9.5 C
New York

Mamady Doumbouya; Luteni wa jeshi aliyepindua Serikali Guinea

Published:

SIASA za Afrika Magharibi zimetikiswa na tukio la mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo jeshi la Guinea liliamua kushika hatamu kwa kuipindua Serikali ya Rais Alpha Condé.

Aliyesimamia mapinduzi hayo ya Jumapili si mwingine, bali ni kiongozi mwandamizi wa jeshi, Luteni Mamady Doumbouya.

Kwa mujibu wa Luteni Doumbouya mwenye umri wa miaka 41, jeshi lililazimika kufanya hivyo kutokana na sababu kuu tatu; kukithiri kwa rushwa, ukandamizaji wa haki za binadamu, na mdororo wa uchumi.

Huku jumuhiya za kimataifa, kwa maana ya Umoja wa Mataifa (UN) na ule wa Afrika (AU) zikilaani, Luteni Doumbouya alikiri kumshikilia Rais Conde akisisitiza kuwa bosi wake huyo yuko salama kabisa.

Ni nani huyo Doumbouya?

Luteni Doumbouya anatajwa kupata mafunzo ya kijeshi katika nchi za Israel, Senegal, Gabon, na Ufaransa.

Ni mwandamizi wa jeshi akiwa na uzoefu wa miaka zaidi ya 15 na ameshiriki vita mbalimbali, zikiwamo za Afghanistan, Ivory Coast, Djibouti na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Alirejea Guinea mwaka 2018 akitokea Ufaransa alikokuwa akifanya kazi za kijeshi na ni Rais Conde ndiye aliyemuomba kurejea nchini na kulitumikia jeshi la taifa lake.

Lengo la Rais Conde kumtaka arejee ni kuingia kuongoza kikosi cha kukabiliana na ugaidi na matukio ya utekaji meli yaliyokuwa yameshamiri nchini humo.

Umoja wa Ulaya (EU) unamtambua kuwa ni mmoja kati ya vigogo 25 nchini Guinea walioshiriki kwa kiasi kikubwa katika vitendo vya ukandamizaji wa haki za binadamu chini ya utawala wa Rais Conde.

Nini kilichomponza Rais Conde?

Aliingia madarakani mwaka 2010 akiwa ni rais wa kwanza kuingia madarakani kwa njia ya demokrasia. Muda mchache baada ya kuapishwa, mwanasiasa huyo wa zamani wa upinzani, ambaye ana umri wa miaka 83, alinusurika kuuawa.

Conde aliyechaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, anaelezwa kuponzwa na kitendo chake cha mwaka jana, alipotangaza mabadiliko ya Katiba ili awanie tena awamu ya tatu na si miwili inayofahamika.

Itakumbukwa kuwa maandamano ya kupinga hatua yake hiyo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 20, hivyo kulaaniwa vikali ndani na nje ya nchi hiyo.

Guinea ilikuwa kwenye hali mbaya zaidi kwa miaka mitatu (2013 – 2016), chanzo kikiwa ni ugonjwa wa Ebola ulioua watu 11,000.

Ripoti juu ya utawala wake ilionesha kuwa Conde ametimiza ahadi 40 kati ya 315 alizokuwa ameahidi, sawa na asilimia 13 tu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img