1.7 C
New York

Dk. Kikwete kuwaaga wapanda mlima 61 Kampeni ya GGML KiliChallenge-2023

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

RAIS mstaafu Dk. Jakaya Kikwete kesho Ijumaa Julai 14, 2023 anatarajiwa kuwaaga jumla ya washiriki 61 watakaopanda mlima Kilimanjaro kupitia kampeni ya ‘GGML KiliChallenge -2023’ inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na kuendeleza mapambano ya kutokomeza Virusi Vya Ukimwi (VVU).

 Kampeni hiyo iliasisiwa mwaka 2002 na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML kwa ushirikiano na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS).

Taarifa iliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda imeeleza kuwa baada ya Dk. Kikwete kuwaaga washiriki hao katika lango la Machame Julai 14, watapokewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu katika lango la Mweka Kibosho Julai 20 mwaka huu saa 3 asubuhi.

Aidha, akifafanua kuhusu kampeni hiyo, Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema mwaka huu jumla ya washiriki 35 watapanda mlima huo kwa njia ya kawaida ilihali washiriki 26 wataupanda mlima kwa kutumia baiskeli.

Alisema katika kampeni hiyo kutakuwa na utolewaji wa huduma bure za upimaji wa VVU, ushauri nasaha na kujitolea kutoa damu.

Mbali na kuishukuru Serikali kwa kuunga mkono kampeni hiyo iliyoasisiwa mwaka 2002, Shayo alisema  wakiwa wadau wa mapambano haya ya UKIMWI na VVU, GGML imepokea msaada ambao uliiwezesha Kili Challenge kupiga hatua kubwa hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20.

Fedha hizo ambazo hukusanywa kila mwaka, hulenga kuchangia juhudi za serikali ya Tanzania katika jitihada zake kufikia malengo ya sifuri tatu yaani kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img