8.5 C
New York

Mabadiliko tabianchi kikwazo Ajenda 10/30

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Mabadiliko ya tabianchi imeelezwa kuwa moja ya changamoto inayoathiri sekta ya kilimo nchini hatua ambayo imesababisha hata mbegu zilizopo kushindwa kustahimili muda mrefu.

Moja ya athari za mabadiliko hayo ni pamoja na kuongezeka kwa joto linalosababisha mimea kushindwa kuhimili joto hilo, kuibuka kwa magonjwa mapya na wadudu wapya hali ambayo itawalazimisha watafiti hususan wa mbegu za mazao kufanya kazi ya ziada katika kubuni mbegu zinazoendana na mazingira ya sasa.

Changamoto hizo zinaibuka wakati ambapo Tanzania inatekeleza ajenda ya 10/30 inayolenga kuongeza mchango wa kilimo katika pato la taifa kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 ikiwamo kuwezesha vijana kuchangamkia kilimo kupitia mradi wa Jenga Kesho iliyobora (BBT).

Mtaalamu na Mshauri wa Utafiti wa mbegu nchini, Dk. Emmarold Mneney.

Hayo yamebainishwa Novemba 4, 2023 mjini Bagamoyo mkoani Pwani na Mtaalamu na Mshauri wa Utafiti wa mbegu nchini, Dk. Emmarold Mneney, wakati wa warsha ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini kuhusu mbegu za mazao iyoandaliwa na Shirikisho la Uendelezaji na Ustawishaji wa Mifumo ya Chakula barani Afrika (AGRA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Media Brains.

“Mabadiliko ya tabianchi sasa hivi yameingia kwenye kilimo na yameleta changamoto nyingi katika kupanda na kulima, kwa upande wa mbegu changamoto tunayoiona inatokana na mbegu tulizonazo za kisasa na za asili kwani hazikugunduliwa kukiwa kuna changamoto zilizopo sasa.

“Matatizo haya ni mapya na hizi mbegu tulizonazo haziwezi kustahimili, kwa hiyo kuna changamoto sasa ya watafiti wafanye ugunduzi wahakikishe kwamba hizi mbegu za asili au hizi tulizonazo sasa hivi zinapata hizi sifa za kukabiliana na mabadiliko haya ya tabianchi,” amesema Dk. Mneney.

Dk. Mneney amezitaja changamoto nyingi ambazo zinarudisha nyuma kilimo na upatikanaji wa mbegu kuwa ni pamoja na ukame wa muda mrefu nchini ikilinganishwa na miaka ya iliyopita.

“Changamoto kubwa hapa ni kuwapo kwa kipindi kirefu cha ukame hivyo mbegu zilizopo zinashindwa kustahimili muda huo bila maji, pia kuna ongezeko la joto ambalo mazao mengi yanashindwa kuhimili na hata yanayoota yanashindwa kutoa maua vizuri,” anasema Dk. Mneney.

Mwakilishi kutoka AGRA, Ipyana Mwakasaka akizungumzia jinsi taasisi hiyo ilivyojipanga kuwasaidia wakulima.

Mtaalamu huyo anasema kadhalika mabadilikoa ya tabianchi yamesababisha kuibuka kwa magonjwa ikiwamo wadudu wapya ambao wameleta magonjwa mapya na kwamba mimea inashindwa kuhimili.

Kipi kifanyike?

Dk. Mneney amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo watafiti hawana budi kuhakikisha kwamba wanaumiza vichwa kwa kuja na mbegu mpya ambazo zitaweza kustahimili changamoto hizo.

“Kazi ambayo ipo ni kwa watafiti wetu wafanye bidii ya kuhakikisha kwamba utafiti unafanyika wakupata mbegu mpya ambazo zinakuwa na uwezo wa kustahimili changamoto hizi zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi kwani zipo na zitaendelea kuwepo hivyo ni muhimu mbegu zetu kuendana na hali ambayo ipo,” amesema Dk. Mneney.

Ameongeza kuwa wakati mbegu mpya zikisubiriwa, wakulima wanaweza kuanza kufanya mabadiliko ya kilimo kwa kuchanganya mazao badala ya kulima zao moja kila mwaka hatua ambayo hata hivyo amekiri kuwa itapunguza ufanisi wa uzalishaji.

Kwa upande wake akizungumza katika warsha hiyo, Bob Shuma kutoka TASTA amesema iwapo hazitafanyika juhudi za kutenga maeneo ya kuzalisha mbegu za mazao nchini bado itakuwa ni kazi kubwa kwa wananchi kuinua uchumi kupitia kilimo huku akionya kuhusu siasa.

“Elimu ya mbegu ni muhimu sana kuwafikia wananchi sababu utaona kuwa kwa sasa bado tunategemea kuagiza mbegu za mazao kutoka nje ya nchi na sote ni mashahidi kuwa kwa siku za karibuni kumekuwa na changamoto ya uhaba wa Dola ya Marekani kila mtu ni shahidi wa yaliyotokea.

“Je inapotokea hali kama hiyo tunafanyaje hivyo ni muhimu kuwa na wataalamu wetu wa kutosha ambao watasaidia katika uzalishaji wa mbegu zinazoweza kukabiliana na changamoto zilizopo.

“Shida kubwa nyingine tuliyonayo kama nchi ni kuhusu kuweka siasa katika kila kitu, hatua hii inachochea kukosekana kwa uhalisia, tunatakiwa tuachane na mwenendo huu na kuweka vitu halisia ili tuje kwamba kama nchi tumepia hatua kiasi gani katika nyanja hii ya uzalishaji mbegu na siyo kuwa na takwimu ambazo siyo halisia,” amesema Shuma.

Awali, akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Media Brains Ltd, Jesse Kwayu amesema lengo la warsha hiyo ni kujenga uelewa wa kutosha kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini ambao wananafasi kubwa ya wakufaikia wananchi kupitia vyombo vyao.

“Tumeandaa warsha hii baada ya kuwapo kwa ufahamu mdogo kwa wananchi juu ya namna ya kupata mbegu bora jambo ambalo linarudisha nyuma azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa kilimo kinachangia asimilia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2030.

“Mfano utaona kwa hapa nchini tafiti zinaonyesha kuwa hakuna zao lolote nchini ambalo mbegu zake zinazalishwa kwa walau asilimia 50, hakuna zote ni chini ya hapo iwe ni mahindi, maharage na mazao mengine,” amesema Kwayu.

Hali ya mbegu nchini

Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 20 tu ya wakulima nchini Tanzania ambao wanatumia mbegu bora hatua inayodhorotesha ufaisi wa kilimo.

Aidha, utafiti wa mahitaji ya mbegu unaonyesha kuwa mahitaji ya mbegu nchini Tanzania ni tani 120,000 hata hivyo kiwango hicho imekuwa ni changamoto kufikiwa, mathalani katika msimu wa kilimo wa 2020/21 mahitaji ya mbegu yalikuwa 97,928 huku upatikanaji wa mbegu ukiwa ni tani 85,005 tu sawa na upungufu wa tani 12,923.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img