Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Kulingana na machapisho mbalimbali, Bundi ni miongoni mwa ndege ambae huishi kutegemea nyama kama chakula chake kikuu.
Bundi hutafuta mawindo yake nyakati za usiku na mara nyingi huutumia mchana kwa mapumziko. Katika uainishaji wa kisayansi, bundi huainiswa kama himaya ya wanyama ya wanyama wenye uti wa mgongo, ngeli ya ndege na familia ya bundi.
Tafiti zinabainisha uwepo wa aina nyingi za ndege hawa jamii ya bundi diniani, zikiwa ni zaidi ya spishi 200.
Bundi huwinda wanyama wadogo wadogo kama vile: panya, mijusi, ndege na wadudu, mawindo yake hufanyika majira ya usiku ili kuepusha ushindani dhidi ya ndege wengine walao nyama kama vile: mwew, na tai, pia hii humsaidia kukamata wanyama hawa kwa urahisi usiku wakiwa wamelala.
Hifadhi ya Taifa ya Mazingira ya Misitu ya Amani iliyoko mkoani Tanga katika Wilaya za Muheza na Korogwe inasifika kwa kuwa na bundi wa kipekee anayefahamika kama Usambara Eagle Owl.
Hivi karibuni Waandishi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) katika kutekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili walitembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani iliyopo Muheza mkoani Tanga na kwa lengo la kujifunza namna uhifadhi wa mazingira unavyotekelezwa katika hifadhi hiyo.
Edigar Apolinary ni Afisa Mfuatiliaji kutoka Shirika la Nature Tanzania katika Hifadhi ya Misitu Asilia ya Amani, akimuelezea bundi huyo anayepatikana katika hifadhi hiyo ‘Usambara Eagle Owl’ ambaye huwezi kumpata sehemu nyingine duniani mbali na Tanzania, anasema bundi huyo huonekana usiku.
“Bundi huyu hupatikana tu hapa katika milima hii ya Usambara Mashariki. Bundi hasababishi uchoro kama ambavyo wengi wamekuwa wakisema, hivyo dhana hii inapaswa kuondoka badala yake wamuone kama fursa.
“Watu wengi wanadhani kwamba kwa kutoa sauti kubwa ya kuogopesha na kupatikana kwake tu usiku ikiwamo macho yake ya kuogopesha kwamba anasababisha uchuro. Hapana, siyo kweli kabisa. Ndiyo maana tunafanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii yetu,” amesema Apolinary.
Tofauti yake na ndege wengine
Kulingana na mtaalamu huyo, bundi amejitofutisha na ndege wengine walao nyama kama vile tai na mwewe kwa kufanya mawindo yake usiku, hii humpunguza ushindani wa chakula kati yake na ndege wengine walao nyama, halikadhalika uwindaji wa usiku humsaidia bundi kuotea na kuvamia wawindo yake kwa urahisi kwani muda wa usiku wanyama wengi hupumzika.
Mabawa na manyoya na bundi yana muuondo na mfumo ya kipekee ambayo humfanya bundi kupaa kimyakimya hivyo kuweza kumlega na kumkamata mbawa wake pasipo kupiga kelele. Hii hufanya uwindaji wa bundi kuwa mwepesi kwani mbawa wake hawawezi kumsikia bundi akiwa anaenda kuwavamia.
Kutokana na kufanana sana na mazingira yake, bundi huweza kujikinga dhidi ya maadui au mashambulizi ya wanyama wengine akiwemo binadamu. Siyo rangi tu pia bundi huweza hukaa kwenye tawi la mti au sehemu nyingine bila kutingishika hivyo kuonekana kama kiumbe kisicho na uhai kama vile jani la mti au kisiki.
Kulingana na mtaalamu huyo, bundi ni ndege kama walivyo ndege wengine, ambapo hufanya mawindo yake usiku siyo kwa sababu ni mchawi au katumwa na mchawi.
Lengo la kuwinda na kuwa macho usiku huku mchana akitumia kupumzika ni kupunguza ama kuepuka mapambano ya kugombania chakula na ndege au wanyama walao nyama ambao huwinda mchana.
Dhana juu ya mlio wa bundi
Kulingana na wataalamu wa hifadhi ya Amani, mlio wa bundi usikikapo usiku siyo mkosi kama wasemavyo watu wengi, kama ilivyo kwa ndege wengine bundi hutoa mlio kwa ajili ya mawasiliano baina yao hii inaweza kuwa;
“Kuitana, kuogopa, kumtishia au kumkimbiza adui na sababu nyingine ziwafanyao ndege wote kutoa milio,” anasema.
Kidunia idadi ya bundi imekuwa ikipungua, aidha kuna sababu kadha wa kadha zilizosababisha kupungua kwa idadi ya bundi duniani, ikiwamo uwindaji wa bundi, ukosefu wa chakula kutokana kutoweka kwa baadhi ya viumbe kama wadudu na wanyama wadogo wadogo ambao ndio chakula cha bundi pamoja na magonjwa.
Katika jamii nyingi hususan za Kitanzania bundi huwindwa si kwa sababu ya chakula, bali huuliwa kutokana na jamii kuwa mtazamo hasi kwa kiumbe hiki kisicho na hatia.
Izingatiwe kiumbe huyu ni muhimu kwani ana mchango mkubwa katika ikolojia ya mazingira kwani ni husaidia kudhibiti ongezeko la wanyama waliwao na bundi, baadhi ya wanyama hao ni waharibifu hasa wa mazao ya kilimo kama vile panya na wadudu waharibuo mazao.
Wataalamu wanaeleza kuwa kutoweka kwa bundi kutasababisha madhara ambayo yataathiri ustawi wa viumbe wengi ikiwemo binadamu kutoka na kuathirika kwa mfumo mzima wa kiikolojia.
Hata hivyo, kutokana na kuwapo kwa mtazamo hasi ndani ya jamii juu ya bundi kuna haja kubwa ya kutoa elimu katika jamii ili kuondoa mtazamo hasi uliojengeka miongoni mwa watu wengi.
Elimu hii inapaswa igusie uhalisia na sababua ya mfumo wa maisha ya ndege huyu, umuhimu wa bundi na faida zake zinapaswa kuwekwa banayana hasahasa kwa wakulima kwani bundi anaweza kutumika kudhibiti wadudu na wanyama waharibifu hivyo kutumika kama mbadala wa dawa za chemikali zinazotumiwa na wakulima.
Mfano, Mei, 2022 iliripoti na vyombo vya habari kuwa wakulima zaidi ya 200 kutoka katika wilaya ya Iringa na Mufindi mkoani Iringa walipata mafunzo kuhusu matumizi ya bundi kudhibiti visumbufu vya mazao mashambani na kuacha kumuhusisha bundi na imani za kishirikina.
Akitoa mafunzo hayo Mei 30, 2022 katika Kijiji cha Mgama wilaya ya Iring, Dk. Nikolaus Mwalusaka kutoka Chuo cha SUA ambaye ni Mtafiti Mkuu wa mradi unaohusu uelewa mtazamo wa wakulima kuhusu kutumia bundi kukabiliana na viumbe wasumbufu wa mazao hasa panya.
Dk. Mwalukasa alisema kuwa lengo kuu la utafiti huo ni baada ya kuwa na upotevu wa mahindi kwa asilimia 5-15 kwa mwaka kutokana na panya wanaokula mahindi, sababu mazingira yanawezesha panya kuzaliana na kukua kwa kasi kubwa.