1.7 C
New York

Tanzania yapunguza vifo vya mama wajawazito mara tano zaidi ya mwaka 2016

Published:

*Nikutoka 556 mwaka 2016 hadi 104 mwaka jana

Na Patricia Kimelemeta, Gazetini

SERIKALI imeweza kupunguza idadi ya vifo vya mama mjamzito kutoka 556 kwa Mwaka 2016 hadi kufikia 104 kwa mwaka 2022.

Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete amesema hayo wakati akifungua kongamano la pili la kisayansi la afya ya mama na mtoto lililofanyika hivi karibuni ambapo pamoja na mambo mengine, ameipongeza serikali kutokana na kuweka mazingira bora ya utoaji wa huduma za afya kwa mama mjamzito na watoto wachanga, jambo ambalo limechangia kupungua kwa idadi ya vifo hivyo.

Kongamano hilo limejumuisha watalam wa sekta ya afya, madaktari wabobezi pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya na uzazi salama wakiwa na lengo la kujadiliana mambo mbalimbali ikiwamo kupunguza vifo vya mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano.

Amesema kuwa, inafedhehesha kuona mama mjamzito ambaye analeta kiumbe duniani anafariki kutokana na kukosa huduma bora za afya wakati serikali imewekeza katika uzazi salama, hivyo basi kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake.

“Ni fedheha kuona mjamzito anafariki kwa ajili ya uzazi, kisa daktari ameshindwa kutimiza wajibu wake wakati serikali imejitahidi kuboresha mazingira ili kuwepo na uzazi salama.

“Ni wakati sasa wa kila mmoja katika sekta ya afya, madaktari na watalaam wengine kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu, kwa sababu uhai wa mama mjamzito na mtoto upo mikononi mwenu, hakikisheni mnafanya kazi kwa weledi na uadilifu ili mjamzito anapojifungua awe salama yeye pamoja na mtoto wake,” amesema Kikwete.

Ameongeza kuwa, kupungua kwa vifo hivyo kutokana na juhudi za serikali za kuboresha mazingira bora ya utoaji wa huduma za afya nchini huku ikienda sambamba na ongezeko la watalaam wa sekta ya afya wakiwamo madaktari bingwa pamoja na vifaa tiba.

Naye Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Mstaafu Kikwete kwa kutambua umuhimu wa uzazi salama ambapo katika kipindi chake za uongozi, mwaka 2014 alizindua Mpango wa huduma bora za afya ya uzazi salama kwa mama mjamzito na watoto.

Amesema kuwa, mpango huo ulilenga kuboresha utoaji wa huduma bora za afya kwa wajawazito na watoto ili kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi.

“Serikali imeweza kuboresha miundombinu ya hospitali mbalimbali nchini pamoja na kuzipandisha hadhi baadhi ya hospitali ili kuhakikisha wanatoa huduma bora za afya.

“Lakini pia imeweza kuweka vifaa tiba vya kisasa kwenye wodi ikiwamo wodi za wajawazito, chumba cha kujifungulia na wodi za watoto wachanga ili waweze kukaa kwenye mazingira bora wakiwa wanapatiwa matibabu,” amesema Mwalimu.

Ameongeza kuwa, licha ya kuboresha mazingira hayo lakini pia serikali imeweza kuongeza watalaam wa afya kuanzia ngazi ya kata hadi Taifa kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa huduma bora za matibabu kwa wananchi,” amesema Mwalimu.

Hata hivyo, Daktari Bingwa kutoa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Profesa Fransis Furia amesema kuwa, vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutokana na serikali kuboresha mazingira bora ya utoaji wa huduma za afya.

“Sasa hivi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ina vifaa vya kisasa ambavyo vinasaidia kutoa huduma bora ya afya ya uzazi kwa mama mjamzito na mtoto, Hali hiyo imesaidia kuwa na uzazi salama hata Kwa watoto wanaozaliwa,” amesema Profesa Furia.

Hata hivyo baadhi ya wajawazito wamesema kuwa, katika kipindi hiki kumekua na utoaji wa huduma bora Kwa wajawazito, tofauti na kipindi kilichopita.

“Zamani ukienda hospitali kujifungua hakuna vifaa wala dawa, vitanda havitoshi mnalala wawili hadi watatu na wengine wanalala chini, inategemea na hospitali unayokwenda, madaktari wachache kwa sababu idadi ya wajawazito ni kubwa, unaambiwa njoo na vifaa vyako pamoja na ndoo ya maji, wakati mwingine ukishajifungua ndugu zako wanaambiwa kuletee maji ya moto kutoka nyumbani, lakini sasa hivi hali ni tofauti, mjamzito ukinda kujiandikisha, unapewa begi la vifaa vya kujifungulia, hakuna ndoo ya maji ya kwenda nayo wala maji ya moto kuyatoa nyumbani kwa sababu kila kitu unapata huko huko,” amesema Mwajuma Othman (32) mjamzito na mkazi wa mtaa wa Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Upendo Lameck (38) mjamzito na mkazi wa Sinza ameipongeza serikali kutokana na kuwepo kwa ongezeko la madaktari katika hospitali mbalimbali, hii inasaidia mjamzito anapoumwa uchungu anapata msaada haraka tofauti na kipindi kilichopita.

“Zamani unaumwa uchungu hakuna daktari wa nesi,usipoangalia unaweza kujifungua mwenyewe halafu na wenyewe ndo wanakuja, wakati mwingine mtoto anakuja amekufa kwa kukosa msaada au kunywa maji ya uzazi, lakini Sasa hivi kidogo ni tofauti hata madaktari na manesi wana nidhamu ya kazi, wakikuona karibu unajifungua hawakai mbali, kila wakati wanakufuata ili kujua hali yako mpaka utakapojifungua,” amesema Lameck.

Sera ya afya pamoja vipaumbele vya Wizara ya Afya kwa mwaka 2022/23/2024 inaitaka serikali kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama mjamzito na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga.

Hata hivyo katika kuhakikisha kulwa mpango huo unafanikiwa, Serikali ilizindua Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto (PJT-MMMAM) ambapo pamoja na mambo mengine, imeboresha utoaji wa huduma za afya kwa mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano kwenye afua tano za afya, lishe, elimu, Malezi yenye mwitikio na ulinzi na usalama. Programu hiyo inalenga watoto wenye umri kuanzia sifuri hadi miaka minane.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img