1.4 C
New York

Dk. Mpango akerwa na uchafu soko la Ilala

Published:

*Atoa maagizo Dawasa kutoa maji yote machafu yaliyoatuama kwenye mifereji

Na Grace Mwakalinga, Gazetini

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango ametoa muda wa wiki moja kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Jiji la Dar es Salaam( DAWASA), kuondoa maji machafu yaliyotuama kwenye mifereji na kutoa harufu mbaya soko la Ilala.

Dk. Mpango ametoa maagizo hayo Juni mosi, 2024 aliposhiriki usafi sokoni hapo ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya mazingira itayohitimishwa Juni 5, mwaka huu amesema maji hayo yanahatarisha afya ya wananchi, hivyo Dawasa wahakikishe wanatoa maji hayo haraka.

“Dawasa mchukue hatua za dharura ili haya maji machafu yanayotoka sokoni yaondolewe, hali hii sio nzuri, tunahatarisha afya za wananchi wetu. Nataka ndani ya wiki moja maji yasitiririke tena hapa,” amesema Dk. Mpango.

Awali akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Dawasa, Mkuu wa Kitengo cha Tehama na Takwimu wa Mamlaka hiyo, Kiula Kingu, amesema wameanza kuchukua hatua za kuondoa tatizo hilo na tayari wamempata mkandarasi wa ujenzi mabwawa ya kuhifadhia maji taka eneo la Buguruni.

Amesema mradi huo utakamilika ndani ya miezi 18 na utatumia kiasi cha Sh bilioni 290, na kwamba kwa sasa wanaendelea na jitihada za kutafuta wadau watakaochakata taka kuwa mbolea ili kupunguza taka zinazozalishwa.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema uzalishaji wa taka ni mkubwa lakini miundombinu ya kuhifadhi sio rafiki kwa sababu maeneo ya mkoa huo hayana madampo; hata hivyo wameanza jitihada za kuboresha miundombinu ya eneo la dampo la Pugu lenye ukubwa wa hekta 60 litumike lote kuhifadhia taka kuliko ilivyo sasa ambapo ni hekta 10 tu ndizo zinatumika.

Mwenyekiti wa soko la Ilala, Ally Mbiko, amesema kwa saaa soko hilo lina wafanyabiashara 2000 lakini lina uwezo wa kuchukua 6300 na wanazalisha taka nyingi licha ya kwamba hawana mindombinu ya kuhifadhia.

Amesema wanahitaji gari la taka ambalo litakuwa sokoni hapo muda wote kuliko ilivyo sasa ambapo kuna gari linakuja na kuondoka.

“Hitaji letu hasa ni magari ya kuhifadhia taka hapa sokoni yawepo muda wote hili soko linachangia fedha nyingi Sh milioni 100 kila mwezi zinakusanywa ni muhimu tuboreshewe miundombinu ya maji taka ili kuepukana na magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu,”amesema Mbiko.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img