Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeitaka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu, huduma za kinga, matibabu na matunzo kwa wavuvi wanaoishi katika maeneo ya maziwa na bahari.
Hii ni baada ya kubaini kuwa kiwango cha elimu ya kujikinga na VVU miongoni mwa wavuvi bado ni cha chini, huku upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI ukiendelea kutokidhi viwango vya kuridhisha.
Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika leo Oktoba 22, 2024 Bungeni jijini Dodoma, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Christina Mzava, alisema maambukizi ya VVU kwa wavuvi bado ni tatizo kubwa, ambapo kiwango cha maambukizi kipo juu kwa asilimia 7, ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa.
Amesisitiza kuwa TACAIDS inahitaji kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu na huduma katika maeneo ya mialo ili kukabiliana na hali hiyo.
“Lazima tuongeze kasi katika kutoa elimu ya kujikinga na VVU, pamoja na huduma za kinga, matibabu, na matunzo kwa jamii za wavuvi, ambao kwa sasa wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU. TACAIDS inakazi kubwa ya kuhakikisha huduma hizi zinawafikia kwa ufanisi wavuvi walio kwenye maziwa na bahari,” amesema Dk. Mzava.
Wajibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Samweli Mwashamba, aliwasilisha taarifa kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega. Amesema Wizara hiyo inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za VVU, UKIMWI, na magonjwa sugu yasiyoambukiza kwa mujibu wa waraka wa Utumishi wa Umma wa mwaka 2014.
Mwashamba alieleza kuwa hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na ujumuishaji wa masuala ya VVU na UKIMWI katika sera ya Uvuvi ya mwaka 2015, kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa afua hizo, pamoja na utoaji wa lishe, elimu, na upimaji wa hiari kwa watumishi wa Wizara na wavuvi.
“Wizara pia imeanzisha vituo vya upimaji na ushauri nasaha kwa wavuvi, huku ikisambaza makasha 30 ya kuhifadhia kondomu na kondomu 334,872 kwenye maeneo ya kazi ya Wizara katika kipindi cha mwaka 2023/24,” ameongeza Mwashamba.
Changamoto za maambukizi kwa wavuvi
Mwashamba amebainisha kuwa sababu kuu zinazochangia kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU kwa wavuvi ni pamoja na matumizi yasiyosahihi ya kondomu, imani potofu juu ya matumizi ya kondomu, na uelewa mdogo kuhusu VVU na UKIMWI.
Hali hiyo imechangiwa zaidi na upatikanaji hafifu wa huduma za afya katika maeneo ya mialo, hususan kwenye visiwa.
Amesema kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI katika mialo, kwani asilimia 51 ya huduma hizo zinapatikana katika mialo 1307 pekee. Pia, aliainisha kuwa sensa za wavuvi zinaendelea ili kuweka mikakati bora ya utoaji wa huduma hizo.
Elimu na huduma kwa watumishi wa Wizara
Katika kipindi cha mwaka 2023/24, jumla ya watumishi 387 wa Wizara walipatiwa elimu ya VVU na UKIMWI pamoja na ushauri nasaha na vipimo. Aidha, Wizara ilitoa lishe na nauli kwa watumishi waliojulikana kuishi na VVU ili kusaidia afya na ustawi wao.
Kamati hiyo ya Bunge ilihitimisha kwa kuhimiza TACAIDS kushirikiana zaidi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuongeza nguvu za kutoa huduma bora za VVU na UKIMWI kwa jamii za wavuvi ili kupunguza kiwango cha maambukizi kwenye sekta hiyo muhimu.