1.6 C
New York

Dk. Biteko awaasa wananchi wa Bukombe Matumizi ya Pori la Kigosi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, mkoani Geita, amewataka wananchi wa jimbo hilo kuwa na subira wakati serikali inaandaa utaratibu maalum wa kutumia Pori la Kigosi kwa shughuli mbalimbali. Dk. Biteko alitoa wito huu Juni 6, 2024, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa soko la zamani, Kata ya Igulwa, Jimbo la Bukombe.

“Watu wema wa Bukombe, naomba niwakumbushe historia ya Pori hili la Kigosi lenye ukubwa wa mita za mraba 13,000 ambalo lilikuwa Hifadhi ya Wanyamapori. Wakati nachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hili, kulikuwa na mgogoro kati ya hifadhi na wananchi, hasa wafugaji wa nyuki waliokuwa wakizuiwa kuingia porini,” alisema Dk. Biteko. Aliongeza kuwa alimweleza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu changamoto hiyo, na hatimaye pori hilo lilishushwa hadhi na kuwa Hifadhi za Misitu za Taifa.

Dk. Biteko aliwaambia wananchi kwamba Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Hifadhi za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, alifika kusikiliza kero zao. Hata hivyo, aliwasihi kuwa na subira kwani mchakato wa kuweka utaratibu rasmi unaendelea. “Nimewaeleza Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa Ardhi waje hapa kuwaeleza utaratibu ni upi,” alisema Dk. Biteko.

Aidha, Dk. Biteko aliwaonya wananchi wa Bukombe dhidi ya kuingia katika pori hilo bila kufuata utaratibu, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaovunja sheria. “Uhai wa Watanzania una thamani kubwa, hivyo wananchi wanaoingia huko bila kufuata utaratibu wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na washitakiwe,” alisisitiza.

Pamoja na hayo, Dk. Biteko alitoa wito kwa wananchi kulinda misitu na kuimarisha uhusiano mwema kati yao na hifadhi. Alisisitiza kuwa wafugaji wa nyuki wanaweza kuendelea na shughuli zao kwa kibali maalum na kwamba serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila, akizungumzia suala la Pori la Kigosi, alisema serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha wananchi wananufaika na shughuli za uchimbaji dhahabu bila migogoro. “Serikali inaendelea na mchakato ili jambo hili lifike mwisho wananchi waweze kunufaika kutokana na shughuli za uchimbaji wa dhahabu,” alisema Kasendamila, akisisitiza subira na utii wa sheria wakati utaratibu ukisubiriwa.

Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Geita, Rose Busiga, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya hospitali, barabara na maji. “Nimpongeze sana Dk. Biteko, mbunge wetu, kwa jitihada zake za kuhakikisha Bukombe inapata maendeleo kwa kutuletea miradi mbalimbali,” alisema Busiga.

Kwa ujumla, viongozi waliokutana na wananchi wa Bukombe waliwasihi kuwa na subira na kufuata sheria wakati serikali ikiendelea kuandaa utaratibu maalum wa matumizi bora ya Pori la Kigosi, ili kuhakikisha rasilimali hizi zinatumika kwa manufaa ya wote.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img