1.4 C
New York

Serikali yaahidi kuunga mkono kampeni GGML KiliChallenge

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema Serikali itaendelea kuunga mkono kampeni ya GGML KiliChallenge inayolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwani inalandana na jitihada za Serikali kutokomeza maambukizi mapya ya ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Mwanafunzi wa Shule ya msingi kivukoni, Rebecca Damian (14) akikabidhiwa cheti na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama (kushoto) baada ya kufika katika kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro kuhamasisha uchangishaji wa fedha za mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi kupitia kampeni ya GGML KiliChalenge -2023. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong.

Pia amemwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha wanafunzi wawili wa miaka 14 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa siku 7 kupitia kampeni hiyo iliyoasisiwa miaka 22 iliyopita kuingizwa kwenye orodha ya miongoni mwa watu watakaohudhuria sikukuu ya mashujaa ambayo itafanyika Julai 25, mwaka huu.

Kampeni hiyo iliyoasisiwa na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) mwaka 2002 pia inalenga kuisaidia Serikali kutimiza malengo ya kitaifa ya kufikia sifuri tatu – kutokuwa na maambukizi mapya, kutokuwa na unyanyapaa na ubaguzi, na kutokuwa na vifo vitokanavyo na Ukimwi.

Akizungumza katika hafla ya kuwapokea washiriki 35 waliopanda mlima Kilimanjaro na 26 waliouzunguka mlima huo kwa baiskeli mwishoni mwa wiki wilayani Moshi, Mhagama alisema GGML imeonesha kitendo cha kishujaa kuratibu kampeni hiyo kwa miaka zaidi ya 22.

“Kwa hiyo GGML kujitoa kubeba maumivu ya siku saba kwa ajili ya maumivu ya watanzania, hili jambo hili ni la kijasiri, la kishujaa litaendelea kukaa kwenye vitabu vya mambo ya msingi yaliyofanywa na taasisi zetu nchini. Kwa mfano huu mzuri uliooneshwa na GGML napenda kuwaambia hongereni sana,” alisema.

Alitoa wito kwa mashirika mengine ya kitanzania na ya kimataifa kuiga mfano wa GGML kuihudumia jamii kwa moyo wa dhati na kujitoa.

Aidha, aliwapongeza washiriki pamoja na watoto hao waliopanda mlima tarehe 14 Julai mwaka huu na kushuka Julai 20, na kusisitiza kuwa ni mashujaa ambao mafanikio yao yamedhihirisha kuwa mwitikio dhidi ya VVU na Ukimwi unawezekana iwapo kutakuwa na dhamira ya dhati kwa kila Mtanzania kutokomeza janga hilo nchini.

Mmoja kati ya wanafunzi hao ambaye alifanikiwa kupanda mlima Kilimanjaro na kufika katika kilele cha uhuru ni Rebecca Damiani(14) mwanafunzi wa shule ya msingi Kivukoni na Abel Musa(14) mwanafunzi  wa shule ya msingi Mbugani ambaye alirudia njiani baada ya kuugua malaria akiwa mlimani.

Wanafunzi hao ni wanatoka katika kituo cha Moyo wa Huruma – Geita ambacho kinalea watoto wanaoishi katika mazingira magumu chini ya ufadhili wa GGML.

Mhagama alisema watoto hao wameonyesha uzalendo mkubwa kwa Taifa kwa  kujitosa kuungana na watanzania wengine katika kuchochea nguvu ya mapambano dhidi ya maambukizi mapya  ya virusi vya Ukimwi nakwambia wanapaswa kutambuliwa kama mashujaa katika nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong akizungumza katika hafla ya mapokezi ya washiriki 61 walipanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuhamasisha uchangishaji wa fedha za mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi kupitia kampeni ya GGML KiliChalenge -2023.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong aliishukuru serikali kwa kuunga mkono katika mapambano hayo nakuhakikisha zinapatikana fedha kwa ajili ya kutokomeza janga la Ukimwi hapa nchini.

Aidha, aliwapongeza watoto hao kwa rekodi ya kipekee waliyoiweka na kuahidi kuwa GGML itaendelea kuwaunga mkono katika kutimiza ndoto zao.

Waendesha baiskeli 26 walipanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuhamasisha uchangishaji wa fedha za kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi kupitia kampeni ya GGML KiliChalenge -2023.

Kaimu Mkurugenzi Tacaids, Jerome Kamwela  aliwapongeza wapanda mlima hao na kusema wamekuwa mabalozi wazuri katika kuendeleza mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi hapa nchini.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img