11.3 C
New York

TTB kuboresha maeneo ya Uhifadhi wa Nyuki kwa Shughuli za Utalii

Published:

Na Grace Mwakalinga, Gazetini-Morogoro

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imeanza mikakati ya kuboresha maeneo yote nchini yenye uhifadhi wa nyuki na kuwekea utaratibu maalum kwa ajili ya shughuli za utalii. Hatua hii inakuja baada ya Tanzania kutambuliwa kama moja ya nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa asali bora duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru, alisema katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Morogoro, kwamba wataainisha maeneo yote yenye uhifadhi wa nyuki na kuboresha mazingira kwa ajili ya watalii.

“Tuna kazi kubwa ya kueleza ulimwengu juu ya vivutio tulivyonavyo na ili watalii wavutiwe kuja kujionea, ni lazima tuboreshe miundombinu yetu, kuanzia barabara hadi vivutio vyenyewe, hasa haya mazao mapya ya utalii ambayo tumeweka utaratibu wake,” alisema Mafuru.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele, alisema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa maonesho ya nyuki duniani yatakayofanyika mwaka 2027 jijini Arusha. Hii ni kutokana na ubora wa asali inayozalishwa nchini, ambapo sampuli 70 zilizochukuliwa kutoka wilaya 34 zilionyesha kiwango cha juu cha ubora duniani.

Mapepele aliongeza kuwa zaidi ya watu 6,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kushiriki katika maonesho hayo, ambayo yatajumuisha shughuli mbalimbali zinazohusiana na utalii wa nyuki.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img