8.8 C
New York

Visual| Sababu za kuhitaji nishati safi ya kupikia

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Takwimu za Wizara ya Nishati nchini zinaonyesha kuwa watu 33,000 wanafariki dunia kila mwaka nchini kutokana na kupikia mazingira yenye moshi wenye sumu unaotokana na matumizi ya mkaa, kuni na mabaki ya mazao.

Kama hiyo haitoshi, Shirika la Clean Cooking Alliance watu milioni 4 kote ulimwenguni hufa kabla ya wakati kila mwaka sababu ya kupikia kwa moto na nishati ngumu kama mkaa.

Shirika hilo linaongeza kuwa watu milioni 950 wanategemea kuni na mkaa kupikia, idadi inayokadiriwa kukua hadi bilioni 1.67 ifikapo 2050.

Wadau wanasemaje

Estomih Sawe ni Mkururugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Huduma za Nishati Endelevu na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania(TaTEDO) ambapo anasema kuwa wamekuwa wakihamasisha matumizi ya kupikia joto badala ya moto ili kulinda mazingira na kupunguza athari za kiafya.

Usanifu juu ya madhara ya mkaa.

Kwa mujibu wa Sawe Dar es Salaam inatumia zaidi ya asilimia 60 ya mkaa wote unaozalishwa nchini ambapo miaka michache iliyopita zaidi ya tani milioni mbili za mkaa ulitumika.

“Changamoto kubwa inakuja kwamba hapa Dar es Salaam ni eneo ambalo karibu watu wote wana umeme, gesi na nishati zingine zote lakini bado wanatumia mkaa kwa wingi, hivyo sisi tuliona umuhimu wa kuwa na teknolojia ya jiko linalotumia nishati kidogo sana ya umeme kuliko kutumia gesi, mkaa katika matumizi ya kupikia kwa haraka,” anasema Sawe.

Aidha, anataja sababu za watu kutumia zaidi nishati ya mkaa kuwa inatokana na mila na tamaduni ikiwemo kutokufahamu mbadala wa kutumia mkaa na kuni katika matumizi ya kupikia.

“Kwa changamoto hizo tunahitaji kuwahamasisha wananchi na kuwaelimisha ili wafahamu kwamba kuna nishati safi ambazo unaweza kutumia badala ya mkaa na ukapika chakula kwa bei nafuu,haraka na kwa usalama.

“Tunataka kuwakikishia kuwa lazima tuhamie teknolojia nyingine ya kupikia joto badala ya moto na natoa wito kwa Serikali na wananchi tushirikiane kuhusu kujua umuhimu wa kuwa na nishati mbadala katika kupikia na upo uwezekano wa kupika kwa kutumia joto badala ya moto kwa ufanisi mkubwa na usiharibu mazingira,” anasema Sawe.

Anaongeza kuwa ni muhimu kwa Watanzania kutumia vifaa vinavyotengenezwa na teknolojia isiyoharibu mazingira kwa kuwa Tanzania itakuwa na umeme wa ziada mwingi baada ya kukamilika bwawa la Nyerere hivyo ni lazima watumie umeme huo kwa matumizi ya kupikia kupikia majiko waliyoyasanifu ambayo wanaweza kuyatumia kwa haraka na kuwahi shughuli zake zingine.

Miti inateketea

Mratibu wa Mabadiliko ya Tabianchi na Tungamotaka kutoka TaTEDO, Shima Sago amesema sababu za kuhimiza Nishati Jadidifu hasa wakati huu kutokana na kwamba nishati zingine zinachangia uharibifu wa tabaka la juu linazozuia mionzi ya jua kufika ardhini hivyo kuchochea ongezeko la joto na ukame.

Mratibu wa Mabadiliko ya Tabianchi na Tungamotaka kutoka Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania(TaTEDO), Shima Sago akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Novemba 10,2022 kuhusu umuhimu wa Nishatin Jadidifu

“Faida za Nishati Jadidifu ni pamoja na kupunguza gharama za kununua umeme mara kwa mara, kutoa ajira, kukaushia vyakula shambani, kuepuka matatizo ya kiafya kwa kuvuta hewa chafu, kupunguza hewa ukaa na kutunza tabaka la kuzuia mionzi ya jua.

“Ili upate tani moja ya mkaa lazima ukate magogo 12 ya miti na kwa mwaka tunatumia tani milioni 2.5 za mkaa nchini hivyo ni lazima tuendeleze kuhifadhi mazingira na kutumia nishati jadidifu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo,” anasema Sago.

Kwa nini nishati safi

Meneja Nishati kutoka TaTEDO, Mary Swai anasema wao waliamua kubuni jiko la kisasa linaloweza kupika chakula chochote ikiwemo Kande, Maharagwe, Kunde, Ugali, Nyama na vyakula vingine ambavyo hutumia gharama kubwa hadi vinapoiva kwa kutumia gharama kidogo ili kulinda mazingira na afya za watanzania.

“Hili jiko yaani Pressure cooker ni jiko, sufuria na ni nishati ya kutumika nyumbani isiyo na moshi wala kuharibu mazingira unatumia umeme kidogo kuliko ungetumia mkaa na gesi.

“Hivyo, tunawashauri wananchi wote kutumia jiko hilo la kisasa ili kupunguza gharama za matumizi ya nishati chafu kama mkaa na zingine.

Majiko ya kisasa

“Pia tuna teknolojia kwa ajili ya wakulima inayoweza kukausha mazao bila kupoteza uwezo wake hivyo majiko haya ni salama kwa yeyote anayetumia kwa kuwa hujizima kulingana na muda ulioweka bila kuleta athari zozote,” anasema Swai.

Hatari ya kutumia mkaa, kuni

Matumizi ya mkaa na kuni hutoa moshi ambao huleta madhara kwa binadamu. Aidha, kwenye kuni na mkaa pia hutoa chembechembe ndogo ambazo huweza kupenya katika njia ya hewa na kuleta athari kiafya.

Pia hewa ya kaboni monoksidi inayotolewa na mkaa na kuni huweza kuingia mwilini na kupenya hadi kwenye damu kisha inaanza kuondoa hewa ya oksijeni kwenye damu na kusababisha madhara ya muda mrefu na hata kifo kama itaingia kwa wingi.

‘’Mkaa na kuni kwa ujumla inaweza kuathiri njia ya hewa na damu lakini mtu akishapata matatizo ya njia ya hewa kutokana na matumizi ya mkaa na kuni, ni chanzo cha matatizo mengine ya kiafya kama moyo, unakuta mgonjwa moyo umefeli lakini sababu inakua ni matatizo yanayotokana na shida ya mapafu ambayo imesbabishwa na matumizi ya mkaa na kuni,” anasema Dk. Elisha Osati, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani.

Serikali inasemaje

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda, anasema Serikali ipo katika maandalizi ya kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Anasema serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa nishati jadidifu kupitia Wizara ya Nishati ili kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda.

Anasema Nishati Jadidifu ni vyanzo vya kuzalisha umeme visivyoisha ikiwemo Upepo,Jua,Jotoardhi,Mawimbi ya bahari, Maporomoko ya maji ambayo ni chini ya megawati 10 na vingine ambavyo vinauwezo wa kuzalisha nishati bila kuchafua mazingira.

“Serikali kupitia Sera yake ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 inaweka kipaumbele katika uendelezaji wa rasilimali za nishati jadidifu kwa kuwa ni rasilimali endelevu na nyingi zinapatikana hapa nchini.
“Sera yetu inatambua nishati jadidifu lakini na sera zingine kama ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Mkakati wa Kitaita wa Mazingira ambazo zote hizo ni muendelezo wa nishati jadidifu”amesema Nyanda.

Nyanda anasema kukamilika kwa mkakati huo kutatoa muongozo mzuri wa uendelezaji wa nishati jadidifu hapa nchini.

“Kwa sasa Wizara ya Nishati inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu na tupo katika hatua nzuri na tayari mshauri elekezi ameshaanza maandalizi ya mkakati na kwa sasa anaendelea kupata maoni ya wadau hadi mwakani mwezi wa pili itakuwa imekamilika.

“Changamoto nyingine iliyokuwepo ni Sera ya Mkakati wa Nishati Jadidifu na jinsi gani unapata nyenzo ya kutekeleza sera yako inayotambua nishati Jadidifu ndio maana sasa hivi serikali imewekeza katika kuandaa Mkakati ya Nishati Jadidifu na Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati,” anasema Nyanda.

John Chikomo ni Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) ambapo anasema kuwa chama hicho kitaendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kujikita zaidi katika kuandika habari za mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo ili kupunguza athari zitokanazo na nishati iziyo salama.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img