24.4 C
New York

Waziri Mkuu awataka wanahabari kutumia Akili Mnemba kama nyenzo na si kikwazo

Published:

Mwandishi Wetu, Gazetini

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka  waandishi wa habari nchini kutumia Akili Mnemba (IA) kama nyenzo ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo na si kikwazo cha uhuru wao.

Amesema kuwa katika dunia ya sasa, vyombo vya habari vinakutana na changamoto mpya zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo Akili Mnemba inachukua nafasi kubwa katika uzalishaji na usambazaji wa habari.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Aprili 29, 2025, katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yalifanyika  kitaifa Jijini Arusha.

Amesema Serikali inaendelea kuandaa sera maalum ya Akili Mnemba, ambayo itatoa mwongozo wa matumizi yake katika vyombo vya habari ili kuhakikisha kuwa teknolojia hiyo inaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi, na uadilifu wa uandishi wa habari.  

“Ni ukweli usiopingika kwamba, Akili Mnemba inaweza kuwa msaada mkubwa kwa wanahabari, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha changamoto kubwa ikiwa haitatumika kwa busara. Hili linahitaji mjadala wa wazi, sera madhubuti, na ushirikiano wa karibu kati ya sekta zote,” amesema Waziri Mkuu.

Ameeleza Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika maendeleo ya Taifa, kwa kupitia vyombo hivyo, imeweza kuwahabarisha wananchi kuhusu shughuli na mipango ya Serikali, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kimaendeleo.

Amesema viongozi wanatambua na kuthamini mchango mkubwa wa waandishi wa habari na vyombo vya habari katika kuhabarisha jamii, kuhimiza uwajibikaji na kuimarisha demokrasia nchini.

Aidha, wanawahimiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi, maadili na uzalendo kwa ajili ya mustakabali wa wananchi na dunia kwa ujumla.

Majaliwa amesema vyombo vya habari vimekuwa sehemu muhimu katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu ya uzalishaji, ujasiriamali, na maendeleo ya kijamii.

Waziri Mkuu ameongeza kwa kusema kuwa vyombo vya habari vimekuwa na nafasi kubwa katika kulinda na kudumisha amani, umoja, na mshikamano wa kitaifa na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuijenga taswira chanya ya Tanzania kimataifa.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema  Akili Mnemba isiwafanye waandishi wa habari nchini wakafubaa na badala yake wahakikishe wanaitumia vizuri katika utekelezaji wa majukumu  yao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa ametumia fursa hiyo kuwapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kupambania matumaini ya wananchi.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2025 inasema: “Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba (AI) katika Uhuru wa Vyombo vya Habari.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img