1.6 C
New York

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa: Urithi wa Asili wa Tanzania

Published:

*Mchango wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili watajwa

Na Faraja Masinde-Aliyekuwa Mang’ula

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, mojawapo ya hifadhi za asili zinazoonekana kuvutia zaidi barani Afrika, ni hazina ya kipekee ya wanyama na mimea.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho(kushoto) akifafanua jambo kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo.

Ipo kusini mwa Tanzania. Hifadhi hii ni sehemu ya safu za Milima ya Tao Mashariki ambazo ni maarufu kwa viumbe hai wa aina ya pekee na mandhari mazuri.

Eneo hili linajumuisha misitu minene, milima yenye kupendeza na maporomoko ya maji ya kuvutia, yakiwa na mchango mkubwa katika bayoanuai ya Afrika Mashariki.

Ina eneo la takribani kilomita za mraba 1,990 na inajulikana kwa kuwa na aina nyingi za mimea na wanyama ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani.

Hivi karibuni Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kinachotekeleza  mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kiliratibu timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira kwenda wilayani Kilombero mkoani Morogoro, kuangalia namna ambavyo mpango wa kulinda ushoroba wa wanyamapori wa Nyerere- Selous – Udzungwa unavyotekelezwa.

Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho, anasema kuwa Shirika la USAID ni moja kati ya wadau wanaosaidia kulinda urithi huo muhimu wa Tanzania kwa kufadhili shughuli za uhifadhi endelevu.

“Mazingira ndiyo kila kitu, kwani bila mazingira hakuna maisha. Hakuna hewa nzuri wala udongo utakaostawisha mazao, hivyo sisi sote tunategemea sehemu hizi zilizotengwa kama hifadhi, tufike mahala tujumuike kwa pamoja kupanda miti na kuelimishana kuhusu umuhimu wake,” anasema Theodora na kuongeza kuwa:

“Udzungwa ni hazina ya bayoanuai, inayoakisi utajiri wa urithi wa asili wa Tanzania. Ni sehemu ambayo watafiti na wapenda asili wanapenda kutembelea kutokana na upekee wa viumbe hai wanaopatikana hapa mfano kuna aina 20 ya viumbe wenye uti wa mgongo,” anasema Theodora.

Anasema miongoni mwa viumbe hai maarufu wanaopatikana Udzungwa ni pamoja na nyani wa Iringa Red Colobus, samaki wa mto Kilombero na wanyama wengine wa pekee kama mbega wa Udzungwa.

“Aidha, hifadhi hii ni makazi ya zaidi ya aina 400 za ndege na inakadiriwa kuwa na aina 2,500 za mimea, ikiwa na asilimia kubwa ya mimea ya pekee duniani,” anasema Theodora.

Ni moja ya maeneo yenye bioanuwai kubwa zaidi barani Afrika na ni sehemu muhimu ya mfumo wa Ikolojia ya Mashariki ya Arc.

Hifadhi hii ipo kusini mwa Tanzania na ni kivutio kikubwa kwa watalii, wanasayansi na wapenda mazingira kutoka kote ulimwenguni.

“Hifadhi ya Udzungwa ilianzishwa rasmi mwaka 1992 kwa lengo la kuhifadhi na kulinda wanyama pori na mimea adimu inayopatikana katika milima hii,” anasema Theodora.

Udzungwa ni maarufu kwa kuwa na aina nyingi za mimea na wanyama ambao hawaonekani mahali pengine popote duniani.

“Udzungwa ni hazina ya pekee ya Tanzania na dunia. Tunao wanyama na mimea ambao ni wa kipekee kwa eneo hili na ni jukumu letu kuhakikisha wanahifadhiwa kwa vizazi vijavyo.

“Pia hapa tuna wanyama wadogo kama panya na mijusi. Aidha, Udzungwa ni nyumbani kwa aina nyingi za mimea ambazo zimekuwa zikichunguzwa kwa matumizi ya kitiba na kisayansi,” anasema Theodora.

Vivutio vya Utalii

Moja ya vivutio vikubwa vya hifadhi ya Udzungwa ni maporomoko ya maji ya Sanje, ambayo yanaanguka kutoka urefu wa mita 170.

“Kutembea kuelekea maporomoko haya ni uzoefu wa kipekee, unaowapa watalii nafasi ya kuona mandhari ya kuvutia na bioanuwai ya hifadhi hii. Pia, Udzungwa ina njia nyingi za kupanda milima na matembezi ya misituni, ambazo zinawawezesha watalii kuchunguza kwa kina uzuri wa asili,” anasema Theodora na kuongeza kuwa:

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho.

“Tunawakaribisha watalii kutoka sehemu zote za dunia kuja kujionea uzuri wa asili wa Udzungwa. Kupitia utalii endelevu, tunaweza kusaidia kuhifadhi mazingira yetu huku tukiboresha maisha ya jamii zinazotuzunguka,” anasema.

Changamoto za Uhifadhi

Pamoja na umuhimu wake mkubwa, hifadhi ya Udzungwa inakabiliwa na changamoto zikiwamo ukataji miti, shughuli za kilimo na uwindaji haramu kama moja ya vihatarishi vya hifadhi hii.

“Kulingana na cha gamoto hii ya ukataji miti kwa ajili ya kuni, tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi pia kuona namna gani tunaweza kuzuia vitendo hivi kwa kuhakikisha wanapata nishati safi ikiwamo majiko ya gesi ili kuondoa kabisa ukataji miti.

“Katika hili wananchi wengi hasa akina mama wanatamani kuona nishati ya gesi ikiwafikia hata leo, ndiyo sababu tunaendelea kuomba wadau mbao wanaweza kusaidia wananchi hawa waweze kupata majiko ya gesi ili tulinde hifadhi yetu,” anasema Theodora.

Mhifadhi Mkuu, Theodora, anaeleza, “Changamoto za uhifadhi ni nyingi na ngumu, lakini tumejizatiti kukabiliana nazo kwa kutumia mbinu za kisayansi na kushirikiana na jamii za maeneo ya jirani. Tunahitaji msaada wa wadau wote, ikiwa ni pamoja na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali,” anasema.

Lakini pamoja na changamoto hizo, anasema uwepo wa mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umesaidia kufanikisha shughuli nyingi za ulinzi wa hifadhi kwa ujumla wake, hata hivyo zipo changamoto ambazo wanaamini wadau hao wanawaweza kuwasaidia.

“Mfano, kwasasa hatuwezi kufika kwenye maeneo mengi ya hifadhi, msitu umefunga sana, sio rahisi kutuma askari kwenda kwenye kila eneo la msitu, yapo maeneo hayajafikiwa kabisa, kwenye maeneo haya tunahitaji ndege isiyo na rubani (Drone) ambayo inaweza kutusaidia kuangaza juu kabisa ya mlima na kuangalia shughuli zinazofanyika ndani ya hifadhi ikiwamo kilimo,” anasema Theodora.

Anasema hifadhi ya Udzungwa imechukua hatua kadhaa za kuimarisha uhifadhi na kuendeleza utalii endelevu. Elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi na njia mbadala za kujipatia kipato imekuwa ni sehemu muhimu ya mipango ya uhifadhi.

“Tumeanzisha miradi kadhaa ya uhifadhi ambayo inahusisha jamii, kama vile upandaji miti na ufugaji wa nyuki. Miradi hii inasaidia si tu kuhifadhi mazingira bali pia kuongeza kipato kwa jamii zetu,” anasema Theodora.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa, Theodora Batiho(kushoto) akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, kwa niaba ya waandishi wa habari waliotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni.

Moja ya mikakati muhimu ya kuhifadhi hifadhi ya Udzungwa ni ushirikiano na jamii zinazozunguka hifadhi.

“Kwa kuwa shughuli za kibinadamu zinaathiri moja kwa moja uhifadhi wa mazingira, ni muhimu kuwashirikisha wanajamii katika juhudi za kuhifadhi hifadhi hii.

“Tubafanya kazi kwa karibu na jamii za maeneo ya jirani kwa kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi na kuwahusisha katika miradi ya maendeleo endelevu. Wanajamii wanashiriki katika mipango ya upandaji miti, ufugaji endelevu na kuhamasisha wananchi kutokukata miti kwa ajili ya kuni badala yake kutumia nishati mbadala.

“Tunaamini kwamba ushirikiano na jamii ni ufunguo wa mafanikio ya uhifadhi. Wanajamii wanapokuwa na uelewa wa umuhimu wa hifadhi na wanaposhiriki moja kwa moja katika miradi ya uhifadhi, wanakuwa walinzi wakuu wa mazingira yetu,” anasema Theodora.

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ni urithi wa asili wa thamani kubwa kwa Tanzania na dunia nzima. Pamoja na changamoto za uhifadhi, juhudi zinazofanywa na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii za maeneo ya jirani zinaonyesha matumaini makubwa kwa mustakabali wa hifadhi hii.

Udzungwa ni sehemu ya urithi wetu wa asili. Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda na kuhifadhi hazina hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Kwa pamoja, tunaweza kufanikisha hili.

Kwa hivyo, ni muhimu kuendelea kushirikiana katika juhudi za uhifadhi, kukuza utalii endelevu, na kuwajengea uwezo wanajamii ili kuhakikisha kwamba Hifadhi ya Udzungwa inabaki kuwa kito cha mazingira kinachong’aa kwa miaka mingi ijayo.

Afisa Uhifadhi wa Hifadhi hiyo, Christina Kibwe.

Upande wake, Afisa Uhifadhi wa Hifadhi hiyo, Christina Kibwe, amesema malengo yao ni kuhakikisha hifadhi hiyo inakuwa ya mfano hasa katika kulinda wanyama na kutunza shoroba.

Akizungumzia ziara hiyo, Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alimpongeza Mhifadhi Mkuu, Batiho na timu yake kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa timu ya Waandishi wa Habari za Mazingira waliofika ofisini kwake, ambapo aliahidi JET kuendelea kushirikiana na hifadhi hiyo katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu na kutambua umuhimu wa hifadhi hiyo muhimu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img