HAKUNA namna nyingine zaidi ya uwekezaji wa maana ndipo maendeleo ya mchezo wa soka yaweze kuonekana. Uwekezaji si tu huziwezesha klabu kumudu gharama za uendeshaji, pia huchagiza ushindani wa ndani ya uwanja.
Safari hii, Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoanza hivi karibuni imepewa uzito mkubwa na Kampuni ya Azam Media Limited (AML). Kampuni hiyo imeongeza utamu mwingine kwenye michuano hii, achili mbali kazi kubwa iliyofanya ya kurusha ‘live’ mechi.
AML waliohodhi haki ya matangazo ya televisheni kwenye Ligi Kuu hii, wametanua uwezekaji wao na kufikia bilioni 225.6, ukiwa ni mkataba mpya wa miaka 10 utakaoanza msimu huu na kufikia ukomo mwishoni mwa msimu wa 2030-2031.
Klabu na mabilioni kila msimu
Ili kuongeza ushindani, ambao tunaweza kukubaliana kuwa umekuwa ukipungua kutokana na tofauti kubwa ya kiuchumi kati ya klabu moja na nyingine, AML kupitia mkataba wake na TFF wataweka mezani mabilioni ya fedha kila msimu.
Mathalan, AML wataweka kiasi cha Sh bil. 12 kwa msimu ujao, ambapo bilioni nane (67%) itakwenda moja kwa moja kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu, huku sehemu ya fedha iliyobaki ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya soka, TFF na Bodi ya Ligi.
Usichokifahamu ni kwamba, kiasi cha fedha kitapanda kila msimu. Msimu unaofuata (2022-23), AML itatanua mfuko kwa kuweka mezani Sh bil 13.2 na hapo unaweza kuona fungu la klabu likiongezeka na kufikia Sh bil. 8.8.
Ikiwa ni katika kipengele cha ongezeko hilo, AML itaweka Sh bil 28, ikiwa na maana kwamba klabu zitavuna Sh bil. 19 katika msimu wa mwisho (2030-31) na huo utakuwa mwisho wa mkataba wake na Shirikisho (TFF).
Vita nzito kwa Yanga, Simba, Azam
Kwa kufuata historia, timu hizo hupewa nafasi ya kutwaa ubingwa kila msimu unapoanza na hiyo inatokana na mafanikio na uimara wake kiuchumi. AML wameongeza vita kati ya timu hizi kwa kuweka zawadi kwa ile itakayotwaa ‘ndoo’.
Iko hivi, kwa misimu mitatu mfululizo ijayo (2021-22 hadi 2023-24), AML itakuwa ikimpatia bingwa kitita cha Sh mil. 500, huku timu itakayomaliza katika nafasi ya pili ikijichukulia asilimia 50 ya mkwanja huo (Sh mil. 250). Timu ya tatu itapewa Sh mil. 225, wakati ile itakayofunga ‘top four’ ikijiondokea na Sh mil. 200.
Dau litakuwa likiongezeka. Mfano, bingwa wa misimu mitatu ya mwisho wa mkataba (2028-29, 2029-30 na 2030-31), atanyakua Sh mil. 700, nafasi ya pili itakuwa na Sh mil. 325, mshindi wa tatu atapata Sh mil. 275, huku timu itakayohitimisha top four ikijibebea Sh mil. 250.
Hata ‘play-off’ bado mkwanja tu
Hata timu zitakazomaliza msimu zikiwa nje ya nafasi nne za juu bado zimefikiwa na mkono wa AML na hapa utakuwa sahihi kusema AML wameonesha kwa vitendo dhana ya motisha ilivyo na tija kwenye soka la ushindani.
Kwa misimu yote mitatu ijayo, timu itakayomaliza nafasi ya tano itapewa Sh mil. 65, inayofuata itapewa Sh mil 60, nafasi ya saba itapata Sh mil 55, itakayokuwa nyuma yake itapokea Sh mil 50, huku timu ya tisa kwenye msimamo ikiondoka na Sh mil. 45.
Kama hiyo haitoshi kwenye motisha, timu itakayomaliza nafasi ya 10 nayo itachukua Sh mil. 40, ikayofuata itanyakua Sh mil 35, nafasi ya 12 itakuwa na Sh mil. 30, wakati itakayokuwa ya 13 itajihakikishia Sh mil. 25.
Cha kufurahisha zaidi, AML haikuiacha nyuma timu itakayojikuta imevurunda na kuangukia kwenye play-off’ (mechi za kuamua hatima ya kubaki Ligi Kuu au kushuka daraja). Mkono wa sapoti kutoka kwa AML utaipatia Sh mil. 20 za kujiandaa na hatua ngumu hiyo.