11.3 C
New York

Infographic| Askofu Gwajima, Silaa kwenye mtego wa kihistoria

Published:

HIVI karibuni, siasa za Tanzania zilishuhudia Bunge likiazimia adhabu ya kuwafungia vikao viwili wabunge na makada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Josephat Gwajima anayewakilisha Jimbo la Kawe na Jerry Silaa wa Ukonga.

Wawili hao ‘walikaangwa’ kupitia Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Nne wa Bunge la 12 kilichokaa Agosti 31 jijini Dodoma.

Adhabu ya Gwajima ilikuja baada ya ukosoaji wake wa muda mrefu juu ya chanjo ya Corona, mjadala uliotikisa nchi kutokana na vita ya maneno kati yake na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima.

Kwa upande wake, Silaa alishukiwa na rungu baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujiridhisha kuwa alidanganya umma kwa madai yake kuwa wabunge hawakatwi kodi.

Gwajima alianzaje kulikoroga?

Ilikuwa Mei 11, mwaka huu, ambapo Askofu Gwajima alianza kuibua mjadala juu ya chanjo alipokuwa akichangia mapendekezo katika muswada wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya (2021-2022) uliowasilishwa Bungeni na Waziri wake, Dkt. Gwajima.

“Leo nataka kuzungumzia chanjo za Corona. Kuna chanjo ambayo imeruhusiwa kuanza kutumika inaitwa Jonson Jonson. Watengeneza chanjo wenyewe wanasema madhara ya chanjo hii ni kushindwa kupumua sawasawa, kuvimba kwenye uso, mapigo ya moyo yanakwenda haraka na damu kuganda.

“Kama watengeneza chanjo wenyewe wanaonyesha kwenye ‘website’ (tovuti) yao kuwa kuna shida hiyo, basi sisi tuwe makini najua mheshimiwa Rais ameshaunda kamati lakini mimi kama Mbunge nina haja ya kujadili na ‘ku-alert’ wawe makini wanapochagua aina ya chanjo hizi,” alisema Askofu Gwajima.

Kuanzia hapo, Askofu Gwajima aliendelea kutumia Mahubiri ya Kanisani kwake kuhamasisha mgomo dhidi ya zoezi la uchanjaji, hali iliyomwingiza kwenye vita ya maneno na Waziri wa Afya, Dkt. Gwajima.

Silaa naye ilikuwaje?

Silaa naye alijikuta hatiani kwa kauli yake ya Julai 24, mwaka huu, aliposema imefikia hatua wabunge waanze kulipa kodi kupitia mishahara yao na si kuwaachia wananchi mzigo huo. “Ni wakati mwafaka sisi waheshimiwa wabunge ili tupate uwezo wa kuwaambia watu waanze kulipa kodi na sisi tuanze kulipa kodi katika mishahara yetu…”

Walivyoingia kwenye ‘18’ za Kamati

Kwa mara ya kwanza, ilikuwa Agosti 21, mwaka huu, ndipo Gwajima na Silaa walipopokea wito wa kutakiwa kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Gwajima alifika siku mbili baadaye (Agosti 23), kisha Silaa ‘alijikabidhi’ Agosti 24.

Baada ya kuhojiwa siku ya kwanza, Gwajima alirejea mbele ya Kamati hiyo siku mbili baadaye (Agosti 25), wakati Silaa aliyetakiwa kufika tena Agosti 26 aliingia mitini.

Kamati na historia ya ‘kutumbua’

Huenda Kamati hii ni ngeni kwa wengi, hivyo ikaonekana ni ajabu kwa wabunge kuweka kitimoto na hatimaye kushukiwa na rungu.

Kwa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania, watakumbuka makali ya Kamati hii enzi za Bunge la Samwel Sitta (2005-2010), ambapo aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini wakati huo, Zitto Kabwe, alifungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kosa lake la kutoa shutuma dhidi ya baadhi ya mawaziri.

Aidha, Kamati hii pia ‘ilichanua’ wakati wa Bunge la Anne Makinda (2010-2015) kwa kuwazuia kuhudhuria vikao vya Bunge wawakilishi wa upinzani; Highness Kiwia, Ezekiel Wenje na wengineo kwa kosa la kupuuza mamlaka ya Spika.

Ni kama ilivyokuwa kwa Bunge la awamu ya kwanza la Job Ndugai (2015-2020) lilipowafungia kushiriki vikao wabunge Zitto Kabwe, Godbless Lema, John Heche, Halima Mdee, Esther Bulaya, Pauline Gekul na Tundu Lissu.

Awamu ya pili hii ya Bunge la Ndugai, kwa maana ya 2020-2025, ndipo inaposhuhudiwa Gwajima na Slaa wakiingia kikaangoni.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img