4.1 C
New York

OSHA yaeleza jinsi TEHAMA inavyorahisisha usimamizi wa usalama na afya

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeeleza kuwa matumizi ya mifumo ya TEHEMA umeiwezesha Taasisi hiyo kupata taarifa muhimu kuhusiana na mtawanyiko wa shughuli za kiuchumi nchini na hivyo kuweza kuandaa mipango madhubuti ya kulinda nguvukazi inayotumika katika shughuli husika dhidi ya vihatarishi vya magonjwa na ajali mahali pa kazi.

Mkuu wa Kitengo cha TEHEMA wa OSHA, Raymond Machary, akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa TEHAMA katika usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi katika  Mkutano wa 4 wa Serikali Mtandao uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha TEHEMA wa Taasisi hiyo, Raymond Machary, mara baada ya kuwasilisha mada kuhusu umuhimu wa TEHAMA katika usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya katika ­Maneo ya kazi.

Machary amesema Taasisi ya OSHA imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA ambapo inao mfumo wake wa ndani wa usimamizi wa taarifa za maeneo ya kazi (Workplace Information Management System) ambao umeunganishwa na mifumo mingine ya serikali ukiwemo mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG).

“Kupitia matumizi ya mfumo wetu wa WIMS na mifumo mingine ya serikali, Taasisi yetu imeweza kukusanya na kuhifadhi taarifa muhimu kuhusiana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika nchini jambo ambalo linarahisisha usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi husika. Aidha, kupitia mfumo huo wadau wetu wanaweza kupata huduma zetu ikiwemo usajili wa maeneo yao ya kazi bila kulazimika kufika katika ofisi za OSHA,” ameeleza Machary na kuongeza:

“Mathalani sisi OSHA tunao uwezo wa kutoa taarifa za miradi ya ujenzi yote inayoendelea nchini wakati wowote ambapo kwa sasa mkoa wenye miradi mingi ni Dar es Salaam ukifuatiwa na Dodoma na Arusha jambo ambalo lilikuwa haliwezekani kabla ya kuwekeza katika mifumo ya TEHEMA,”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja (Director of Corporate Services) wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), CPA Salum Rugambwa, ameipongeza Taasisi ya OSHA kwa kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya TEHEMA.

“OSHA wanao mfumo wao wa ndani ambao waliutengeneza kwa kuzingatia taratibu zote za serikali zinazosimamiwa na eGA na sisi kama wadhibiti wa serikali mtandao tunaendelea kushirikiana nao pamoja na Taasisi nyingine za umma ili kuhakikisha kwamba mifumo iliyopo inafanya kazi kwa ufanisi ikiwemo wataalam wetu kutoa msaada pale mifumo inapopata changamoto,” amesema CPA Rugambwa.

Soma pia: https://gazetini.co.tz/2022/03/13/infographic-osha-inavyosaidia-kukuweka-salama-kazini/

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img