22.9 C
New York

TAWA yaitumia Sabasaba kutoa fursa za uwekezaji

Published:

Na Beatus Maganja, TAWA

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetoa wito kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia.

TAWA imeamua kutumia maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Kibiashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam kuhamasisha wafanyabiashara wa ndani na wageni kutoka mataifa mbalimbali kufanya uwekezaji wenye tija.

Akizungumza na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, Afisa Utalii Daud Tesha amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika mamlaka hiyo.

Tesha alibainisha kuwa maeneo yanayofaa kwa uwekezaji ni pamoja na utalii wa picha katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA), uwindaji wa kitalii, na ufugaji wa wanyamapori.

“TAWA imetenga maeneo kadhaa kwa ajili ya kufanya shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo, ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya kumi yanayotoa burudani safi kwa watalii,” amesema Daud Tesha.

“Maeneo mengine ni Pori la Akiba Wamimbiki, Tabora ZOO, Ruhila ZOO, na Makuyuni Wildlife Park, ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii, ikiwemo kujenga kambi za kulala wageni (campsites), hosteli, loji, na maeneo ya mapumziko mafupi kwa watalii (picnic sites),” ameongeza Tesha.

Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja.

Kwa upande wake, Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda la TAWA ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.

“Kama kaulimbiu ya maonesho haya inavyosema, ‘Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji,’ natumia fursa hii kuwaambia Watanzania wote kuwa TAWA ni taasisi sahihi kwa biashara na uwekezaji, kwani inatoa fursa za uwekezaji wa aina mbalimbali kama vile ujenzi wa loji, kumbi za mikutano katika maeneo yetu, kambi za watalii, michezo ya watoto, na pia uwekezaji katika mashamba ya wanyamapori na bustani za wanyamapori,” amesema Maganja.

“Hii ni fursa adhimu kwa wawekezaji wote kutembelea banda letu ili waweze kupata ufafanuzi wa fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi yetu,” ameongeza Maganja.

Maonesho haya yenye kaulimbiu “Tanzania ni Mahali Salama pa Biashara na Uwekezaji” yalianza Juni 28, 2024 na yanatarajiwa kufikia tamati Julai 14, 2024.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img