1.4 C
New York

Maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua-TACAIDS

Published:

*….yadhamiria kupunguza zaidi

Na Faraja Masinde, Gazetini

Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 7 hadi kufikia asilimia 5, lengo likiwa ni kufikia chini ya asilimia 4. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Jerome Kamwela, alieleza hayo Juni 7, 2024, jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandiishi wa habari kuhusu hali ya maambukizi mapya ya VVU kwa vijana wa kike.

“Tumeanza mbali katika kuhakikisha tunatokomeza maambukizi hayo, na matarajio yetu ni kufikia asilimia 4, hali itakayoonesha tumefanikiwa kuondoa au kutokomeza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto,” amesema Dk. Kamwela.

Ameongeza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI zina imani kwamba malengo hayo yatafikiwa, kwani kiwango cha kufubaza virusi katika jamii kipo asilimia 1 chini ya lengo la kidunia.

Kulingana na TACAIDS, idadi ya maambukizi mapya ya VVU nchini imeendelea kupungua kutoka watu 72,000 mwaka 2016/2017 hadi kufikia watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023, idadi inayolingana na punguzo la asilimia 16. Hata hivyo, kiwango cha maambukizi mapya kwa kundi la vijana wa kike wenye umri wa miaka 15 hadi 24 kimeongezeka kutoka asilimia 0.14 mwaka 2016/2017 hadi asilimia 0.33 mwaka 2022/2023.

Dk. Kamwela alitaja visababishi vya kuongezeka kwa maambukizi hayo kwa wasichana kuwa ni pamoja na kutokuwa na uelewa wa kutosha wa mbinu za kujikinga, ndoa za utotoni, kufanya ngono zembe, utandawazi, tamaa, umaskini, na kujihusisha na wapenzi zaidi ya mmoja.

Utafiti wa viashiria vya VVU na UKIMWI mwaka 2022/2023 unaonesha kuwa kiwango cha ushamiri wa VVU kitaifa ni asilimia 4.4, ambapo kwa wanawake ni asilimia 5.6 na kwa wanaume ni asilimia 3.0. Hii inamaanisha kuwa Watanzania takribani 1,548,000 wanaishi na maambukizi ya VVU. Umri wenye kiwango kikubwa cha ushamiri kwa wanaume ni miaka 50-54, na kwa wanawake ni miaka 45-49.

TACAIDS kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza afua mbalimbali zinazowalenga vijana wa umri wa miaka 15-24 waliopo shuleni na wale walio nje ya shule, ili kuwapatia elimu ya stadi za maisha na kuondokana na ushawishi unaoweza kupelekea kupata maambukizi.

“Afua hizo ni pamoja na zile zilizotekelezwa kwa kuwahusisha vijana balehe na wanawake kupitia mradi wa Timiza Malengo wa DREAMS, ili kuwapatia elimu ya VVU na UKIMWI, afya ya uzazi na stadi za maisha. Wasichana walio nje ya shule wamewezeshwa kiuchumi na kuwa salama,” alisema Dk. Kamwela.

TACAIDS pia inatekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuhakikisha kuwa vijana wanapata elimu sahihi na kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU.

“Tunashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha tunafikia malengo ya kupunguza maambukizi na hatimaye kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” aliongeza Dk. Kamwela.

Kwa ujumla, Serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakifanya juhudi kubwa katika kupambana na maambukizi ya VVU nchini Tanzania. Hatua hizi zimeonyesha mafanikio, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa hasa kwa vijana wa kike, ambao wameonekana kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi mapya. Serikali inaendelea kuimarisha mikakati yake na kushirikiana na wadau ili kuhakikisha kuwa malengo ya kupunguza maambukizi yanatimia.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img