1.6 C
New York

Ripoti| Wagonjwa wa afya ya akili wanaongezeka nchini

Published:

Na Grace Mwakalinga, Gazetini

KATI ya mikoa  28 iliyopo nchini, mikoa mitano ndio yenye vituo vinavyotoa huduma ya utengamo wa afya ya akili ikiwemo Dodoma na Mbeya.

Kwa mujibu  wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, ya mwaka 2022/2023, ni kwamba wagonjwa wa afya ya akili wanaongezeka kila mwaka na vifo huku moja ya sababu ikiwa  ni upungufu wa vituo vya utoaji huduma kwa jamii.

Sababu nyingine ni kukosekana kwa sera ya afya ya akili  inachangia tatizo hilo, ambapo licha ya kuwepo na sheria iliyorekebishwa ya mwaka 2008 bado haikidhi ipasavyo mahitaji ya sasa kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili.

CAG anaeleza kumekuwa na ukosefu wa umakini katika kutambua watu wenye tatizo la afya ya akili badala yake juhudi za utambuzi zinazingatia makundi mengine yenye udhaifu amesema huduma za kisaikolojia na kijamii hazijaingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti, sera na programu katika ngazi mbalimbali za utawala.

“Kuna uhaba wa wataalamu, miundombinu, vifaa tiba na dawa za kufanikisha utoaji wa huduma za afya ya akili, uhaba huu unahusisha vituo vyote vya afya kutoka ngazi ya kitaifa hadi za kikanda na za wilaya,” imeeleza ripoti hiyo.  

Aidha, inaeleza vituo vya afya vina upungufu mkubwa wa miundombinu ya kuhudumia mahitaji ya wagonjwa wa afya ya akili, kutokuwepo kwa wodi za kutosha kwa watu wazima, watoto na vijana,” imeeleza ripoti.

Pia ripoti hiyo inabainisha kuwa, takwimu Hospitali ya Taifa ya Akili ya Mirembe mwaka 2022 kulikuwa na ongezeko la wagonjwa waliopatiwa matibabu kutoka 3,472 mwaka 2019 hadi  5,060 mwaka 2022 sawa na asilimia 31 ya wagonjwa.

“Mwaka 2022 ripoti ya Wizara ya Afya inaeleza maradhi ya akili yameongezeka kutoka wagonjwa 386,358 hadi  2,102,726 kuanzia mwaka 2012 hadi 2021 sawa na  ongezeko la asilimia 82,” imeeleza  ripoti ya CAG.

Katika mapendekezo yake, CAG, anaitaka  Wizara ya Afya iandae miongozo ya kliniki ya kitaifa na taratibu za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuunda miundombinu ya urekebishaji kwa huduma za afya ya akili.

Pia ihakikishe kuna upatikanaji wa wafanyakazi wenye uwezo na vifaa muhimu kwa ajili ya huduma za afya ya akili.

Akizungumzia  hali ya afya ya akili nchini, Mkurugenzi wa Empower Youth Prosperity, Ipyana Mwakyusa, anasema mzigo wa matatizo ya akili miongoni mwa vijana unasababishwa na  msongo wa mawazo  na matumizi mabaya ya pombe na mihadarati huku waathirika wakubwa wakiwa  vijana wengi wenye umri kati ya miaka 15-39.

Kutokana na hali ya hiyo, anasema Empower Youth Prosperity waliamua kuwezesha vijana katika nyanja mbalimbali za kiafya na kijamii katika kuona namna athari za changamoto za afya ya akili zinazoweza kudhoofisha ustawi wao kwa kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na kutatua matatizo yanayowakabili.

Kupitia program ya BRO FUNGUKA inayoendesha kongamano la kongamano la vijana wa kiume na wanaume kwa miaka sita sasa  limewafikia 4570 na kuwajengea uwezo namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo,  kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia na kujikwamua kiuchumi.

“Kulingana na takwimu wanaume wamekuwa wanapitia vikwazo mbalimbali kwenye jamii na kusababisha madhara ya moja kwa moja kwao na kwa wengine, tumeona wakiongoza kwa kujiua na kuuwa wengine, kijidhuru au kudhuru,” amesema Mwakyusa.

Ameongeza EYP tumekuwa tukifanya kwa kushirikiana na wadau wetu kama vile NASAHA HUB na WOUNDED HEALERS Org ambao husaidia kutoa msaada wa kisaikolojia kwa wale wenye matatizo ya afya ya akili.

Kwa upande wake Daktari wa Afya na magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH), Dk. Raymond Mgeni, katika kipindi cha mwaka 2023 wametoa huduma ya ushauri na matibabu kwa wagonjwa waliofika hospitalini hapo

Anafafanua wagonjwa waliotibiwa kuwa ni Sikizofrenia (Magonjwa ya ufahamu) 1?500, mgonjwa ya hisia (baipola na sonona) 950, magonjwa ya mfumo umeme wa ubongo (kifafa) 460, magonjwa ya matumizi ya vilevi (pombe, bangi) 190  na magonjwa ya wazee hasa ya kukosa kumbukumbu 100.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img