1.6 C
New York

AGENDA yaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mama Sayari Dunia na Malaria duniani

Published:

Na Grace Mwakalinga, Gazetini

WATU zaidi ya milioni 500 duniani kila mwaka huambukizwa ugonjwa wa malaria unaosambazwa kwa kung’atwa na mbu jike aina ya Anopheles ambaye ana vijidudu vya malaria.

Takribani nusu ya idadi ya watu duniani wako katika hatari ya kuambukizwa malaria na hasa katika nchi masikini japo ugonjwa huo unazuilika na kutibika.

Afisa Programu Mkuu wa Asasi inayojihusisha na mazingira pamoja na  maendeleo AGENDA, Silvan Mng’anya, alisema kila mwaka ifikapo Aprili 22 na 25, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mama Sayari Dunia na Malaria Duniani ambapo wao wametumia siku hiyo kufanya usafi katika ufukwe wa bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa namna ya kuilinda dunia kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, uchafuzi wa mazingira, kupotea kwa baionuai na kujilinda dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Mng’anya amesema licha ya jitihada zinazofanywa na wadau pamoja na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria bado hatua zaidi zinahitajika ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutumia vyandarau, usafi wa  mazingira na kuwahi tiba pindi wanapoona dalili zozote za ugonjwa huo.

“Siku hii inatambua kuwa dunia na mfumo wa ikolojia ni makazi ya pamoja ya binadamu, wanyama na mimea na inapaswa kulindwa ili kuinua maisha ya watu, kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na kuzuia upotevu wa baioanuai ambao unasababishwa na ukataji miti, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, shughuli za kilimo na ufugaji, biashara ya wanyamapori, yanaweza kuharakisha uharibifu wa dunia,” amema Mng’anya.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa AGENDA, Dorah Swai, amesema kauli mbiu ya mwaka huu katika kuadhimisha siku ya malaria duniani ni: “Utayari wa kukabiliana na Malaria” ikiwa imebeba ajenda ya kujitoa kwa pamoja katika kuungana jitihada za kupambana  na kuwa na dunia isiyokuwa na malaria.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limejiwekea malengo ya kuzuia malaria na kupunguza vifo vya watu 400,000 kila mwaka na AGENDA inaungana na wadau wengine nchini kuchukua hatua endelevu, ikiwemo kuzuia mazalia ya mbu kwa kuondoa plastiki zinazozagaa kwenye  mazingira ambazo ni chanzo kimojawapo cha mazalia ya mbu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img