22.9 C
New York

Chart| Hali ya ukosefu wa chanjo kwa watoto Kusini na Mashariki mwa Afrika

Published:

Na Hassan Daudi, Gazetini

Ripoti ya Mwaka ya Hali ya Watoto Duniani iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) inayofahamika kama “State of the World’s Children” inaonyesha kuwa hali bado ni tete zaidi maeneo ya vijijini Kusini mwa Jangwa la Sahara katika utoaji chanjo kwa watoto ikilinganishwa na mijini.

Mfano katika nchi ya Ethiopia ambayo ndiyo kinara, ukosefu wa chanjo kwa watoto katika maeneo ya vijijini ni asilimia 50.6 huku kwa mijini ikiwa asilimia 18.5.

Upande wa Tanzania pamoja na kufanya vizuri katika utoaji wa chanjo lakini bado takwimu haziibebi ikilinganishwa na nchi kama Burundi.

Takwimu zinaonyesha kuwa ukosefu wa chanjo kwa watoto Tanzania ni asilimia 3.9 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 1 kwa mijini huku Burundi ikiwa na asilimia 0.8 kwa vijijini na 0.9 kwa mijini.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa chanjo ina tija kubwa katika maisha ya binadamu. Tafiti zinaonesha kuwa vifo vingi vitaepukika endapo Ajenda ya Chanjo ya mwaka 2030 itafanikiwa. Mkakati wa kidunia ni kuhakikisha ‘kila mtu, kokote aliko, kwa umri alionao, anafaidika na chanjo kwa ustawi wa afya yake’.

Aidha, kwa watoto, faida kubwa ya chanjo ni kuwawezesha kuepuka changamoto ya maradhi mbalimbali. Kwa karne ya 20 pekee, magonjwa ya watoto yamesababisha vifo zaidi ya milioni 300 duniani kote. Hata hivyo, kuondosha polio ni moja ya mafanikio makubwa ya chanjo.

Kwa upande mwingine, nguvu ya chanjo ilionekana wakati wa janga la Uviko-19. Ugonjwa huo uligharimu maisha ya watu milioni 14.9 kuanzia mwaka 2020 hadi 2021, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Licha ya kuchukua muda mrefu kwa chanjo ya Uviko-19 kufika, takwimu zinathibitisha kuwa nchi masikini nazo zimefaidika, huku ikielezwa kuwa zimeepusha vifo zaidi ya milioni 20 duniani kote.

Ukiacha hiyo ya Uviko-19, takwimu zinaonesha kuwa watoto milioni 67 duniani walikosa chanjo mbalimbali kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.

Kwa Mashariki na Kusini mwa Afrika, watoto waliokosa chanjo kwa kipindi hicho ni milioni 4.6, ambapo wengi kati yao walishavuka umri wakati chanjo hizo zikitolewa. Somalia ni moja ya nchi zilizo nyuma zaidi.

Aidha, athari za ukame na njaa zimesababisha watoto nchini Somalia kuwa kwenye hatari ya magonjwa, ikiwamo surua. Kuanzia Januari 2022 hadi Oktoba, asilimia 75 ya wagonjwa wa surua nchini humo walikuwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Nasro Dire, raia wa Somalia anayeishi katika kambi ya watu wasio na makazi ya Jawle, ni mama wa watoto wanne ambapo anasema kufiwa na watoto wake wawili kulimfanya aone umuhimu wa chanjo.

Dire mwenye umri wa miaka 23, anasimulia akisema watoto hao, Aanas wa umri wa miaka miwili na Masude aliyekuwa na mwaka mmoja, walianza kusumbuliwa na homa mwanzoni mwa mwaka 2022.

“Walifariki kwa kupishana mwezi mmoja,” anasema Dire, akiongeza kuwa vifo hivyo vilimsukuma kuwapa chanjo watoto wake wote watatu waliobaki. “Kilichotokea kwa watoto wangu kilinisukuma kuwalinda hawa wengine,” anasema.

Mbaya zaidi, wakati mwamko ukionekana kuwa chini Mashariki na Kusini mwa Afrika, dunia imeendelea kushuhudia na kugubikwa na mlipuko wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Itakumbukwa, kwa mwaka 2022 pekee, nchi 11 kati ya 23 za Mashariki na Kusini mwa Afrika zilikumbana na changamoto ya magonjwa ya surua, kipindupindu na virusi vya polio.

Vilevile, kuliacha nyuma kundi la watoto kunaathiri moja kwa moja matarajio ya Taifa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Ifahamike kuwa chanjo ni nyenzo muhimu ya SDGs, ambapo inasisitiza ‘Kuhakikisha maisha na afya bora kwa watu wa rika zote’.

Kile kilichoelezwa na ripoti ya State of the World’s Children ya mwaka 2023 ni kwamba zipo sababu mbalimbali, zikiwamo za kiuchumi, zinazochochea mwamko mdogo wa chanjo ya watoto, hasa katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, ikiwamo Somalia.

Ripoti hiyo inaanisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa watoto wa familia masikini kupata chanjo. Tofauti hiyo inaweza kuwapo pia kati ya watoto wa maeneo ya vijijini na wenzao wa mijini.

Katika hatua nyingine, ripoti hiyo inaweka wazi kuwa uelewa wa wazazi ni sababu nyingine, kwamba asilimia kubwa ya wale wasio na elimu hupuuzia chanjo kwa watoto wao.

Aidha, wakati chanjo ikionekana kuwa kwenye mwendo wa kusuasua Mashariki na Kusini mwa Afrika, takwimu za dunia zinayataja maeneo mawili hayo kuwa ndiyo kinara wa ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.

Lakini, licha ya kwamba ugonjwa huo ni wanne wa kusababisha vifo vingi duniani, bado mwamko wa chanjo yake iitwayo HPV (The Human Papillomavirus) si wa kuridhisha katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img