22.9 C
New York

Mtazamo; Kitendawili cha watoto wa mitaani, nani akitegue?

Published:

Na Yohana Paul, Gazetini

WALIZALIWA na mama John, wakalelewa na mama Jose, wakatamani maisha ya watoto wa mama Prince, wakaamua kuondoka makwao na sasa wapo mtaani wanaomba pesa kwenye gari la baba Jane kama si chakula kwa mama Ntilie.

Wapo Mbagala, Kinondoni, Ubungo, Ilala, Temeke mpaka Kigamboni, wamejaa mitaa ya Makongo Juu, Mbezi Mwisho na hata Kwa Mtogole, wamefurika Kariakoo, mitaa ya Karume, Makumbusho mpaka Mbezi Kwa Msuguli.

Nilipokuwa mdogo niliaminishwa na kuamini hawa wapo jijini Dar es Salaam pekee, nilipobarehe niligutuka na kuwakuta kumbe wapo hata mjini Songwe, Misungwi, Chato, Kahama mpaka kule kisiwani Ukerewe.

Jina lao ni watoto wa mtaani, ukitaka kujua wametoka wapi hamna mwenye jibu moja, kwani wapo waliosafiri kutokea Uyui, Makambako na Njombe na wengine asili yao ni Kwimba na Magu kama siyo Butiama kwa Mwalimu.

Hivi leo hao ndio wamegeuka wenyeji wa mitaa ya Sinza, Keko na Mbagala na wengine wameamua kuwa vibarua wa Mianzini, Tegeta, Tabata na Segerea ingawa baadhi wamejitosa kuwa wadokozi kule Tandare kwa Mtogole.

Hawaishi jijini Dar es Salaam peke yake, bali wapo kila mji, halmashauri, wilaya hadi kwenye zile manispaa zenye tuzo ya usafi wa mazingira, usimamizi thabiti wa sera ya mipango miji na mapato makubwa ya kodi na tozo.

Hii inaashiria kwamba suala la watoto wa mitaani imefikia hatua sasa tunaweza kuita ni janga la kitaifa kwani linamugusa kila mtu pasipo kujali imani, kabila na asili yake na watoto hawa wanazidi kuongezeka kila uchwao.

Ingawa suala hili ni mtambuka, lakini leo hii ukiwauliza ndugu na jamaa watasema watoto wameshindakana, ukiwahoji wanaharakati watakuambia tumeandika dokezo huku wanasiasa watakuomba mitano tena.

Ni kweli kwamba kila mmoja ana hoja yake kuhusu ongezeko la watoto wa mitaani, kila upande una mtazamo tofauti juu ya jambo hili na kila taasisi wana mapendekezo yao kuhusu njia sahihi ya kukabili ongezeko hilo.

Mbali na uwingi wa hoja zilizopo bila kusahau mipango lukuki juu ya kukabiliana na tatizo hili, lakini bado zimeshindwa kuwa na tija na wala hazitoi matumaini ya kuweza kumaliza tatizo la watoto wa mitaani.

Suala la watoto wa mitaani siyo jipya, ila ni kama limeshindikana, kwani wapo waliowahi kuja na mikakati ikatenguliwa, mipango ikapanguliwa na walioandaa maandiko mradi hawajwahi kufanikiwa.

Inatafakarisha na inafikirisha sana kwani mpaka sasa hakuna mwenye jibu kamili juu ya kiini halisi cha tatizo na suluhisho la kudumu kwenye suala hili bali kilichobaki ni kusukumiana mpira mhusika halisi wa watoto hawa.

Wapo wanaoamini chanzo cha tatizo ni malezi dhaifu, wengine wanahisi ni changamoto za kiuchumi huku sababu zingine zikitajwa kuwa ni vishawishi na tamaa pekee ndio vinachangia watoto kutoka majumbani kwenda mitaani.

Huenda kila sababu ikawa inachangia uwepo wa tatizo, lakini hoja kubwa ni nani atategua kitendawili hiki ambacho hadi sasa mtunzi wake hafahamiki na mwenye jawabu halisi hajulikani, kwani tunahitaji suluhu zaidi ya lawama.

Kwa mtazamo wangu natamani kuona suala hili linageuka kubwa ajenda ya kitaifa, ili kila halmashauri inapoweka mipango yake ijumuishe ajenga ya watoto wa mitaani na mikakati halisi ya kuweza kuwasaidia kurejea makwao.

Naamini hili haliwezi kuwa rahisi lakini angalau tunaweza kupiga hatua, na kuchonga barabara iwe ya zege ama ya lami itakayoonyesha uelekeo sahihi wa watoto wa mtaani ili tusiendelee kuzalisha kizazi kilichokengeuka.

Yohana Paul-Mwandishi wa Mtazamo huu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img