2.6 C
New York

Serikali yasisitiza umuhimu wa kuondoa madini ya risasi kwenye rangi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuhimiza hatua za kuondoa madini ya risasi kwenye rangi, likisisitiza madhara makubwa ya kemikali hiyo kwa afya ya binadamu, hasa watoto wadogo.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Viwango na Maendeleo kutoka TBS, David Ndibalema, katika warsha ya siku moja iliyoratibiwa na Taasisi inayojihusisha na utunzaji wa mazingira ya AGENDA kwa ufadhili wa Shirika la Lead Exposure Elimination Project (LEEP) na kukutanisha wadau mbalimbali wa tasnia ya rangi nchini.

Picha ya pamoja.

Ndibalema alibainisha kuwa madini ya risasi yamekuwa yakitumika kwa muda mrefu katika uzalishaji wa rangi, lakini sasa imebainika kwamba yanasababisha madhara makubwa ya kiafya.

“Madhara ya madini ya risasi ni pamoja na shinikizo la damu, upungufu wa damu, matatizo ya mfumo wa fahamu, na athari kubwa kwa watoto, ikiwemo kuathiri ukuaji wao kiakili na kiafya,” alisema Ndibalema, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TBS.

Kwa mujibu wa Ndibalema, Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) limekuwa likihamasisha kuachana kabisa na matumizi ya risasi kwenye rangi kutokana na madhara hayo.

“TBS tumeweka viwango vya chini kabisa vya risasi kwenye rangi, tukiamini kuwa teknolojia mbadala ya kuzalisha rangi salama zaidi ipo,” aliongeza Ndibalema, huku akibainisha kuwa shirika hilo linaendesha kampeni ya kuondoa kabisa madini ya risasi kwenye rangi.

Mkurugenzi wa Viwango na Maendeleo kutoka TBS, David Ndibalem, akifungua warsha hiyo.

Ushirikiano katika kuzuia matumizi ya risasi kwenye rangi

Vera Swai, kutoka Taasisi ya AGENDA inayojihusisha na utunzaji wa mazingira, alieleza kuwa kwa kushirikiana na TBS pamoja na Shirika la LEEP ya Uingereza, wamekuwa wakiandaa mikutano ya wadau wa tasnia ya rangi ili kujadili njia bora za kuondoa madini ya risasi kwenye rangi zinazouzwa nchini.

“Kwa sasa, asilimia 32 ya rangi zinazouzwa nchini Tanzania zina madini ya risasi, kiwango ambacho ni pungufu ikilinganishwa na asilimia 64 mwaka 2015. Ingawa tumepiga hatua, bado kiwango hiki ni kikubwa, na wazalishaji wanapaswa kufuata viwango vya TBS ili kulinda afya ya jamii,” alisema Swai.

Aidha, Yohana Goshshi kutoka Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Sumu kilicho chini ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) alisema kuwa mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya risasi na inafanya utafiti kwenye masoko yanayouza rangi.

Yohana Goshshi kutoka Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Sumu kilicho chini ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA)?

“Tumeanza kufanya utafiti na matokeo yake tutayatoa hivi karibuni. Kando na rangi, tunachunguza pia bidhaa nyingine zenye viwango vya hatari vya madini ya risasi, kama vile betri za sola,” aliongeza Goshshi.

Madhara ya risasi kwa watoto na watu wazima

Afisa Programu Mkuu wa AGENDA, Silvani Mng’anya, aliainisha madhara makubwa ya risasi kwa watoto, akisema kuwa yanaweza kuathiri ukuaji wa ubongo na kusababisha matatizo ya uelewa.

Afisa Programu Mkuu wa AGENDA, Silvani Mng’anya, akizungumza wakati wa warsha hiyo.

“Madini ya risasi yanaweza kusababisha upungufu wa uwezo wa mtoto kuelewa, mabadiliko ya tabia, na ugumu wa kufikia malengo ya kimasomo,” alisema Mng’anya. Pia aliongeza kuwa risasi inasababisha shinikizo la damu, upungufu wa damu, na matatizo katika figo, ini, na mfumo wa uzazi.

Takwimu za Kimataifa kuhusu madhara ya risasi

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya vifo bilioni mbili vilivyotokea mwaka 2019 vilihusishwa na madhara ya kemikali, huku asilimia 50 ya vifo hivyo vikitokana na risasi. Zaidi ya watoto milioni 815 duniani wameathirika na sumu ya risasi, huku watoto 1,540,000 wakifariki dunia kila mwaka kutokana na athari za madini haya.

Dk. Scott Matwafali, Meneja Mipango wa Shirika la Lead Exposure Elimination Project (LEEP), alisifu hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kupunguza matumizi ya risasi kwenye rangi.

Dk. Scott Matwafali, Meneja Mipango wa Shirika la Lead Exposure Elimination Project (LEEP), akiwasilisha mada katika warsha hiyo.

“Kwa sasa, rangi zenye risasi zinazouzwa Tanzania ni asilimia 32, ukilinganisha na asilimia 77 mwaka 2009. Hii ni hatua kubwa, na tunaamini ifikapo mwaka 2030, Tanzania itaweza kuondoa kabisa risasi kwenye rangi,” alisema Dk. Matwafali.

Jinsi madini ya risasi yanavyoingia mwilini

Madini ya risasi huingia mwilini kupitia rangi zilizochakaa au kuharibika. Vipande vidogo vya rangi hizi huchanganyika na vumbi na udongo na kusambaa kwenye mazingira yanayozunguka nyumba. Kwa watoto, athari hujitokeza zaidi kutokana na tabia yao ya kucheza karibu na ukuta au vifaa vilivyopakwa rangi yenye risasi, na kuweka mikono kinywani. Kwa wakubwa, madini haya huingia mwilini wakati wa kupiga msasa maeneo yaliyopakwa rangi yenye risasi, au kwa kula vyakula vilivyochafuliwa na kemikali hiyo.

Kuchukua tahadhari, kama vile kuepuka matumizi ya rangi zilizo na risasi na kuhakikisha usafi wa maeneo ya nyumbani, ni muhimu katika kupunguza athari hizi na kulinda afya ya jamii. https://leadelimination.org/

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img