Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Siah Malle ni mfano mzuri wa mwanamke ambaye amefanikiwa kuvunja dhana iliyojengeka na kuwagawa wanawake na wanaume kwenye uwanja wa taaluma mbalimbali duniani. Safari yake ya kuwa jaji katika Kongamano na Maonesho ya 8 ya Wanawake Wahandisi Tanzania (TAWECE) ni uthibitisho tosha kuwa ari na bidii yake katika tasnia ya uhandisi imezidi kumuinua.
Alipokuwa anakua, Siah alivutiwa na ulimwengu wa sayansi na teknolojia. Kaka yake ambaye ni mhandisi wa ujenzi, alichochea shauku yake katika kuingia kwenye tasnia ya uhandisi na alidhamiria kufuata nyayo zake.
Lakini pia kwa kutiwa moyo na walimu wake, alisoma sayansi na hisabati katika elimu ya sekondari na kufanikiwa kufaulu vizuri katika masomo hayo.
Baadaye Siah aliendelea na elimu yake katika kozi ya uhandisi ngazi ya stashahada ambayo alisoma kwa muda wa miaka mitatu katika Chuo cha Ufundi Arusha.
Mmoja wa walimu wake aliyefahamika kwa jina la John Mbando, alitambua uwezo wake mapema na kumtia moyo katika fani hiyo kisha kumshawishi kuachana na uhandisi wa ujenzi na kubobea katika uhandisi wa mitambo.
Mbando alimshawishi kuwa uhandisi wa mitambo kuwa una manufaa mengi, ikiwa ni pamoja na kuajiriwa, manufaa na kubuni vitu mbalimbali ambavyo vinatatua changamoto au matatizo yanayoikumba jamii.
Hali hiyo ilisababisha mapenzi ya Siah katika uhandisi wa mitambo kuongezeka na alidhamiria kuingia katika taaluma hii.
Baada ya kuhitimu vizuri stashahada yake, Siah alisoma kwa miaka mitatu katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ambako alihitimu Shahada ya Kwanza ya Uhandisi Mitambo na kupata alama zenye wastani wa (GPA) 4.3 na kutunukiwa tuzo ya Mwanafunzi Bora wa Kike aliyehitimu mwaka wa kuhitimu 2019.
Mwalimu wa Siah, Mbando ndiye aliyefanikisha safari muhimu ya mwanadada huyu ambaye sasa ni mhandisi mbobevu.
Hakumfundisha tu ujuzi wa kiufundi wa uhandisi wa mitambo, lakini pia alimjengea dhima nzima ya umuhimu wa kuzingatia maadili, mawasiliano na kufanya kazi kwa pamoja.
Alimhimiza kufuata ndoto zake na kamwe asikate tamaa, hata anapokabiliwa na changamoto. Uzoefu wa Siah ni ushuhuda wa nguvu ya ushauri na athari ambayo mwanamke au mtu yeyote anaweza kuwa nayo kwenye kazi na maisha ya kila siku.
Baada ya kumaliza masomo yake, Siah aliajiriwa na kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa ajili ya mafunzo ya ufundi mitambo kama mhandisi wa mitambo.
Leo, anafanya kazi kama Mratibu 2 – katika idara ya inayoundwa na timu ya wahandisi. Anafurahi kuwa sehemu ya kampuni hiyo inayojitolea kuwajibika kwa kwa jamii kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo zaidi wafanyakazi wake bila kujali jinsia huku ikiendelea na shughuli za uchimbaji madini mkoani Geita.
Katika GGML, Siah amepata fursa ya kufanya kazi katika miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubuni na kutekeleza ufumbuzi wa nishati endelevu.
Akiwa jaji katika maonesho hayo ya TAWECE 2023 yaliyofanyika Visiwani Zanziba, Siah alitunukiwa jukumu hilo muhimu katika kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake vijana kutimiza ndoto zao katika fani ya uhandisi.
Alikagua miradi ya uhandisi iliyowasilishwa na wahandisi wachanga wa kike na kutoa maoni na mwongozo muhimu kwao ili kupiga hatua kumfikia n ahata zaidi yake.
Siah alifurahishwa na mawazo ya kiubunifu yanayoibua suluhu kwa matatizo mbalimbali ya jamii. Alishuhudia mawazo muhimu ya kibunifu kama vile miradi ya uzalishaji wa nishati ya inayotokana na jua (solar power), pikipiki za kiubunifu za matairi mawili zinazotumika katika kusafirisha abiria mijini na programu nyingine za kurahisisha maisha kwa binadamu.
Miradi hii ilionyesha uwezo wa uhandisi kushughulikia changamoto za ulimwengu halisi na kuboresha maisha ya watu.
Siah alijivunia kuwa sehemu ya hafla hiyo iliyopinga dhana potofu za kijinsia na kuvunja vizuizi dhidi ya wanawake kuingia kwenye fani ya uhandisi.
Siah anaamini kwamba matukio kama vile TAWECE ni muhimu katika kuhamasisha wanawake na wasichana wengi zaidi kufuata taaluma ya uhandisi, kuondokana na dhana potofu za kijinsia ya kwamba baadhi ya fani zinatakiwa kuhusishwa na wanaume pekee.
Ili kuwa mhandisi aliyefanikiwa, unahitaji kuwa na ujuzi na sifa kadhaa muhimu.
Hizi ni pamoja na ujuzi wa kiufundi, ujuzi wa kutatua matatizo, ubunifu na uvumbuzi, ujuzi wa mawasiliano, mawazo bora, usimamizi dhabiti wakati mnafanya kazi ya pamoja.
Pia Siah anasisitiza umuhimu wa uadilifu, uwazi na maendeleo ya kitaaluma, pamoja na haja ya wahandisi kufahamu maendeleo ya sasa yanayoendena na mabadiliko ya teknolojia.
Kama mfano wa kuigwa kwa wahandisi wanawake wanaotarajia kubobea kwenye fani hiyo, malengo ya Siah ni kuboresha ufanisi wa kazi, kuendeleza uvumbuzi na teknolojia, na kutafuta elimu na mafunzo zaidi.
Mradi wa ndoto yake ni kubuni mfumo ambao utaibua utatuzi changamoto mbalimbali zinazoikwamisha sekya ya madini… mradi ambao pia mbali na kuongeza ufanisi kwenye sekta hiyo pia utainufaisha GGML na sekta ya madini kwa ujumla.
Lakinin pia amedhamiri kujiendeleza kielimu, kuwatia moyo wasichana na wanawake wachanga kufuata taaluma ya uhandisi.
Safari ya Siah kama mhandisi wa kike ni msukumo chanya kwa wanawake wote. Kwa msaada wa walimu wake, washauri na mwajiri, ameshinda changamoto na kutekeleza ndoto zake, akiwawezesha wengine waliotaka kuishia njiani.
Historia yake ni ushuhuda wa ushauri unaweza kuwa na nguvu ya kubadilisha maisha ya mtu pindi anapoamua kujitolea na kuongeza bidi katika maisha ya kia siku.
Ushauri alioupata Siah ni kama ukumbusho kwamba wanawake wanaweza kufaulu katika nyanja zinazotawaliwa na wanaume kama vile uhandisi kwenye sekta ya madini.