Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wafanyabiashara wa betri chakavu kuzingatia kanuni na maelekezo waliyopewa katika vibali vyao ili kuhakikisha biashara hiyo haileti madhara kwa mazingira na afya ya binadamu.
Ushauri huo umetolewa leo, Oktoba 22, 2024, jijini Dar es Salaam na Meneja wa Uzingatiaji wa NEMC, Hamad Taimuru, alipokuwa akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC katika semina iliyoandaliwa na Asasi ya AGENDA kwa kushirikiana na NEMC pamoja na Taasisi ya Utafiti ya Oeko-Institut ya Ujerumani kwa ufadhili wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ).
Taimuru amesisitiza kuwa biashara ya kukusanya betri chakavu ina umuhimu wa kiuchumi, lakini ni lazima ifanyike kwa kufuata sheria ili kuepuka madhara.
“Tunawasihi jamii kuacha kumwaga asidi ovyo kwenye mazingira. Wafanyabiashara wanapaswa kukusanya betri na kuzipeleka kwenye viwanda vilivyopata vibali vya kuchakata betri hizo na kuhakikisha asidi na plastiki zinashughulikiwa ipasavyo,” amesema.
Kukusanya betri kwa usalama
Akiendelea kufafanua, Taimuru alieleza kuwa wakusanyaji wa betri chakavu wanapaswa kupata vibali maalum vya ukusanyaji na usafirishaji wa betri hizo ili kuzipeleka viwandani kwa ajili ya urejelezaji wa salama. Aliongeza kuwa NEMC imekuwa ikiendesha mafunzo kwa wadau mbalimbali ili kuboresha utaratibu wa urejelezaji wa betri chakavu nchini Tanzania.
“Lazima tuangalie kwa makini asidi kutoka kwenye betri hizi chakavu inapelekwa wapi. Asidi hiyo ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu. Ikiingia kwenye maji au kudhuru wanyama, inaweza kusababisha madhara makubwa kama vile magonjwa ya figo na ubongo,” alionya Taimuru.
Semina ya wadau wa urejelezaji wa betri chakavu
Semina hiyo ililenga kujadili njia bora za urejelezaji wa betri chakavu, na ilihusisha wadau kutoka sekta mbalimbali. Wadau walibadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa taka hatarishi kama vile betri, ambapo viwanda vilivyohusishwa katika semina hiyo vilieleza changamoto wanazokutana nazo.
Moja ya hoja kubwa iliyojadiliwa ni upokeaji wa betri ambazo hazina asidi, jambo ambalo linazua swali la wapi asidi hiyo inapelekwa. “Hili ni tatizo linalopaswa kufuatiliwa kwa sababu limegundulika kuwa betri nyingi zinazokusanywa mitaani zimekuwa zikipokewa viwandani zikiwa hazina asidi, hali inayohatarisha afya ya jamii,” alisema.
Madhara ya kumwaga asidi ovyo
Taimuru aliendelea kusisitiza kuwa madhara ya kumwaga asidi kwenye mazingira ni makubwa, na NEMC itachukua hatua kali kwa wale wanaokiuka sheria. Aliwahimiza wakusanyaji wote kuhakikisha wanapata vibali halali na kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni ili kulinda mazingira na afya za wananchi.
“Tunatoa wito kwa wanaofanya biashara hii bila vibali waache mara moja. Ofisi zetu ziko wazi katika kanda zote nchini, na mchakato wa kupata vibali ni rahisi. Tunataka wote wafanye biashara hii kwa usalama na kwa mujibu wa sheria,” alihitimisha.
Kwa pamoja, semina hiyo ilifikia makubaliano ya kutoa mwongozo wa kitaifa utakaosaidia kuimarisha usimamizi wa betri chakavu na kuhakikisha mazingira na afya za wananchi zinalindwa dhidi ya madhara ya taka hatarishi.
Akizungumza kuhusu warsha hiyo, Afisa Programu Mkuu wa AGENDA, Silvan Mng’anya, alisema kuwa mafunzo hayo yamepokelewa kwa mwamko mkubwa kwani yamebainisha mapungufu yaliyokuwepo katika udhibiti wa bidhaa hizo.
“Mafunzo haya yatasaidia wazalishaji kuboresha shughuli zao za urejelezwaji wa betri chakavu. Ujumbe muhimu ni kuhakikisha tunaboresha au kupunguza sumu kwenye mazingira yetu kwa ujumla ili kuepuka athari zinazotokana na madini haya hatarishi,” alisema Mng’anya. Aliendelea kufafanua kuwa wanapanga, baada ya warsha hiyo, kubaini kiwango halisi cha betri chakavu zinazosambazwa.
Awadh Milasi, Meneja Mradi wa GIZ nchini Tanzania, amesema kuwa GIZ kama kampuni ya shirikisho inayohusika na ushirikiano wa kiufundi inaunga mkono utekelezaji wa miradi endelevu duniani kote.
Nchini Tanzania, GIZ inatekeleza mpango wa kukuza ajira kwa wanawake kwa ajili ya mabadiliko ya kijani barani Afrika (WE4D), ambao ni mradi wa kikanda unaolenga kukuza ajira na kuboresha hali ya kiuchumi ya wanawake katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hususan katika sekta zinazochangia mabadiliko ya kijani.
Mpango huu unapata ufadhili kutoka Wizara ya Shirikisho la Ujerumani ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ), Umoja wa Ulaya (EU), na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Norway (Norad).
Hii inatoa uhusiano wa moja kwa moja na miradi mingine ya uchumi wa mzunguko na usimamizi wa taka za kielektroniki inayotekelezwa na taasisi ya Oko Institut e.V., hivyo kuleta ushirikiano wa asili kwa lengo la kuhakikisha athari pana zaidi ndani ya sekta hiyo.