Na Faraja Masinde, Gazetini
Maisha ya wanawake 556 wanaofariki dunia kutokana na uzazi yanaweza kuokolewa iwapo tu uwekezaji utafanyika kwa Wakunga.
Aidha, vifo vya watoto 67 chini ya miaka mitano kwa kila vizazi hai 1,000 vinaweza kuokolewa sawa na ilivyo kwa vifo 25 vya watoto wachanga katika kila vizazi hai 1,000.
Haya yote yanaweza kudhibitiwa iwapo Serikali na wadau wataamua kutiliamkazo kwenye sekta ya Wakunga nchini.
Takwimu zinabainisha kuwa kwa Tanzania upungufu wa Wakunga ni asilimia 52 huku kwa dunia nzima wakihitajika wakunga 900,000.
Hata, hivyo uwapo uwekezaji utafanyika kikamilifu ikiwamo kuzalisha wakunga wa kutosha wenye sifa na weledi unaohitajika pengo hilo linaweza kushuka hadi 750,000 ifikapo mwaka 2030.
Hali ilivyo nchini
Wakati mahitaji yakiwa hivyo, Takwimu za mwaka 2021 kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga(TNMC) zinaonyesha kuwa Wakunga na Wauguzi waliopo nchini ni 46,000 huku wale waliosajiliwa na kupewa leseni wakiwa 8,983 tu.
Feddy Mwanga ni Rais wa Chama cha Wakunga nchini Tanzania(TAMA) ambapo anasema kuwa iwapo uwekezaji utafanyika kikamilifu basi maisha ya watu wengi yataokolewa.
“Takwimu zinaonyesha kuwa uhaba wa Wakunga Tanzania ni asilimia 52, lakini kwa duniania nzima upungufu ni wakunga 900,000 na iwapo jitihada zitafanyika basi inaweza kupunguza pengo hiki hadi kufikia 750,000 kufikia mwaka 2030.
“Hivyo ifahamike kwamba kama tutawekeza vizuri kwa Wakunga wanaweza kuokoa vifo milioni 4.2 vya akina mama ifikapo mwaka 2035, kwani wanaweza kufanya kazi kwa asilimia 90 katika afya ya uzazi kwa kina mama na watoto wadogo, kwani pia mkunga anajukumu la kuhakikisha kuwa wote wawili wanakuwa salama,” amesema Mwanga.
Ameongeza kuwa jitihada nyingi zimeendelea kufanyika katika kuhakikisha kuwa idadi ya wakuunga inaongezeka ikiwamo kufikia maeneo ya vijijini ili kuokoa maisha.
“Wakunga wamekuwa wachache sana na hata wenye ujuzi bado hawatoshelezi, kama tunavyojua kuwa vifo vya kina mama vitokanavyo na uzazi bado ni changamoto katika nchi yetu na imedhihirika kuwa bado kuna umuhimu wa wakunga, hivyo Vyombo vya habari mna mchango mkubwa wa kuhakikisha kuwa mnafikisha ujumbe huu.
“Juhudi zaidi zinafanyika kuhakikisha kuwa wakunga wanaoajiriwa wanaenda vijijini, ajira nyingi zinapitia kwa wakurugenzi na ndiyo maana wanajitahidi kuwavuta kwenye maeneo ya vijijini kwa kuwapatia nyumba za kukaa,” amesema Mwanga.
Sababu za vifo kwa wajawazito
Mwanga anasema kuwa kuna sababu kadhaa ambazo zinachangia kuwapo kwa vifo vya akina mama wakati na baada ya kujifungua.
“Kwanza, asilimia 25 inasababishwa nakutoka dani nyingi baada ya kujifungua, asilimia 17 ni kifafa cha mimba, asilikmia 19 ni utoaji mimba usio salama.
“Nyingine ni uzazi pingamizi ambao unachangia vifo vya akina mama kwa asiliamia 11 na uambukizo ambao unachangia vifo kwa asilimia 11,” anasema Mwanga.
Vifo kwa Watoto
Akizungumzia vifo kwa watoto wachanga Mwanga anasema kuwa kumekuwa na sababu nyingi ikiwamo kushindwa kupumua kwa mtoto kunakochangia asiliamia 11.
“Pia asilimia 25 ni kutokana na kuzaliwa kabla ya kufikia siku na asilimia 20 ni uambukizo,” anasema Mwanga.
Tunawezaje kuzuia vifo hivi
Mwanga anasema kuwa kama taifa inawezekana kudhibiti aina hiyo ya vifo kwa kufanya mambo kadhaa ya msingi ikiwamo wakunga kupata elimu kulingana na viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
“Pia Serikali iajiri wakunga wenye stadi kulingana na idadi ya wateja wanaowahudumia tofauti na sasa ambapo wakunga niwachache na mahitaji nimakubwa.
“Eneo jingine ni kuendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma ikiwamo vifaa tiba, dawa muhimu na nyumba karibu na vituo vya kutolea huduma ,” anasema Mwanga Rais wa TAMA ambayo ilianza ikiwa na wananchama 100 pekee na sasa wapo zaidi ya 4,000.
Mchango wa UNFPA
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA), limekuwa bega kwa bega na wakunga kote duniani katika kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kikamilifu.
Felista Bwana kutoka UNFPA anasema kuwa wamekuwa wakishikamana na wakunga katika kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Wakunga duniani ambayo hufanyika Mei 5 ya kila mwaka lengo likiwa ni kukumbuka mchango wao katika kuimarisha afya ya uzazi kwa kina mama na watoto.
“Wakunga wamekuwa na mchango mkubwa katika kutoa huduma bora wakati wa zazi na ndio maana tumekuwa tukikumbuka mchango wa wakunga nchini, hadi kufika mwaka 2022, UNFPA imesaidia nchi 120 duniani kuhakikisha kuwa zinapunguza vifo vya mama na mtoto,” anasema Mbwana.