22.9 C
New York

Visual| Ufahamu mradi wa kusambaza gesi asilia-Mini LNG

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Tanzania inaendelea kuchukua hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.

Hatua hiyo pamoja na mambo mengine itasaidia kuokoa mazingira na maisha kwa kiasi kikubwa, kwani takwimu zinaonesha takribani Watanzania 32,000 kila mwaka wanapoteza maisha kutokana na kutumia nishati chafu kupikia.

Kulingana na takwimu hizo hii ina maana kwamba kila mwezi Watanzania takribani 2,600 wanapoteza maisha au unaweza kusema kwamba watu 88 kila siku wanafariki dunia.

Katika kulidhibiti hilo ifikapo mwaka 2033 kama ilivyobainishwa katika mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) limesaini mkataba wa awali wa makubaliano ya uwezeshaji wa kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi na uendelezaji wa mradi mdogo wa gesi kimiminika (Mini LNG), itakayosambazwa mbali na maeneo yaliyopita mabomba ya gesi.

Makubaliano ya ubia uliyoingiwa Mei 17, 2024  kati ya TPDC, Rosetta na Africa 50 kwa uwekezaji katika mradi wa Mini LNG utaleta suluhu ya ufikishaji gesi asili katika maeneo ambayo bomba la nishati hiyo bado haijafika.

Ikumbukwe kuwa ndani ya mkakati huo ambao ni wa miaka 10, Rais Samia anataka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza chachu kufikia malengo yake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kuingia mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC,  Mussa Makame amesema kumekuwa na changamoto ya kufikisha gesi  asilia iliyoshindiliwa (CNG) na gesi asilia inayopita kwenye mabomba katika maeneo ya mbali, kwa sababu ya kukosekana kwa uwekezaji mkubwa ambao ungesambaza gesi nchi nzima.

“CNG unapoipeleka mbali zaidi ya kilomita 400 au 500 kiuchumi bei ambayo unakwenda kuuza inakaribia gharama ya kueneza,  ili kuitatua changamoto ya kutoeneza mabomba nchi nzima tumeamua kuingia makubaliano na wenzetu,”amesema Makame.

Katika utekelezaji wa mradi huo amesema utakuwa wa mafanikio hautahakikisha tu upatikanaji wa mapema wa gesi asilia kwa viwanda, kaya na magari bali utatangaza enzi mpya ya ufanisi wa nishati na uendelevu  wa matumaini makubwa  kwa sekta ya nishati nchini.

Huo ni mkataba wa pili kusainiwa kati ya TPDC na wawekezaji binafsi kwa ajili ya uwekezaji katika mradi wa Mini LNG baada ya ule uliotiwa saini Januari 2024 na KS Energy.

Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi TPDC, Paul Makanza  amesema  kusainiwa kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu kwani inaendana na mipango yao ya kuongeza usambazaji wa gesi asilia kufikia mikoa mingi hapa nchini. Zaidi angalia usanifu wetu kufahamu zaidi kuhusu mpango huo wa kusambaza gesi kwa wananchi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img