Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Mwanza
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wezesha Binti na Mama Mjasiriamali (WBM) linatarajia kupanda miti 6,000 ndani ya Mwaka mmoja katika shule 60 za mikoa ya Mwanza, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha na Mtwara kupitia kampeni yao ya ‘Twiga wa Kijani’.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika Machi 28, mwaka huu katika shule ya msingi Jeshini iliyopo wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza, ambayo ni miongoni mwa shule 30 za msingi zitazofikiwa na kampeni hiyo na nyingine 30 za sekondari kwenye mikoa hiyo sita.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo limetoa Sh milioni 124 kusaidia kampeni hiyo, Ladislaus Matindi, amesema usafiri wa anga unachangia kuchafua mazingira kwa asilimia nne na ongezeko la joto duniani kwa asilimia tano, hivyo, wameamua kutoa mchango wao kulinda mazingira.
“Sisi na jumuiya ya kimataifa ya usafiri wa anga tulikubaliana tuchukue hatua ikiwemo kutumia nishati ambayo haichafui mazingira na kuzalisha hewa ya ukaa na kuwa na mipango ya uendeshaji wa ndege zifike haraka zisikae angani muda mrefu kuchafua mazingira,” amesema Matindi na kuongeza;
“Lakini pia kuunga mkono jitihada za wadau na Serikali kulinda mazingira ndiyo maana lilipokuja hili wazo tukaona tuwawezeshe kufanikisha hili na kufikisha ujumbe wa shirika letu. Hivi ni vizazi ambavyo bado vipo na ni endelevu tukiviwezesha katika kupunguza hewa ya ukaa na kulinda mazingira tutakuwa tumeokoa jamii yetu,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa kupanda miti, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Seleman Jafo amezitaka halmashauri zote nchini kutekeleza kwa vitendo mkakati wa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka ili kuokoa hekta 462,000 za miti zinazopotea kila mwaka nchini.
Waziri huyo amesema kampeni hiyo ni kichagizo cha kupeleka agenda katika shule nchini kutunza mazingira ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya Soma na Mti iliyozinduliwa mwaka 2012 ikihamasisha wanafunzi kupanda miti wakiwa katika umri mdogo.
“Kila mwaka tunapoteza hekta 462,000 za miti kutokana na sababu mbalimbali na ni maelekezo ya Serikali kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka ili tupande miti milioni 276 kwa halmashauri zote 184,” amesema Waziri Jafo.
“Kila mwaka tunapoteza hekta 462,000 za miti kutokana na sababu mbalimbali na ni maelekezo ya Serikali kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka ili tupande miti milioni 276 kwa halmashauri zote 184,”.
Waziri Jafo.
Naye, Mkurugenzi wa taasisi ya Wezesha Binti na Mama Mjasiriamali (WBM) inayotekeleza kampeni hiyo, Latifa Mohamed, amesema wamejikita kwa wanafunzi ambao ni taifa la kesho wapate elimu na kuhamasishwa kupanda miti, kutoa elimu ya kutunza mazingira, kuboresha na kuanzisha klabu za mazingira shule za msingi ili kuweka mabadiliko endelevu.
“Kila mkoa tutapanda miti 1,000 kwa kushirikiana na Shirika la Ndege (ATCL), tumechagua mikoa sita kwanza ambayo shirika letu la ndege linafanya safari zake lakini ni programu endelevu tutakwenda mikoa mingine zaidi,” amesema Latifa.
“Moja ya changamoto zinazomkwamisha mwanamke kuinuka kiuchumi ni mabadiliko ya tabianchi ndiyo maana tumeona tuje na mradi huu kutatua changamoto hiyo na kuwawezesha mabinti na wanawake kuinuka kiuchumi na kulisaidia taifa lake kuwa la kijani,” amesema.