Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameliomba bunge kuidhinisha makadirio ya bajeti ya jumla ya Sh 224.98 bilioni kwa ajili ya kutekeleza shughuli za wizara na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo bungeni leo, Mei 2, 2025, Mavunde imetaja vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa.
Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati,kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito pamoja na kuongeza uwekezaji kwenye yafiti za kina za madini.

Pia kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini.
Ameongeza kuwa mchango wa sekta ya madini umeimarika kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024. Pia, shughuli za uchimbaji madini zimekua, maduhuli ya Serikali yameongezeka, na zaidi ya maeneo 142 ya biashara ya madini yamepewa hadhi.
Ameeleza kuwa wizara hiyo imefanikiwa kuvuka lengo la kuchangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa mwaka mmoja kabla ya muda ulioanishwa katika Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 hadi 2025/26, na kufikia mchango wa asilimia 10.1 mwaka 2024.

“Mafanikio haya yanatokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25,” amesema.
Mavunde amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo, ili kuwahamasisha kufanya uwekezaji wenye tija katika sekta hiyo.
Amesema moja ya mikakati ya msingi ni kuhamasisha taasisi za kifedha kutoa mikopo ya fedha na vifaa kwa wachimbaji wadogo, ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Ameeleza kuwa Serikali pia itaendelea kuboresha vituo vya mfano kwa lengo la kutoa huduma na mafunzo bora kwa wachimbaji wadogo, sambamba na kuimarisha huduma za uchorongaji, ili kuwasaidia kupata taarifa sahihi za kijiolojia kabla ya kuanza uchimbaji.

“Wizara itaendelea kutekeleza mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo rasmi ya uchimbaji na kuwapatia leseni katika maeneo yenye taarifa za uhakika za kijiolojia,” amesema Mavunde.
Aidha ametoa wito kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kujiepusha na utoroshaji wa madini akisisitiza kuwa ni harasa kwa biashara zao na Taifa kwa ujumla.
Amesema Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini nchini Tanzania kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali, hasa katika mikoa ya Geita, Ruvuma, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha.