Na Catherine Sungura-TARURA
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga barabara, vivuko na madaraja katika maeneo mbalimbali mkoani Rukwa ili kuinua shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi William Lameck amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuimarisha miundombinu ya barabara za wilaya nchini.
Mhandisi Lameck amemshukuru Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya TARURA Mkoa wa Rukwa kutoka Sh Bilioni 5.63 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia Sh Bilioni 12.3 mwaka 2023/24 ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha mtandao wa barabara mkoani humo.
“Barabara kwa kiwango cha changarawe zimeongezeka kutoka Km 867.25 hadi Km 1,143.05,” alibainisha.
“Tumeongeza mtandao wa barabara za lami na kufanyia matengenezo ya kawaida maeneo korofi jumla ya Km 196.66, ujenzi wa lami Km 0.8 na zege Km 1.55 zitatengenezwa katika Manispaa ya Sumbawanga na Wilaya ya Kalambo na Nkasi,” amesema.
“Pia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe Km 179.5 na ujenzi wa daraja la Kavunja lenye urefu wa mita 39 linalounganisha vijiji vya Kirando, Kazovu na Korongwe wilayani Nkasi lenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.76 ambapo ujenzi wake umekamilika na daraja linatumika,” amesema.
Amesisitiza daraja hilo limepunguza gharama za usafiri na usafirishaji ambapo hapo awali wananchi walikuwa wanazunguka katika vijiji vya Wilaya ya Kalambo lakini sasa wanatumia daraja hilo bila kuwa na wasiwasi juu ya mali zao na usalama wao.
Mkazi wa Nkasi, Sarafina Mbalamwezi ameipongeza kwa kile inachokifanya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na kukamilika kwa wakati na wananchi kuondokana na changamoto ya barabara.
Amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara umeweza kuwasaidia wananchi kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma mbalimbali ikiwemo ya matibabu.
Mkazi wa Sopa wilayani Kalambo, Amon Kabwe amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuboresha miundombinu vijijini ili kuhakikisha wananchi wanasafiri na kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi,” amesema.
Amesema hapo awali kulikuwa na changamoto ya barabara kutopitika hasa kipindi cha masika lakini kwa sasa barabara hizo zinapitika muda wote na madaraja korofi yametengenezwa na yote yanatumika.