, ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikifaidika na misaada ya kifedha na kitaalamu kutoka CDC kwa kipindi kirefu. Hata hivyo, alisema kuwa wakati umefika kwa nchi kuandaa mazingira ya kujitegemea katika mwitikio wa UKIMWI.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa huduma bora za VVU na UKIMWI zinatolewa kwa wote kwa njia endelevu, kupitia mifumo ya kitaifa. Tunaamini kuwa kupitia ushirikiano wa karibu na taasisi kama TACAIDS, Tanzania inaweza kufikia hatua ya kujitegemea katika mwitikio wake,” amesema Dk. Swaminathan.
Mkutano huo umetajwa kuwa ni sehemu ya juhudi endelevu za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kutokomeza maambukizi mapya ya VVU, kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI, pamoja na kupambana na unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na VVU.