1.4 C
New York

NIDA ilipofikia utoaji wa vitambulisho vya Taifa

Published:

Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) hadi sasa imefanikiwa kusajili watu 24,495,804 kutoa namba za utambulisho kwa watu 20,832,225 na kuzalisha vitambulisho 20,286,420.

Hayonyamebainisha Aprili 15, 2024 jijini Dodoma na Waziri Masauni wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Masauni amesema mwaka 2008 Serikali iliidhinisha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambayo hadi sasa imefanikiwa kusajili watu 24,495,804, kutoa namba za utambulisho kwa watu 20,832,225 na kuzalisha vitambulisho 20,286,420.

Amesema mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imefanikiwa kuondokana na tatizo la upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa lililokuwa likilalamikiwa na wananchi wengi.

“Katika kuhakikisha kuwa tunapoadhimisha miaka 60 ya Muungano tatizo hili linakwisha na kubaki historia, NIDA ilikuja na mpango mkakati wa uzalishaji mkubwa wa vitambulisho vya Taifa (Mass production).

“Sambamba na ugawaji wa Vitambulisho kwa Umma (mass issuance) ulioanza kutekelezwa mwezi Oktoba 2023,” amesema Waziri Masauni.

Amesema zoezi hilo la uzalishaji, usambaji na ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa umma linaendelea katika ofisi za Serikali za Mitaa, Vijiji, Vitongoji na Shehia ambako ndiko vitambulisho vinapelekwa kwa ajili ya wananchi kuvichukua.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeiwezesha NIDA kumaliza tatizo hilo la muda mrefu la upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeiwezesha NIDA kumaliza tatizo la upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar lililokuwa kikwazo kwa wananchi katika kupata huduma mbalimbali za Kiuchumi na Kijamii.

Aidha, kuanzishwa kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo miongoni mwa majukumu yake ni Kusajili na Kutambua Watu, Kujenga na Kutunza Daftari la Kielektroniki (Kanzidata) lenye taarifa za watu.

Pamoja na mambo mengine, kumeisaidia Serikali kuimarisha Ulinzi na Usalama wa raia pamoja na Nchi kwa ujumla.

Amesema Matumizi ya mfumo wa usajili na utambuzi kwa kutumia taarifa za Kanzidata katika masuala ya Ulinzi na Usalama nchini, yamekuwa na mafanikio makubwa kwa Serikali katika nyanja mbalimbali.

“Kusaidia katika kupambana dhidi ya ufadhili wa uhalifu mbalimbali ikiwemo utakatishaji wa fedha kwa kuhakikisha laini za simu zinasajiliwa kwa kutumia utambulisho wa Taifa na akaunti za benki zinafunguliwa kwa kutumia Namba ya Utambulisho wa Taifa,”amesema Waziri Masauni.

Pia, kuwezesha kupambana na makosa ya kimtandao na kusaidia vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kutekeleza majukumu yao.

Amesema Taasisi za Umma na binafsi kadhalika zinatumia Kanzidata iliyojengwa na NIDA kupitia utaratibu wa ushirikishanaji taarifa (Data sharing).

“Utaratibu huu umerahisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo ikiwa ni pamoja na utoaji huduma zao kwa wananchi kwa urahisi na haraka zaidi na hivyo kuokoa fedha na muda,”amesema Waziri Masauni.

Waziri Masauni amesema baadhi ya Taasisi ambazo ni wanufaika wa huduma hiyo ni pamoja na BRELA, TRA, TASAF, ZRB – Zanzibar, NHIF, Benki mbalimbali, Makampuni ya simu na taasisi nyingine kadhaa.

“Bila shaka sote tunajua pia kuwa kupitia Usajili na Utambuzi wa Watu, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewasaidia sana wananchi katika kujiletea maendeleo Kiuchumi na Kijamii,” amesema Waziri Masauni.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img