17.1 C
New York

Vipaumbele vitano Ofisi ya Msajili wa Hazina 2025/26

Published:

Na Ramadhan Hassan, Gazetni-Dodoma

SERIKALI imewasilisha mbele ya Bunge vipaumbele vitano vya Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) kwa mwaka wa fedha 2025/26, ambavyo vinakusudia kuongeza ufanisi wa taasisi za umma, kuboresha usimamizi wa rasilimali za umma na kukuza mapato yasiyo ya kodi.

Vipaumbele hivyo viliwasilishwa Alhamisi, Aprili 24, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai 1, 2025. Katika bajeti hiyo, serikali imeomba kuidhinishiwa Shilingi bilioni 148.63 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali.

Miongoni mwa vipaumbele vya OMH ni utekelezaji wa Mpango wa Muda Mrefu wa Miaka 25, unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2025/26 hadi mwaka 2049/50. Mpango huu utatoa mwongozo wa muda mrefu kuhusu maeneo ya uwekezaji, usimamizi wa mali za serikali na mwelekeo wa kiuchumi unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Aidha, Prof. Mkumbo alieleza kuwa serikali itaendelea kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mali za serikali zilizo chini ya usimamizi wa OMH pamoja na zile zilizobinafsishwa, zikiwemo mashamba, viwanda, nyumba na viwanja. “Lengo ni kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali hizo kwa manufaa ya umma,” alisema.

Kwa upande wa matumizi ya teknolojia, Waziri alisema serikali imepanga kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa OMH katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi. “OMH iko kwenye mchakato wa kuboresha matumizi ya TEHAMA kwa kuandaa dashibodi itakayorahisisha utekelezaji wa majukumu,” alisema.

Maboresho haya yanatarajiwa kuwezesha upatikanaji wa takwimu kwa wakati, kuongeza uwazi na kurahisisha usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi. Kutokana na umuhimu huo, mashirika ya umma yameshauriwa kutenga bajeti za kuwekeza kwenye mifumo ya TEHAMA inayosomana.

Katika mwaka wa fedha 2025/26, OMH pia itajikita katika kuboresha usimamizi wa taasisi na mashirika ya umma, kampuni tanzu pamoja na zile ambazo serikali ni mbia. Hili litahusisha matumizi ya miongozo maalum kuhusu majukumu ya wajumbe wa bodi, tathmini ya utendaji kazi na nafasi ya wawakilishi wa serikali kwenye taasisi ambamo ina hisa chache.

Miongozo hiyo ni pamoja na Waraka wa Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2023, Mwongozo wa Majukumu na Matarajio ya Serikali kwa Wajumbe wa Bodi, Mwongozo wa Tathmini ya Utendaji wa Bodi za Wakurugenzi na Mwongozo wa Wawakilishi wa Serikali katika Taasisi zilizo na umiliki mdogo.

Vilevile, ofisi hiyo itajielekeza katika kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa watumishi wake kwa kuwajengea uwezo zaidi ili kuongeza tija na ufanisi kazini.

Kwa upande wa mapato, Serikali kupitia OMH imepanga kukusanya Shilingi trilioni 1.56 katika mwaka wa fedha 2025/26. Mapato haya yatatokana na vyanzo visivyo vya kodi kama vile gawio kutoka mashirika ya umma, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, mapato kupitia mfumo wa TTMS, rejesho la mikopo, riba na mapato mengineyo.

Kiasi hicho kinaonesha ongezeko kutoka Sh trilioni 1.113 zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2024/25. Hadi kufikia Machi 2025, jumla ya Sh bilioni 664.53 zilikuwa zimekusanywa, sawa na asilimia 60 ya lengo la mwaka mzima na asilimia 86 ya lengo la kipindi hicho.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img