1.6 C
New York

Serikali yawekeza Bilioni 1.49 kutatua changamoto ya maji Kibondo

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Kibondo imetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.49 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 1,500,000, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 95.

Mradi huu unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji wilayani Kibondo, mkoani Kigoma, na kuboresha maisha ya kijamii na kiuchumi ya wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza leo Septemba 18, 2024, baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa tanki hilo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema mradi huo unaojengwa na wataalamu kwa kushirikiana na vijana wa Kitanzania utapunguza mgao wa maji na kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kwa siku. Aliwataka wakazi wa Kigoma kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha mradi huo unadumu kwa muda mrefu.

“Maji yalikuwa machache na yenye tope kutokana na ukosefu wa chujio. Ninawaomba mvilinde vyanzo vya maji. Ukikata miti hovyo na kuchoma mashamba, itasababisha ukame licha ya kuwa na tanki hili. Tunahitaji vyanzo vilindwe ili maji yaendelee kupatikana kwa muda mrefu,” alisema Dk. Biteko.

Ameongeza kuwa mradi huo utaongeza muda wa upatikanaji wa maji kutoka saa nne hadi saa 12 kwa siku, hivyo kuboresha huduma kwa wakazi wa Kibondo.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amewataka wananchi wa Kigoma kushirikiana na kuepuka migogoro ili waweze kuleta maendeleo kwa pamoja.

Shukrani kwa Rais Samia

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo mkoani Kigoma. Amesema kuwa fedha hizo zimejumuisha ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza meli, kiwanda ambacho hakipo popote Afrika Mashariki na Kati.

Aidha, Andengenye ameeleza kuwa fedha pia zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa Meli ya MV Liemba, ambayo itakapokamilika itaendelea kufanya kazi za usafiri na biashara kati ya Tanzania, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Tutaendelea kusimamia matumizi ya fedha za miradi zinazotolewa kwa maendeleo ya watu wa Kigoma,” aliongeza Mkuu wa Mkoa huyo.

Maendeleo Jimboni Muhambwe

Mbunge wa Kibondo Mjini, Dk. Florence Saminzi, amepongeza juhudi za Serikali katika kuleta mabadiliko makubwa jimboni Muhambwe. Amebainisha kuwa, chini ya uongozi wa Rais Samia, jimbo hilo limepata shule tatu mpya za msingi, kuboresha madarasa, vyumba vya walimu, na kupokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.

“Maendeleo haya ni ushahidi wa juhudi kubwa za Serikali ya Rais Samia katika kuimarisha huduma za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Dk. Saminzi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img