Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Serikali imesema kuwa ipo tayari kushirikiana na waandaaji wa Tuzo za Muziki wa Injili Afrika Mashariki ‘East Africa Gospel Awards’,(EAGMA) ili kusaidia kuzifikasha mbali zaidi katika kuhakikisha vipaji vya wanamuziki vinazidi kukua.
Hayo yamebainishwa naKatibu Mtendaji wa Baraza Sanaa la Taifa (BASATA), Dk.Kalman Mapena wakati wa uzinduzi wa tuzo hizo.
Mapena amesema tuzo hizo ni za kihistoria kwa sababu zinafanyika kwa mara ya kwanza hivyo ni vema kuhakikisha zinasimamiwa kikamilifu katika kuhakikisha zinakuwa endelevu.

uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
“Mawazo yenu yawe ya muda mrefu yanayotekelezeka na yanadumu, kumuimbia Mungu ni kusali mara mbili, hivyo waliojitolea kumuimbia Mungu wanatusaidia kusali mara mbili,”amesema.
Amesema wazo hili la uwepo wa Tuzo hizo lisiangalie tu kwa nchi za Afrika Mashariki pekee ila liende mbali zaidi kwa nchi zote za Afrika.
Naye Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Muziki Tanzania, Ado November, amesema kuwa Tanzania imeshirikiana na (EAGMA) zikihusisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Congo, na Sudani Kusini.
November ameongeza kuwa tuzo hizo zitakuwa faraja kwa wasanii wa muziki wa injili nchini, kwani jitihada zao za muda mrefu sasa zinakwenda kuleta matunda.

“Muziki huu sasa utawafuta machozi wasanii wetu baada ya kuufanya kwa muda mrefu, lengo la tuzo hizi ni kuwaleta pamoja wanamuziki wa injili ambao wanafanyakazi kubwa katika kuelimisha na kuburudisha jamii yetu kwa ujumla,” amesema.
Aidha amesema tuzo hizo zinatarajiwa kuinua na kuthamini mchango wa wasanii wa injili katika ukanda wa Afrika Mashariki, huku zikitoa jukwaa la kuutangaza muziki wao kimataifa.
Kwa upande wake Muandaaji wa tuzo hizo, Magreth Chacha amesema EAGMA inaunganisha wasanii, mashabiki na wataalamu wa sekta ya muziki kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Amesema madhumuni ya kuanzisha tuzo hizo ni pamoja na kuvuna nafsi kwa kristo kupitia nguvu ya muziki wa injili hasa kwa vijana ambao mara nyingi wanapotea kwenda kuimba muziki wa kidunia.
“Tunajitahidi kutengeneza muziki wa kuleta mabadiliko ya kudumu katika kusherehekea vipaji vya muziki wa dini.
“Tukio hili la tuzo za injili kwa nchi za Afrika Mashariki ni tukio la matumaini hamasa na imani zinazokutana katika kusherehekea nguvu za muziki wa injili,”amesema.