1.6 C
New York

Uhifadhi uwe ni fursa kwa wananchi- Dk. Kalumanga

Published:

*Atahadharisha kutokubadili matumizi ya eneo la uhifadhi

*JET kujenga wigo zaidi kwa waandishi

Na Faraja Masinde, Gazetini-Bagamoyo

Tanzania ni kati ya nchi chache duniani zilizobarikiwa kuwa na utajiri wa maeneo lukuki ya uhifadhi karibu kila sehemu ya eneo lake ukiwamo ule wa misitu na viumbe pori.

Kama inavyofahamika kwamba uhifadhi ikiwamo ule wa misitu na viumbe pori ni moja ya mihimili ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi ikiwamo kuchochea utalii, kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hewa safi.

Meneja wa Ushirikishwaji Sekta Binafsi katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga.

Hata hivyo, kwa hapa nchini juhudi na mikakati zinahitajika ikiwamo kushirikisha Sekta Binafsi na wadau wengine ili eneo hilo liweze kutumika kikamilifu kama fursa ya uwekezaji utakaoinufaisha nchi.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni mjini Bagamoyo mkoani Pwani na Meneja wa Ushirikishwaji Sekta Binafsi katika Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga, katika warsha ya siku mbili ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa USAID.

“Bado juhudi na mikakati mbalimbali inahitajika kwa Serikali, Sekta binafsi na wadau wengine katika kuhakikisha kwamba angalau tunasaidia watu waanze kuona wanyamapori kama neema ya uwekezaji na hata ufugaji wa nyuki waufanye kama biashara na fursa mbalimbali zinazozunguka maeneo ya hifadhi ziwe na tija kwa wananchi,” amesema Dk. Kalumanga.

Mtaalamu huyo anasema kuwa somo la umuhimu wa uhifadhi ukiwamo wa wanyamapori kando na kufika kwa wananchi pia linapaswa kuanzia shuleni kwa ajili ya kuaandaa kizazi kinachojua umuhimu wakutunza raslimali hiyo muhimu.

“Uhifadhi unafaida nyingi, mfano ukiangalia Mamlaka zinazosambaza maji kazi yake ni kusafisha na kusambaza lakini chanzo chake ni maeneo yaliyohifadhiwa, mfano milima ya Uruguru, usambara, Meru na mingine. Hivyo lazima tuanze kuielimisha jamii na vizazi kaunzia watoto walioko shuleni kuwa faida za maeneo yaliyohifadhiwa ni zaidi ya kuona wanyamapori,” amesema Dk. Kalumanga.

Akitolea mfano; faida nyingine, ameitaja sekta ya nishati ambapo maji yanayopatikana katika bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julias Nyerere (JNHPP) chanzo chake ni maeneo yaliyohifadhiwa.

“Tunapoongelea utalii ni mojawapo tu ya faida inayotokana na uhifadhi, lakini maisha yetu kwa ujumla yanategemea sana uwepo wa viumbe pori, hivyo tusifikirie kuondoa maeneo haya kwa kufanya matumizi mengine, hapana, kwani maisha yetu yanategemea sana uwepo wa viumbe pori,” amesema Dk. Kalumanga.

Akizungumzia mradi huo wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Kalumanga amesema unalenga kuangazia namna wanavyoweza kuzisaidia jamii za kitanzania hasa zinazokaa kando ya maeneo yaliyohifadhiwa kufaidika na uwepo wa raslimali hizo muhimu kwa taifa kwa kuzijengea uwezo.

“Kwani maeneo haya yana fursa nyingi ikiwamo inayotokana na utalii ukiwamo ule wa wanyamapori unaochukua asilimia 80, na ule wa misitu, hivyo changamoto hapa ni kuwaelimisha wananchi hawa waweze kunufaika kwa kujiwekea miongozo kwa manufaa yao,” amesema Dk. Kalumanga.

Mmoja wa wakufunzi katika warsha hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Dunstan Kamanzi, Dastan Kamanzi, wanatamani kuona waandishi wa habari wakiiandika habari hizo za mazingira kwa tija hatua ambayo amesema kwamba itasaidia kutatua pale palipo na changamoto kwa haraka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Dunstan Kamanzi, Dastan Kamanzi.

“Waandishi wa habari wanao wajibu Nna uwezo utakaosaidia kuibua changamoto zitakazosaidia kunyanyua sekta ya uhifadhi nchini kwa kuandika habari zenye tija,” amesema Kamanzi.

Akizungumzia warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET), John Chikomo, amesema lengo ni kuona waandishi wa habari wanajengewa wigo mpana kuhusu eneo la uhifadhi ili waweze kusaidia kujenga uelewa kwa jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET), John Chikomo.

“Mbali na kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari pia tunatarajia kutoa mafunzo kwa Wahariri ili hata habari za uhifadhi zinapofika ndani ya vyombo vya habari basi mhariri awe na uelewa na kuona umuhimu wake badala ya kuzitupa,” amesema Chikomo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img