1.6 C
New York

“MITI KWA UMRI”: Birthday yako inaweza kuiokoa Tanzania na mabadiliko ya tabianchi

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini-Pwani

Katika kuhakikisha Taifa linakabiliana na mabadiliko ya Tabianchi Watanzania wametakiwa kupanda miti kwa wingi hasa wanaposherehekea siku zao za kuzaliwa.

Hayo yamesemwa na Brigedia Jenerali Mstaafu Martin Amos Kemwaga, ambaye pia ni Mkurugenzi wa MAKMar Hoteli iliyopo katika Kata ya Msata Wilayani ya Bagamoyo mkoani Pwani na mwasisi wa kampeni ya “MITI KWA UMRI”-KIJANI KIRUDI Wakati wa Bonanza la Kurudisha Kijani lililofanyika katika hoteli hiyo Juni 16,2024.

Brigedia Jenerali Mstaafu Martin Amos Kemwaga(kushoto), ambaye pia ni Mkurugenzi wa MAKMar Hoteli iliyopo katika Kata ya Msata Wilayani ya Bagamoyo mkoani Pwani akimkabidhi mche wa mti Diwani wa Kata ya Msata, Selestin Semiono, wakati wa Bonaza la Kurudisha Kijani.

Lengo la Bonanza hilo la Kurudisha Kijani lililoshirikisha vikundi mbalimbali vya Jogging kutoka ndani na nje ya mkoa wa Pwani lilikuwa ni kuazimisha miaka mitano tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya MITI KWA UMRI iliyozinduliwa Oktoba 7,2019 na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete.

“Leo Juni 16, 2024 tunafurahi kwamba kampeni yetu ya MITI KWA UMRI imetimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, hivyo ndiyo sababu tukaona tuandae Bonaza hili la KURUDISHA KIJANI kwa kushirikisha vikundi vya Jogging ambavyo vimeungana na kikundi chetu hapa kufanya mazoezi lakini pia kupanda miti 200 katika eneo hili la Hoteli ya MAKMAr,” amesema Brigedia Jen. Kemwaga.

Aidha, akizungumzia kampeni hiyo ya MITI KWA UMRIkijani irudi, Brigedia Jen. Kemwanga ambaye ambaye hadi sasa amepanda zaidi ya miti 500 katika eneo hilo la Msata, amesema kuwa baada ya kutafakari umuhimu wa mazingira na changamoto za mabadiliko ya tabianchi alibaini kuwa mbinu pekee yakuweza kurejesha uoto wa asili ni kupanda miti kwa wingi.

“Kampeni ya MITI KWA UMRI inalenga kupanda miti kulingana na umri wako mfano; kama una umri wa miaka 50 utapanda miti 50,  mwaka ujao utapanda miti 51 kwa kufanya hivyo ninaamini Tanzania itakuwa ya kijani, kikubwa katika hili miti utakayopanda siku ya kuzaliwa kwako utakuwa unawajibika nayo katika kuitunza, tumeona miti mingi ikipandwa katika kapeni mbalimbali lakini haina utunzaji matokeo yake inakauka na kufa.

“Kwa kuzingatia kuwa kila siku kuna Mtanzania anayezaliwa, niliona fursa ya kuunganisha sherehe za siku za kuzaliwa na upandaji miti. Watu hushirikisha ndugu na marafiki kusherehekea siku hizi. Sasa, kama tutasherehekea kwa kupanda miti, tutakuwa na sababu nyingi za kuitunza, matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 yanaonyesha kuwa tuko Watanzania milioni 64 hivyo wote yukiamua kutumia birthday zetu kuazimisha kwa kupanda miti basi Tanzania itakuwa ya kijani na tutarejesha uoto wetu wa asili,” amesema Brigedia Jen. Kemwaga.

Brigedia Jenerali Mstaafu Martin Amos Kemwaga, ambaye pia ni Mkurugenzi wa MAKMar Hoteli iliyopo katika Kata ya Msata wilayani ya Bagamoyo mkoani Pwani na mwasisi wa kampeni ya “MITI KWA UMRI”-KIJANI KIRUDI akimwagilia maji mche baada ya kuupanda wakati wa Bonanza la Kurudisha Kijani lililofanyika katika hoteli hiyo Juni 16,2024.

Mariam Vicent ambaye ni msimamizi wa Hoteli ya MAKMar amesema kampeni hiyo imekuwa na mafanikio makubwa hatua ambayo imeweza kuwavutia hata wageni wanaofika katia hoteli hiyo kuomba kupanda mti.

“Tulipata wazo la kupanda miti kila tunapofikisha umri wa kitu flani, kampeni hii imekwenda mbali zaidi na sasa imekuwa na manufaa makubwa kwa wanajamii wakiwamo wa mkoani Pwani. Ukiacha hilo, hata wageni wanaofika hapa hotelini tumekuwa tukiwafahamisa juu ya utaratibu huu na wote wanauunga mkono, kuna watu kutoka nchi zaidi ya 10 wamefika hapa na kushiriki kupanda miti na mara kwa mara wanapopata nafasi wamekuwa wakifika hapa kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya miti yao huku wengine wakipiga simu kwa njia ya video kuonyeshwa maendeleo ya mti wao.

“Hata hivyo, linalotupa moyo zaiosi sisi kama wana MAKMar nikuona kwamba kwa sasa jamii imeiga utaratibu huu kila wanapotimiza miaka kadhaa ya kuzaliwa basi wanajitahidi kupanda miti kulingana na umri huo kadri mtu anavyoweza, tunajivunia sana hili,” amesema Mariam.

Lenin Festo Paul, Afisa Misitu kutoka Wakala wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (TFS) mkoa wa Pwani, amesema wanaunga mkono kampeni hiyo kwa sababu inachochea utunzaji wa mazingira na kuimarisha misitu nchini. “Hii ni kampeni ya kuigwa kwani inachochea utunzaji wa mazingira. TFS tumetoa miche 200 bure kwa ajili ya kupandwa hapa kama kielelezo cha kuunga mkono kampeni hii. Watanzania wengine waige kampeni hii kwani itasaidia kutunza mazingira,” amesema Paul.

Mmoja wa wananchi walioshiriki kampeni hiyo, ambaye pia ni mdau wa mazingira katika eneo hilo la Msata, Selestine Semeni, amesema kuwa “MITI KWA UMRI” ni kampeni inayopaswa kuwa endelevu kwani inachochea hali nzuri ya hewa. “Kampeni hii inapaswa kuwa ya kitaifa kwani inamgusa kila mtu. Tunampongeza sana Brigedia Jen. Kemwaga kwa kuja na kampeni hii kwani tunasherehekea siku za kuzaliwa kila mwaka. Ikiwa tutachukua mtazamo huu wa kupanda miti kulingana na umri unaofikisha, itasaidia jamii yetu kutunza mazingira,” amesema Semeni.

Diwani wa Kata ya Msata, Selestin Semiono, akipanda mti kwa niaba y Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, katika bonanza hilo.

Kibinda Kibinda, Mwanachama wa Amka Fitness Club ya jijini Dar es Salaam, amesema kuwa elimu hiyo ya kupanda miti ni muhimu kwani hakuna michezo bila kuwa na mazingira mazuri. “Niwahamasishe wenzetu wote kuwa tusitumie muda mwingi kukimbia tu bali tunaweza sasa kuanza kuiga kampeni nzuri kama hizi kwamba tunaweza kutunza afya huku tukitunza pia mazingira kwa kupanda miti hasa tunaposherehekea kumbukumbu zetu za kuzaliwa,” amesema Kibinda.

Upande wake Diwani wa Kata ya Msata, Selestin Semiono, ambaye alimwakilisha Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ameupongeza uongozi wa MAKMar Hoteli kwa kuandaa bonanza hilo na kwamba wao kama kata wanajivunia na kuona fahari kwa uwepo wa watu wanaohamasisha utunzaji wa mazingira.

“Hili ni jambo la kujivunia sana kwetu wana-Msata na Chalinze kwa ujumla kwani linachochea utunzaji wa mazingira na tunatamani kuona kampeni hii ikienea sehemu kubwa zaidi kwani Mkoa wa Pwani ndio umekuwa mhanga mkubwa wa ukutaji miti kwa ajili ya uchomaji mkaa lakini urejeshwaji wake umekuwa wakusuasua,” amesema

Kampeni ya “MITI KWA UMRI” ni njia bora ya kuunganisha sherehe za siku ya kuzaliwa na jitihada za kulinda mazingira. Kwa kupanda mti kila unapotimiza mwaka mmoja zaidi, tunachangia katika kutunza mazingira na kuacha urithi mzuri kwa vizazi vijavyo. Hii ni njia ya kipekee ya kuadhimisha maisha yetu huku tukitunza dunia.

Baadhi ya Washiriki wa Bonanza hilo wakishiriki katika zoezi la upandaji miti.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img