1.6 C
New York

Bonde la maji Nyamitita hatarini kukauka, wadau wataka hatua za haraka zichukuliwe

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini-Serengeti

BONDE la Maji katika Kijiji cha Nyamitita Kata ya Ring’wani wilayani Serengeti mkoani Mara, lipo hatarini kukauka kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika eneo hilo ambapo imeshauriwa hatua za haraka zichukuliwe kunusuru bonde hilo ambalo ni chanzo cha maji.

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Mnada Josephat wakati wa zoezi la kupanda miti eneo hilo kwa lengo la kurejesha uoto wake wa asili.

Bondo hilo linadaiwa kuwa limevamiwa na wananchi ambao wanafanya shughuli za kilimo, kukata miti na kuchoma mkaa na uvunaji mbao.

Viongozi ngazi ya Wilaya, Kata na kijiji wakijiandaa kwenda kupanda miti.

Mhandisi Josephat amesema kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani hapa wamepanda miti 2,000 kwenye chanzo cha maji cha bonde la Nyamitita ili kukinusuru kutokana na kuvamiwa na wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali za kibinadamu.

Mhandisi Josephat amesema baada ya bonde hilo lenye chanzo cha maji kuvamiwa na watu na kuanza kufanya shughuli za kilimo wamelazimika kupanda miti hiyo 2,000 na kuweka mikakati ya kukabiliana na uharibifu unaofanyika.

Amesema katika kutekeleza hilo wameshirikisha uongozi wa kijiji na kata pamoja watu wa bonde la Ziwa Victoria ambapo wameweka mpaka wa zuio la mita 60 kila upande kufanya shughuli nje ya bonde hilo na kuwataka wanaofanya shughuli za kibinadamu kuacha mara moja.

“Sisi RUWASA tumeboresha miundombinu kwa kuweka vifaa vya kusukuma maji kutoka kwenye chanzo cha maji kwenda kwa wananchi wa vijiji vya kata hii, tunataka watu wote wanaozunguka bonde hilo lenye chanzo cha maji wanaofanya shughuli za kilimo, kukata miti, kuchoma mkaa na kuvuna mbao ndani ya mita 60 waache vinginevyo uongozi wa kijiji uchukue hatua ya kuwakamata watu wanaofanya uharibifu wa kufyeka miti kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria,” amesema Mhandisi Josephat.

Naye, Godfrey Nyakunga kutoka -TFS wilayani Serengeti, amesema bonde hilo lenye msitu uliohifadhiwa lipo chini ya uongozi wa kijiji kisheria pia kuna chanzo cha maji ambacho kinahudumia vijiji vya Nyamitita na Kenyana hivyo kinapaswa kulindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

“Tunaendelea kushirikiana na uongozi wa kijiji kuwachukulia hatua watu wanaokata miti ovyo kwenye bonde hili,” amesema Nyakunga.

Diwani wa Kata ya Ring’wani, Hellena Chacha ameutaka uongozi wa kijiji cha Nyamitita kuhakikisha kuwa wanakilinda na kukitunza chanzo hicho cha maji na kuchukua hatua kwa watu wote wanaokiharibu kwa kukata miti ovyo na kuchoma mkaa ambapo amesisitiza kila mtu awe mlinzi wa chanzo hicho hususan bonde lote kwani kinasaidia wananchi wa vijiji vya kata hiyo.

“Naomba uongozi wa kijiji kuacha kufumbia macho watu wanaofanya uharibifu wa aina yoyote katika chanzo hiki cha maji na kuchukua hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine kukinusuru wasiendelee badala yake wakilinde na kukitunza kwa faida ya watoto wetu,” amesema Diwani Chacha.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamitita, Musa Gesari, amesema uharibifu katika bonde hilo la chanzo cha maji nyamitita unafanywa na watu waliovamia eneo hilo kwa nguvu wanafanya shughuli za kibinadamu wanaalikana kwenda kufyeka na kukata miti huku wakifanya sherehe kwa kuchinja mbuzi  tunapofuatilia kuwakamata wanakimbia, hata hivyo tumefanikiwa kukamata baadhi ya watu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, tunaomba serikali isaidie suala hili.

Hata hivyo, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyamitita, Phillipo Rhobi na Afisa Mtendaji wa Kata ya Ring’wani, Joel Mwita wamekiri na kusema kuwa elimu kuhusu umuhimu wa bonde hilo la chanzo cha maji nyamitita imetolewa kwa wananchi hasa kijiji hicho inayowataka kuacha kufanya shughuli zozoteza kibinadamu eneo hilo kwani imekuwa ni mkombozi kwa wananchi na hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa wanaokaidi maelekezo ya viongozi.                                                                            

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img