1.4 C
New York

Makala| Wananchi wanavyoteswa na Watendaji wadanganyifu

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

MACHI, 2022, Zahanati ya Ihumwa mjini Dodoma, iliweka wazi changamoto ya uhaba wa magodoro katika wodi ya wazazi. Unaizungumzia zahanati iliyoko makao makuu ya nchi.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Aisha Abubakary, haikuwa uchache wa magodoro tu, bali pia wodi hiyo ni ndogo, hivyo kutoweza kuchukua wanawake wote wanaotarajia kujifungua na wale ambao wametoka kujifungua.

Ni katika mazingira hayo, wanawake wanaojifungua kawaida (bila upasuaji) huruhusiwa chini ya saa 24 hadi 48, jambo ambalo ni kinyume cha mapendekezo ya kitaalamu.

“Kutokana na idadi ya wajawazito wanaojifungua kila siku na uhaba wa magodoro na ufinyu wa chumba, inatulazimu kuwaruhusu wengine waliojifungua kurudi nyumbani kabla ya ule muda wa saa 24 hadi 48 unaoshauriwa kitaalamu,” anasema Aisha.

Hata hivyo, Zahati hiyo inalazimika kufanya hivyo ili kutoa nafasi kwa wanawake wengine wenye uhitaji.

“Hivi sasa chumba hiki ni kidogo sana, lakini pia kina magodoro mawili tu na akina mama wanaojifungua kila siku ni wastani wa wanne hadi watano.

“Hili eneo lina watu 12,642 ambao wanaitegemea zahanati hii, lakini kila mwaka zaidi ya akina mama 427 wanapatiwa huduma ya kujifungua hapa,” anasema.

Kwa mujibu wa Aisha, kero nyingine ni kukosekana kwa chumba cha maabara. hivyo kuwalazimu kubeba vipimo kila siku kupeleka katika hospitali nyingine kwa uchunguzi.

“Jengo la maabara lipo lakini halijakamilika. Ni nguvu za wananchi walijiotolea na kuanzisha ujenzi na lilitarajiwa kuanza kutumika mwaka jana lakini hadi sasa bado halijakamilika,” anasema Aisha na kutaja kero zingine kuwa ni ufinyu wa chumba, upimaji na kukosekana kwa uzio.

Ofisa Muuguzi wa zahanati hiyo, Tabitha Nyansika, anasema wanashukuru baadhi ya wadau wanaojitolea misaada ya magodoro kwa kuwa awali walikuwa na matatu, moja OPD na mawili wodi ya wazazi, hali iliyokuwa ikisababisha wajawazito kupata wakati mgumu wanapojifungua.

“Walikuwa wanajifungua kwa kupokezana. Sasa unakuta wakati fulani inatokea wanakwenda kwa pamoja, hivyo inabidi uwaruhusu kurudi nyumbani kabla ya muda wa kitaalamu wa saa 24 hadi 48, ili kutoa nafasi kwa wengine kujifungua,” anasema Nyansika.

Wakati hali ikiwa hivyo, Tamko la Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ni kwamba: “Serikali itasimamia upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, samani pamoja na mitambo husika katika vituo vya kutolea huduma za afya.”

Ripoti ya CAG inaeleza nini?

Kwa upande mwingine, wakati Zahanati ya Ihumwa ikikabiliwa na uhaba wa magodoro na huduma zingine muhimu, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka 2021/2022 imefichua ucheleweshwaji wa kukamilika na kutoanza kwa ujenzi wa vituo vya afya nchini.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere. Picha | Tovuti ya Mwananchi

“Katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 91 zilipokea jumla ya Sh bilioni 82.59 kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati.

“Hata hivyo, tathmini yangu kwenye utekelezaji wa mikataba, kupitia taarifa za utekelezaji na kutembelea maeneo ya ujenzi, ilionyesha ucheleweshaji katika ukamilishaji wa kazi za ujenzi wa vituo husika kwa kipindi kinachoanzia miezi mitatu hadi miaka mitatu,” inabainisha ripoti ya CAG.

Aidha, kile kinachoigusa moja kwa moja Zahanati ya Ihumwa ni kwamba miongoni mwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizochelewa kukamilisha miradi ya vituo vya afya na zahanati ni Jiji la Dodoma.

Akizungumzia hilo, mwandishi wa habari mwandamizi jijini Dodoma,Ramadhan Hussein, anasema Zahanati hiyo ingeweza kuepuka changamoto zinazoikabili endapo watumishi wangeitendea haki miradi hiyo.

“Ripoti ya CAG inaonesha wazi kwamba uzembe umesababisha kukwama kwa baadhi ya maendeleo katika sekta ya afya. Tunaweza kuitaja Zahanati ya Ihumwa lakini uzembe huo umesababisha vituo vingi vya afya kuwa kwenye hali mbaya. Hili halikubaliki,” anasema Hussein.

Aidha, Ripoti hiyo ya CAG iliyowasilishwa mbele ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Machi 29, mwaka huu, inaongeza kuwa miradi ya ujenzi wa vituo vya afya iliyokamilika yenye thamani ya Sh bilioni 4.93 katika Mamlaka 16 za Serikali za Mitaa haikuanza kutumika.

Ripoti hiyo inaeleza: “Miradi iliyokamilika lakini haitumiki inajumuisha majengo ya upasuaji, vyumba vya kuhifadhia maiti, wodi, zahanati na vituo vya afya.

“Miradi hiyo haitumiki kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa tiba vinavyohitajika, ukosefu wa wafanyakazi na miundombinu mingine.”

Kwa upande mwingine, wakati Zahanati ya Ihumwa ‘ikilia’ na changamoto lukuki, Ripoti ya CAG inaeleza kuwa fedha za hospitali kiasi cha Sh Bilioni 20.66 zinashikiliwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) bila kusambaza dawa na vifaa tiba.

“Kanuni ya 140(3) na 141(3) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma (2013) zinaitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kununua na kusambaza vifaa vya katalogi na visivyo vya katalogi ambavyo vinahitajika mara kwa mara kwa kipindi fulani,” inaeleza Ripoti hiyo.

Katika hatua nyingine, madudu hayo yanakuja huku Bajeti ya Wizara ya Afya kwa miaka mitano ya fedha ya hivi karibuni (2018/19, 2022/23), ikiwa ni wastani wa asilimia 5.8 tu.

Wakati hali ikiwa hivyo, Farid Mussa, mkazi wa Wilaya ya Bahi, anasema Zahanati ya Ihumwa ni sehemu ndogo tu ya hali mbaya iliyoko katika sekta ya afya jijini Dodoma.

“Hapo tumeigusa hiyo lakini ukweli ni kwamba watumishi wasio waaminifu wameifanya sekta ya afya kuwa kwenye hali mbaya sana. Leo hii, unakuta hospitali haina dawa lakini zinauzwa katika duka la nje ya hospitali hiyo.

“Unabaki ukijiuliza, imewezekana vipi kwa mfanyabiashara huyo wa duka la dawa kupata dawa ambayo Serikali imeikosa? Lazima tuondokane na janjajanja iliyopo kwenye sekta ya afya,” anasema.

Aidha, maoni yake hayo yanaungwa mkono na Baraka Femba (30), mkazi wa Nanenane, ambaye anaitolea mfano Zahanati ya Ihumwa na kusema bado vifaa tiba ni changamoto kubwa katika sekta ya afya.

“Afya ya rasilimali watu wake ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote lile duniani. Hii ya kukosa maabara haiishii Ihumwa tu, iko kwenye zahanati nyingi, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali,” anasema Femba.

Nini kifanyike?

Akipokea ripoti ya CAG, Rais Dk. Samia anasema: “’Stupid’, wapumbavu, watupishe. Hatuwezi kwenda hivyo na nadhani hawa wanaopokea hizo ‘invoice’ wakazileta kwa raha zao kabisa Serikalini watupishe. Hawafai kuwa kwenye hizo nafasi, kama wanafaa angepokea huko na angehoji.”

Akizungumzia ripoti hiyo na kutoa maoni yake, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anasema:  “Tuonavyo sisi, mambo ni yaleyale, yakifanywa na watu walewale na bila shaka yoyote na chama kilekile.

“Serikali ya Rais Samia ina mtihani mmoja tu, nao ni kusafisha urathi (legacy) wa maamuzi ya ovyo ya nyuma na kujenga mfumo madhubuti wa taasisi ambao utazuia ubadhirifu wa fedha za umma.

Wakati huo huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIBU inayojihusisha na masuala ya uwazi na uwajibikaji, anasema:

“Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iwachukulie hatua za kinidhamu wakurugenzi na watendaji mbalimbali waliofanya matumizi yasiokuwa na tija kwenye Halmashauri husika.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), anasema:

“Tatizo ni hivi; watu waliopewa dhamana ya kusimamia ndiyo changamoto, hata tutengeneze sheria nzuri kiasi gani, bado watu hawajifunzi. Watu hawathamini kabisa fedha hizi za umma ambazo ni mali ya wananchi, hawana uchungu kabisa.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img