2.6 C
New York

DCEA inavyodhibiti kilimo cha bangi Mara

Published:

*Wananchi wakubali yaishe

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA), ikishirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, ikiwa ni pamoja na jeshi la polisi na jeshi la akiba, imeendesha operesheni kubwa na ya kihistoria kwa muda wa wiki tatu katika wilaya za Tarime na Serengeti, mkoani Mara. Lengo la operesheni hiyo ni kukabiliana na tatizo la uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya, hususan bangi, katika maeneo hayo.

Operesheni hiyo ilihusisha vijiji vya Matongo, Nyarwana, na Weigita katika bonde la Masinki, pamoja na vijiji vya Nkerege, Kembwe, Nyakunguru, na Iseresere kwenye bonde la mto Mara.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema kuwa jumla ya ekari 3,007.5 za mashamba ya bangi zimeteketezwa, kilogramu 7,832.5 za bangi kavu na kilogramu 452 za mbegu za bangi zilikamatwa, huku watuhumiwa 17 wakiwekwa kizuizini.

“Operesheni hii ni sehemu ya jitihada za kulinda jamii yetu dhidi ya madhara ya dawa za kulevya,” alisema Kamishna Lyimo, akiongeza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha vita dhidi ya bangi.

Mamlaka imebaini kuwa kilimo cha bangi mkoani Mara kinafadhiliwa na raia wa nchi jirani, ambao huwapa wakulima mitaji na baadaye kusafirisha bangi hiyo kwa masoko ya nje. “Tunatoa miezi mitatu kwa wananchi kuachana kabisa na kilimo cha bangi. Tutarejea kwa nguvu zaidi na kuhakikisha maeneo haya hayatumiki tena kwa kilimo cha bangi,” alisisitiza Kamishna Lyimo.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alikiri kwamba changamoto ya kilimo cha bangi bado ipo, lakini serikali inafanya jitihada za kutoa elimu na kuchukua hatua kali ili kukabiliana na hali hiyo. “Tumeanza kutoa elimu juu ya madhara ya bangi, na wengi wameahidi kuachana na kilimo hiki,” alisema Meja Gowele.

Mwita Mataro, afisa wa maji kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria, alieleza kuwa kilimo cha bangi kinasababisha uharibifu wa vyanzo vya maji katika mto Mara, na mipango ipo kuhakikisha kuwa sheria za rasilimali za maji zinaheshimiwa. “Kilimo haramu cha bangi hakiruhusiwi ndani ya mita 60 kutoka mtoni,” alisema Mataro, akiongeza kuwa hatua za kuhifadhi mazingira zinachukuliwa.

Aidha, vijiji vya Nkerege na Kata ya Kiore vilifanya uamuzi wa kushirikiana na DCEA kufyeka mashamba ya bangi. “Wakina baba, mama na vijana wameamua kuwa bangi haitalimwa tena kijijini,” alisema Diwani wa Kiore, Rhobi John, huku akiwasihi wananchi kutoa taarifa pindi wanapobaini uhalifu huu.

Mzee Julius Zakaria Matiku, mwenyekiti wa mila wa ukoo wa Wasweta, alieleza kuwa wamekubaliana kutokomeza kilimo cha bangi, huku wakitafuta mazao mengine mbadala kama vile mahindi na maharage. “Kijana atakayekamatwa akilima bangi atatozwa faini ya ng’ombe watano,” alisema mzee Matiku, akihimiza kufuata sheria na kulinda maadili ya kijiji.

Operesheni hiyo ni sehemu ya jitihada za kitaifa kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa huru dhidi ya dawa za kulevya. Hivyo, wananchi wanahimizwa kupiga vita biashara hii haramu ili kuimarisha afya na amani ya taifa.

Soma pia: https://gazetini.co.tz/2024/05/20/visual-hali-ya-dawa-za-kulevya-nchini-mwaka-2023/

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img