1.4 C
New York

‘Viumbe vamizi vinatishia ustawi sekta ya utalii nchini’

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Changamoto ya viumbe vamizi katika nyanja ya uhifadhi imetajwa kama moja ya sababu inayodhorotesha ustawi wa sekta ya utalii na maendeleo kwa ujumla nchini Tanzania.

Hayo yemebainishwa Dar es Saalam leo Juni 21, 2023  na Mtaalamu kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Joseph Olila, wakati wa Mjadala wa kujadili Changamoto za viumbe vamizi kwenye uhifadhi na maendeleo ya jamii ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini(JET).

Kwa mujibu wa Olila, viumbe vamizi vinahusisha aina ya mimea, wanyama au kiumbe chochote kile ambacho kimeletwa kwa mara ya kwanza na kinakuwa vamizi pale kinapoleta uharibifu.

“Kimazingira kiumbe vamizi kinatabia ya kuleta changamoto ikiwamo kuondoa viumbe vilivyokuwapo awali kwa kuchukua nafasi zao. Hii pia inasababisha uharibifu wa eneo la asili kama uotoa wa asili, hivyo kwa namna moja ama nyingine viumbe vilivyopo vitaathirika,” amesema Olila na kuongeza kuwa:

“Kuna changamoto ya kimazingira ambapo husababisha magonjwa kwani viumbe asili vinakuwa havina kinga wala kuandaliwa kibiolojia kumudu changamoto hiyo,” amesema.

Akizungumzia changamoto za kijamii amesema kuwa viumbe vamizi vinatabia ya kuvuruga mimea, kusababisha magonjwa na kwamba changamoto hizi zote zinahusiana na zinategemeana.

“Mfano kuna changamoto za kiuchumi. Hii tunaona kwamba gharama za kuwadhibiti viumbe hawa ni kubwa sana kwani zinahusisha vifaa na watu, hivyo vinapoingia kwenye mfumo wako wa uzalishaji gharama za kudhibiti zinakuwa kubwa sana.

“Pia inaathiri sana utalii, kwani inapotokea kwa muda mrefu kuwa viumbe vamizi wanyama wanapungua jambo ambalo linapunguza watalii kwani mazingira asili yanakuwa yametoweka.

“Hii ni sambamba na kwenye kilimo ambapo wanapoingia wanakuwa wanachochea gharama za kuondoa viumbe hivi,” amesema Olila.

John Noronha-Meneja Ufuatiliaji kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Akizungumza namna ya kudhibiti viumbe hivyo, John Noronha ambaye ni Meneja Ufuatiliaji kutoka Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili amesema, kwanza ni kuhakikisha kuwa viumbe hivyo haviwezi kuingia kwenye mfumo wa uzalishaji

“Sababu ya kuzuia ushamiri wa viumbe hivi ni pamoja na kutokuwapo kwa viumbe ambavyo vinamtegemea kwa chakula. Pia kutoa uelewa mpana kwa jamii na wadau wengine juu ya viumbe hivi.

“Matharani kuna viumbe kama Siam Weed huyu ndiye kiumbe anayesumbua kwa kiwango kikubwa katika sekta ya wanyama nchini Tanzania, hivyo ni wajibu wetu kuendelea kutoa elimu,” amesema Noronha huku akitaja baadhi ya wanayama wanaosababisha mgongano kama Tembo, Simba, Fisi na wengine.

“Sambamba na hayo pia bado kuna changamoto ya upungufu wa sheria, mfano: kama wewe umelima kwenye kingo ya hifadhi basi hautafidiwa, vitu kama hivi vinapaswa kuangaliwa,” amesema.

Mhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda maalum ya Dar es Salaam, Msafiri Kasara(aliyesimama) akifafanua jambo kwenye mjadala huo.

Upande wake, Mhifadhi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda maalum ya Dar es Salaam, Msafiri Kasara amesema wameendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan walioko katika Wilaya zenye mapori hatua ambayo imesaidia kuimarisha ulinzi.

“TAWA tumeweka utaratibu kwamba asilimia 25 ya pato ambalo linapatikana katika pori linalozunguka wananchi linakuwa ni la kwao.

“Hivyo, mwananchi haoni haja ya kufanya ujangili na hadi kufikia sasa Sh bilioni 37 zimetumika kwa ajili ya malipo hayo, mbali na hilo tumeweka kipaumbele cha huduma muhimu kama shule, zahanati na nyingine,” amesema.

Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru.

Awali, Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru, akifungua mjadala huo alisema mafunzo ya bayonuai ni muhimu sana katika uhifadhi wa mazingira nchini.

“Tunafundisha jamii na kuelimisha pia kuhusu sera, lengo likiwa ni kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi katika uhifadhi wa bayonuai kupitia vyombo vya habari,” amesema Dk. Otaru.

JET imekuwa na utaratibu wa kukutana makundi mbalimbali yakiwamo ya wanahabari kwa ajili ya kuwajengea uelewa kuhusu nyanja tofautitofauti zinazohusu mazingira nchini.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img