1.4 C
New York

Kyela Festival kuja na mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Published:

Na Grace Mwakalinga, Gazetini- Kyela

ASASI ya Kijamii ya Kyela Festival, inayofanya shughuli zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, imepanga kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na namna ya kulima kilimo chenye tija ikiwa ni hatua za kuunga mkono jitihada za Serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuitikisa dunia.

Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Aisack Mwaipape amesema, wamemua  kutoa elimu hiyo baada ya kubaini idadi kubwa ya wananchi wa wilaya ya Kyela kulima  kilimo cha mazoea ambacho kinasababisha kupata mavuno kidogo na kuendelea kukata miti ili  kuendeleza shughuli za makazi.

Amesema wamepanga kutoa elimu maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya,kugawa miche ya miti na matunda  na kuwafundisha matumizi bora ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu na mbolea kwa kuzingatia hali ya hewa ili kupata mavuno mengi.

Ameongeza  kuwa  wamewashauri, kulima  mazao mbadala wa mpunga, kama vile  alizeti,  ambayo  inastawi sana wilayani humo, baadhi  waliolima msimu uliopita wamepata mavuno mengi  akiwamo Hillary Mwamkanba wa Kata ya Katumbasongwe.

“Tutajikita zaidi kwenye utoaji wa elimu ya kutunza mazingira, kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo mito, chemchem na athari za ukataji miti kwenye kilimo tutashauriana na wataalam  tulionao katika asasi yetu wakulima watumie pembejeo rafiki wa mazingira na kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa kujua ni wakati gani sahihi wa kupanda mazao yao,” amesema Mwaipape.

Akizungumzia kuhusu Asasi hiyo, amesema inazinduliwa kesho ikiwa na ajenda mbalimbali za kuzitekeleza mbali na kilimo pamoja na mazingira watajikita kwenye elimu ambapo watahamasisha watoto wa kike kupenda shule ili kutimiza ndoto zao na kutoa misaada  ya vifaa vya shule kwa familia zinazoshindwa kusomesha watoto wao.

Kwenye afya watatoa bima za afya kwa kaya masikini zinazoshindwa kumudu gharama za matibabu na kwenye utalii wataanzisha kampeni ya kutembelea vivutio vya utalii zikiwemo fukwe zilizopo nchi jirani ya Malawi kujifunza namna wanavyoendesha vivutio vyao.

Mhamasishaji katika Asasi hiyo, Joseph Mwaijega, amesema lengo la kuanzishwa ni kuisaidia jamii ya Kyela kuwa ya mfano kujiletea maendeleo.

Amesema wanachama wa Asasi hiyo wameweka utaratibu wa kuchangishana fedha ili kuwasaidia wenye uhitaji na kujumuika nao pamoja kwenye shughuli mbalimbali.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img