Na Faraja Masinde, Gazetini
Katika kuhakikisha kuwa jamii inaandaa akina Wangari Maathai wengine watakaotunza mazingira, Ubalozi wa Kenya nchini Tanzania umeeleza kuwa upo tayari kuongeza msukumo wa uanzishwaji wa klabu za mazingira shuleni.
Hayo yameelezwa Machi 16, 2024 na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Balozi Isaac Njenga, wakati wa hafla ya upandaji Miti 300 kwa heshima ya Mazingira ya Afrika na Siku ya Wangari Maathai katika Hifadhi ya Mazingira ya Pugu Kazimzumbwi mkoani Pwani.
Balozi Njenga amesema kuwa kushirikisha watoto katika kutunza mazingira ni jambo muhimu na kwamba ndiyo sababu hata wao wanashirikisha watoto katika zoezi la upandaji miti kwa kuwa ndilo Taifa la kesho litakalochukua kijiti cha kutunza mazingira.
SOMA PIA: Balozi Njenga: Kila mmoja anadeni la kutunza mazingira – gazetini
“Tunahimiza kushirikisha watoto katika shughuli za upandaji miti na utuanzaji wa mazingira kwa ujumla kwa sababu wao ndiyo vizazi vijavyo.
“Hivyo, lengo hapa waone kazi tunayoifanya ili nawao waone kuwa wazazi wetu walipanda miti ili kutunza mazingira kwa sababu hiyo utakuwa ni wajibu kwao kuendeleza utunzaji wa mazingira.
“Pia upande wa shule kule kwetu Kenya kuna klabu zinazojihusisha na utunzaji wa mazingira, nafikiri hata Tanzania klabu hizo zitakuwepo na kama hazipo tutashirikiana na Taasisi pamoja na Wizara ya Elimu ili tuweze kushirikiana katika kufanya mambo ambayo tunaona yanaweza kuwasaidia watoto wetu na vizazi vijavyo kuweza kukua katika hali ya kufahamu kuwa utunzi wa mazingira ni wajibu wetu sote,” amesema Balozi Njenga.