11.3 C
New York

Utafiti| Asilimia 15 ya wagonjwa wa VVU wana kiwango cha juu cha sukari

Published:

Na Nora Damian, Gazetini

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umebaini asilimia 15 ya wagonjwa wenye Virusi vya UKIMWI (VVU) wana kiwango cha juu cha sukari huku unywaji pombe na shinikizo la juu la damu vikitajwa kuchangia.

Akizungumza leo Juni 24,2024 na Waandishi wa habari Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Applolinary Kamuhabwa, amesema matokeo ya utafiti huo na nyingine yanatarajiwa kuwasilishwa katika kongamano la 12 la kisayansi la chuo hicho litakalofanyika Juni 27 na 28,2024.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Applolinary Kamuhabwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano la 12 la kisayansi la chuo hicho. Kushoto ni Mkurugenzi wa Tafiti, Machapisho na Bunifu, Dk. Nahya Salim.

Katika kongamano hilo litakaloshirikisha wajumbe zaidi ya 400 kutoka ndani na nje ya nchi, tafiti 80 zitawasilishwa kwa njia ya maongezi na 107 zitawasilishwa kwa njia mabango.

“Tumefanya tafiti zetu kulingana na mwenendo wa hali ya magonjwa duniani na Tanzania, sasa hivi duniani kote kuna mabadiliko ya magonjwa, kisukari, shinikizo la damu, saratani na mengine yanazidi kuongezeka. Kuna mlipuko wa Uviko 19 haya yote yanahitaji kutafutiwa majibu na yanapatikana kwa kufanya tafiti,” amesema Profesa Kamuhabwa.

Matokeo ya tafiti zingine zitakazowasilishwa katika kongamano hio ni upatikanaji wa huduma za wodi maalumu za kulaza watoto wachanga, utafiti uliofanyika Kinondoni ambao umebaini asilimia 54.5 ya wanawake wanatumia vipodozi vya kujichubua wangi wao ni wale wanaofanya mapokezi.

Profesa Kamuhabwa amesema mijadala mingine itahusisha ufanisi wa kugharimia mifumo ya afya nchini ambapo watafiti watawasilisha jinsi nchi itakavyoweza kutekeleza mfumo huo kuleta tija kwa wananchi wote na mifumo bora ya kuishi kulingana na magonjwa yasiyoambukiza.

Aidha amesema tafiti hizo zimeainishwa katika mada ndogo ambazo ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza, afya ya akili, upasuaji na lishe, magonjwa ya kuambukiza na usugu wa vimelea dhidi ya dawa, afya ya mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana rika, utunzaji na afya ya kinywa.

Mada nyingine ni viamuzi vya kijamii kwa afya, utafiti wa mifumo ya afya, tiba mbadala na asili, uvumbuzi wa dawa na maendeleo ya chanjo, masuala mtambuka; maadili na taaluma, akili bandia, teknolojia na afya ya kazini.

Amesema kongamano la mwaka huu litatumika pia kumuenzi aliyekuwa mkuu wa chuo hicho Hayati Rais Ally Hassan Mwinyi aliyefariki Februari 27,2024 ambapo katika miaka 17 alipokuwa mkuu wa chuo kilinufaika kwa mchango wake katika upanuaji wa miundombinu ya kufundishia, kutoa huduma na tafiti ikiwemo kampasi mpya ya Mloganzila.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ‘Sayansi kama hadithi ya maisha; nguvu ya tafiti bunifu na ushirikiano kwenye kuimarisha mifumo thabiti ya afya’ imechaguliwa mahususi kwa sababu mwelekeo wa magonjwa hapa nchini na duniani umekuwa ukibadilika mara kwa mara ambapo changamoto kubwa sasa ni kwenye magonjwa yasiyoambukiza.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img