21 C
New York

JET kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu uhifadhi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimeandaa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari za Mazingira kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini yenye lengo la kuwapa elimu ya namna ya kuripoti kwa usahihi masuala ya uhifadhi.

Pamoja na mambo mengine elimu hiyo pia inalenga masuala ya uhifadhi wa  shoroba na namna ya kupambana na Uharibifu wa Misitu, Uhalifu wa Wanyamapori, Mabadiliko ya Tabianchi na uhifadhi wa viumbe hai.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika leo Februari 15 na 16, mwaka huu mjini Bagamoyo mkoani Pwani yakijumhisha wanahabari 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari Tanzania.

Mapema, akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo ameiambia GAZETINI (www.gazetini.co.tz) kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa Tuhifadhi Maliasili unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo.

Chikomo amesema kuwa, Mradi wa Tuhifadhi Maliasili ni wa miaka mitano na unalenga zaidi kushughulikia tishio la kutoweka kwa wanyama na viumbe hai nchini Tanzania.

“Kupitia mafunzo haya, waandishi wa habari watajazwa maarifa, ujuzi na  mtazamo chanya ya kuripoti taarifa za uchunguzi kuhusu uhifadhi wa viumbe hai na mabadiliko ya tabianchi kwa usahihi zaidi.

“Hivyo, JET kwa kushirikiana na wadau wengine itawajengea uwezo wanahabari katika eneo la uhifadhi wa shoroba ili kujua namna ya kuchunguza, kuripoti na kuchambua uhusiano wa wanyamapori, uhifadhi wa bahari na misitu, biashara haramu na ujangili sanjari na kukuza uhifadhi wa wanyamapori na masuala ya utalii,” amesema Chikomo.

Ameongeza kuwa mbali na kutengeneza mitandao kwa kuwaunganisha waandishi wa habari na wadau wa uhifadhi katika ngazi tofauti pia waandishi wataboresha ubora wa taarifa zao kwenye masuala ya shoroba.

Mradi wa tuhifadhi Maliasili utahusisha  shoroba ya wanyamapori uliopo Kwakuchinja ambao unaunganisha mfumo wa Ikolojia wa Tarangire-Manyara katika Wilaya za Babati na Monduli zilizopo kwenye Mikoa ya Manyara na Arusha.

Pia kuna Shoroba ya Kigosi Moyowosi-Burigi Chato- unaounganisha Kigosi Moyowosi na Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato zilizopo katika Wilaya za Biharamulo na Kakonko, Mkoa wa Kagera na Kigoma.

Shoroba ya  Nyerere Selous-Udzungwa- unaounganisha Hifadhi za Taifa za Milima ya Nyerere Selous na Udzungwa, katika Mji wa Ifakara, Mkoa wa Morogoro.

Shoroba ya Amani- Nilo unaounganisha Hifadhi ya Mazingira ya Amani na Hifadhi ya Misitu ya Mazingira ya Nilo, katika Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga.

Shoroba ya Ruaha Rungwa-Katavi unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Pori la Akiba la Rungwa, Mapori ya Akiba ya Lukwati na Pigi, na Katavi, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya.

Shoroba ya Ruaha Rungwa-Inyonga unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, na Mapori ya Akiba ya Rungwa na Inyonga, katika Wilaya za Itigi/Sikonge, Mkoa wa Singida/Tabora.

Shoroba ya  Mahale-Katavi unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale na Katavi, katika Wilaya za Tanganyika na Uvinza, Mikoa ya Katavi na Kigoma.

“Kupitia USAID mradi wa Tuhifadhi Maliasili, JET itaweka mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari kufanya uchunguzi na kuripoti ipasavyo masuala ya uhifadhi,” ameongeza Chikomo.

Kwa mujibu wa Chikomo, mara baada ya mafunzo hayo wanahabari watatumia ujuzi walioupata kuzalisha habari za  uchunguzi za uhakika ambazo zitasaidia kuongeza chachu ya uhifadhi wa maliasili, aida waandishi watapata fursa ya kuzungumza  na  wananchi, viongozi na  na wadau wengine kuhusu shoroba.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img